Charlie Munger (1924 – 2023), aliyekuwa bilionea mwekezaji na mshirika wa karibu wa Warren Buffet amefariki dunia tarehe 28/11/2023 akiwa na umri wa miaka 99.



Kwa miaka zaidi ya 50 ambayo wamefanya kazi na Warren Buffet, alikuwa mchango mkubwa kwenye kuijenga kampuni ya Berkshire Hathaway.

Munger pia alikuwa akifundisha na kushauri kuhusu mafanikio kwenye biashara, uwekezaji na maisha kwa ujumla.

Mpaka anafariki dunia akiwa na miaka 99, Munger bado alikuwa anafanya kazi kama makamu mwenyekiti wa kampuni ya Berkshire Hathaway.

Nilimchagua Charlie Munger kuwa mmoja wa mamenta wangu kwa sababu kubwa tatu;
1. Alikuwa bilionea, ambalo ni moja ya malengo yangu makubwa ambayo lazima niyafikie kwenye maisha.
2. Alikuwa anapenda sana kujifunza hasa kwa kusoma, kitu ambacho nimekuwa nafanya pia na ndiyo kimenifikisha hapa nilipo na nina uhakika kitanifikisha kule ninakotaka kufika.
3. Ameishi miaka mingi (99) huku akiwa anaendelea kufanya kazi mpaka anakufa, lengo langu ni kuishi miaka isiyopungua 100 huku nikiendelea kufanya shughuli zangu bila kuacha mpaka nakufa.

Hekima za Charlie Munger.

Munger amekuwa akinukuliwa sana kwenye hekima nyingi alizokuwa anashirikisha.

Hapa nimeshirikisha nukuu 99 zenye hekima kubwa kutoka kwenye miaka 99 ya Charlie Munger.
Karibu tujifunze na kuzitumia ili kuwa na maisha bora.

1. “Sheria tatu za kazi: (1) Usiuze kitu ambacho wewe mwenyewe haupo tayari kukinunua; (2) Usimfanyie kazi mtu ambayo humheshimu na kumkubali; na (3) Fanya kazi na watu unaowafurahia tu.”

2. “Usiwe na wivu, usiwe na chuki, usitumie zaidi ya kipato chako, kuwa na shauku licha ya changamoto unazokuwa nazo, jihusishe na watu wanaoaminika na fanya kile unachopaswa kufanya. Sheria hizi zote zinafanya kazi vizuri sana kuyafanya maisha yako kuwa bora.”

3. “Uzoefu wangu kwenye maisha ni kama utakuwa mtu wa kusoma na kufikiri kwa kina, hutahitaji kufanya kazi.”

4. “Sijawahi kufanikiwa kwenye kitu ambacho sikuwa nakipenda. Kama hukipendi sana kile unachofanya, huwezi kufanikiwa kupitia hicho, hata kama una akili nyingi kiasi gani.”

5. “Ni bora kujihusisha na watu wachache unaowaamini na kuachana na wengine wote. Hili linapaswa kufundishwa kama kateksimo. Watu wenye hekima huwa wanawaepuka wale wenye kisirani, na watu wa aina hiyo ni wengi.”

6. “Angalia hiki kizazi chenye vifaa vingi vya kielektroniki na kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Naweza kutabiri kwa kujiamini kitakuwa na mafanikio kidogo kuliko Warren anayetumia muda wake kusoma. Kama unataka hekima, utaipata kwa kukaa chini na kusoma. Hivyo ndivyo inavyokuja.”

7. “Kwenye ndoa, usiangalie mtu mwenye sura nzuri na tabia. Bali angalia mtu mwenye matarajio madogo.”

8. “Kinachoendesha dunia siyo tamaa, bali wivu.”

9. “Kwenye maisha yangu yote, sijawahi kumjua mtu mwenye hekima ambaye hasomi muda wote – hayupo kabisa. Utashangazwa sana na jinsi ninavyosoma zaidi. Watoto wangu huwa wananicheka. Wanafikiri mimi ni kitabu chenye miguu.”

10. “Nimekuwa ninaona watu wanaofanikiwa sana kwenye maisha, siyo wenye akili sana, wala siyo wachapakazi sana, lakini ni mashine za kujifunza. Wanalala wakiwa na hekima zaidi ya waliyokuwa nayo wakati wanaamka, na hilo linasaidia sana hasa pale unapokuwa na muda mwingi mbele yako.”

11. “Tamaa ya kupata utajiri kwa haraka ni hatari.”

12. “Kama unataka kufanikiwa kwenye uwekezaji, anza mapema, weka juhudi na endelea kufanya bila kuacha. Mafanikio yote huja kwa njia hiyo.”

13. “Nafikiri maisha ambayo mtu ameishi kwa usahihi ni ya jifunze, jifunze, jifunze muda wote.”

14. “Sheria ya kwanza ya maisha ya furaha ni kuwa na matarajio madogo. Unapaswa kuwa na matarajio kiasi na kupokea matokeo ya maisha, mazuri na mabaya kama yanavyokuja kwa kiwango cha Ustoa.

15. “Nilipenda sana kuwa tajiri, siyo kwa sababu nilitaka Ferrari – bali kwa sababu nilitaka uhuru.

16. “Binadamu wote huwa wanafanya kazi vizuri pale wanapopata motisha.”

17. “Kitu bora ambacho binadamu yeyote anaweza kufanya ni kuwasaidia binadamu wengine kujua zaidi.”

18. “Inashangaza mafanikio makubwa na ya muda mrefu watu kama sisi tumeyapata kwa mara zote kuepuka kuwa wapumbavu badala ya kujaribu kuwa na akili kubwa.”

19. “Nimejikataza kuwa na maoni kwenye kitu chochote ambacho siwezi kukielezea vizuri kuliko upande wa pili unavyoweza kukielezea.”

20. “Pesa kubwa haipo kwenye kununua na kuuza, bali ipo kwenye kusubiri.”

21. “Huhitaji kuwa na akili kubwa, bali hekima kidogo zaidi ya wengine, kwa wastani, kwa muda mrefu zaidi.”

22. “Sheria ya kwanza ya uvuvi ni kwenda eneo ambalo samaki wapo. Sheria ya pili ya uvuvi ni kukumbuka sheria ya kwanza.”

23. “Tunafanikiwa siyo kwa sababu tuko vizuri kwenye kutatua matatizo, bali kwa sababu tupo vizuri kwenye kuyaepuka. Tunaangalia mambo ambayo ni rahisi kwetu kufanya.”

24. “Unachohitaji siyo kuchukua hatua nyingi, bali kuwa na subira kubwa. Unapaswa kusimamia misingi yako na pale fursa zinapojitokeza, unazinyakua.”

25. “Kupata mafanikio haiwezi kuwa rahisi. Kama inakuwa rahisi sana kwako, uwezekano ni kuna hatua muhimu unaziruka.”

26. “Tuna makapu matatu kwenye uwekezaji; NDIYO, HAPANA na NGUMU kwetu kuelewa.”

27. “Geuza, mara zote geuza; Geuza hali au tatizo juu chini, angalia mbele na nyuma.”

28. “Huwa naachana na watu wanaojibu maswali kwa kujiamini kuhusu vitu ambavyo hawana ujuzi navyo.”

29. “Unawezaje kupata mwenza bora? Njia moja bora ni wewe kustahili mwenza bora.”

30. “Kufuata mkumbo huwa kuna tabia ya kuleta matokeo ya kawaida.”

31. “Marejesho unayopata siyo muhimu kama kuepuka kupoteza kila kitu.”

32. “Ishi chini ya kipato chako na weka akiba ili kuwekeza. Jifunze yale unayopaswa kuyajua.”

33. “Ielewe nguvu ya riba mkusanyiko.”

34. “Kumbuka sifa yako na uadilifu ndiyo mali zenye thamani kubwa kwako na unaweza kuvipoteza mara moja.”

35. “Chukua wazo moja rahisi na lichukulie kwa uzito mkubwa.”

36. “Sikuzingatia mipaka ya kitaaluma, badala yake nilijifunza kila nilichotaka kujua.”

37. “Mchezo wetu ni kugundua wazo kubwa linapokuja hasa pale inapopita muda wazo la aina hiyo halijaja.”

38. “Subira ndiyo inakusaidia kama mwekezaji na watu wengi hawana subira.”

39. “Kama huna vinasaba vya kuzuia tamaa ya kupata raha kwa haraka, utahitajika kufanya kazi kubwa sana kuvuka hilo.”

40. “Sikufika kwenye kilele cha mafanikio nilipo kwa kukimbizana na fursa za kawaida.”

41. “Watu wengi wenye akili kubwa huwa ni wawekezaji wabovu.”

42. “Dunia imejaa wacheza kamari wapumbavu, lakini hawatafanya vizuri kama wawekezaji wenye subira.”

43. “Watu wanakokotoa sana na kufikiri kidogo.”

44. “Ubepari bila kushindwa ni sawa na dini bila jehanamu.”

45. “Kujua usichojua ndiyo chanzo cha hekima.”

46. “Mara zote huwa nasema ninachotaka kujua ni wapi nikienda nitakufa ili nisiende hapo.”

47. “Kujifunza endelevu ni muhimu, kushindwa kufanya hivyo ni kujiweka kwenye upande wa kushindwa.”

48. “Huwezi kuishi maisha kamili bila ya kufanya makosa.”

49. “Sheria ya chuma ya asili ni; unapata kile unachotuza.”

50. “Sheria ya kwanza ya riba mkusanyiko ni kutokuvuruga bila sababu.”

51. “Nimefanikiwa kwa sababu nina uzingatiaji mkubwa kuliko wengine.”

52. “Sehemu kubwa ya makosa kwenye maisha yanasababishwa na mtu kusahau anachojaribu kufanya.”

53. “Hakuna rubani makini, hata awe na kipaji na uzoefu kiasi gani, ambaye atapuuza nguvu ya orodha ya mambo ya kuzingatia.”

54. “Wivu ndiyo dhambi ya kijinga kwa sababu ndiyo dhambi pekee ambayo hupati raha wakati wa kuifanya. Inakupa maumivu makubwa bila ya raha yoyote, kwa nini utake hilo?”

55. “Kumbuka sheria ya Louis Vincenti: ‘Sema ukweli na hutahitaji kukumbuka uongo wako.’”

56. “Usikubali janga moja kwenye maisha yako lizalishe majanga mengine kwa kushindwa kwa nia.”

57. “Maisha yatawaumiza baadhi ya watu kwa namna fulani na kuwasaidia wengine. Unapaswa kuwa tayari kupokea mapigo ya maisha kama yanavyokuja. Hivyo ndivyo maisha yalivyo, na siyo kulalamika muda wote.”

58. “Silaha bora ya umri wa uzee ni maisha mazuri unayotangulia kuyaishi kabla ya uzee.”

59. “Watu wengi wamefundishwa kwenye eneo moja tu – kwa mfano uchumi – halafu wanajaribu kutatua matatizo yao yote kwa njia hiyo. Unaujua usemi; Kwa mtu mwenye nyundo, dunia inaonekana kama msumari. Hii ni njia mbovu ya kuyakabili matatizo yako.”

60. “Nazidi kupata uzoefu kadiri ninavyozeeka. Ni sawa na mtu aliyeruka kutoka ghorofani na akiwa ghorofa ya tano kufika chini anasema; hata hivyo safari siyo mbaya.”

61. “Tunajifunza, kuboresha na kuharibu mawazo mara zote. Kuharibu mawazo yako kwa haraka pale inapobidi kufanya hivyo ni moja ya sifa bora unazoweza kuwa nazo. Unapaswa kujilazimisha kuzingatia hoja za upande wa pili.”

62. “Kitu kingine kinachopaswa kuepukwa ni itikadi kali kwa sababu zinaharibu akili ya mtu.”

63. “Kuwa mtu wa kufanya maamuzi kwa kufikiri ni takwa la kimaadili. Hupaswi kuwa mpumbavu zaidi ya inavyohitajika.”

64. “Kila mwaka unaopita ambao hujaharibu moja ya mawazo yako pendwa ni mwaka ambao umeupoteza.”

65. “Kubobea kwenye mambo machache ndiyo njia ya kufanikiwa. Watu wengi wanaweza kuwa bora kwa kubobea kwenye machache kuliko kutaka kuelewa ulimwengu mzima. Kubobea ndiyo njia ya kufanikiwa.”

66. “Jua mawazo makuu kutoka kwenye tasnia kubwa na yatumie mara zote – yatumie yote na siyo machache.”

67. “Kwenye demokrasia, kila mtu anachukua zamu yake. Lakini kama unataka hekima kubwa, ni bora kuweka umakini kwa mtu mmoja bora kwenye kufanya maamuzi na michakato. Siyo ajali hili limekuwa na matokeo mazuri kwenye nchi kama Singapore kuliko Marekani. Kwa Singapore, mamlaka yaliwekwa kwa mtu mmoja aliyekuwa na uwezo mkubwa, Lee Kuan Yew, ambaye alikuwa ndiyo Warren Buffett wao.”

68. “Kwetu Berkshire hatujawahi kuwa na mpango mkuu. Yeyote ambaye amekuwa anataka kuandaa mpango huo tumekuwa tunamfukuza kwa sababu unajitengenezea maisha yake wenyewe na hauchukui uhalisia mpya. Tunataka watu wanaozingatia taarifa mpya.”

69. “Kwa wastani, kuweka dau kwenye ubora wa biashara ni bora kuliko kuweka dau kwenye ubora wa uongozi wa biashara … lakini, mara chache sana, unakutana na meneja ambaye ni mzuri sana kiasi cha kuwa ni hekima kumfuata kwenye biashara ambayo ni ya kawaida.”

70. “Tofauti kati ya biashara nzuri na biashara mbaya ni kwamba biashara nzuri inafanya maamuzi rahisi moja baada ya nyingine. Biashara mbaya inafanya maamuzi ya kuumiza kila mara.”

71. “Kwa kipindi cha muda mrefu, historia inaonyesha kwamba uwezekano wa biashara kuendelea kuwa hai kwa namna ambavyo inakubalika na wamiliki wake ni mdogo sana.”

72. “Kuna aina mbili za biashara: Ya kwanza inaingiza faida ya 12%, na unaweza kuichukua mwisho wa mwaka. Ya pili inaingiza faida ya 12%, lakini faida yote inabidi kuwekezwa tena kwenye biashara — hakuna fedha inayobaki. Inanikumbusha mtu ambaye anaangalia vifaa vyake na kusema, ‘Hiyo hapo ndiyo faida yangu yote.’ Tunachukia aina hiyo ya biashara.”

73. “Ukichanganya zabibu na kinyesi, bado unakuwa na kinyesi.”

74. “Tunaweka vichwa vyetu chini na kukabiliana na kila linalotujia, mazuri na mabaya, kwa namna bora tuwezavyo, kisha kuchukua matokeo kila baada ya miaka kadhaa.”

75. “Kama ningekuwa naiendesha dunia ningepunguza kodi ya makampuni, kisha kupata usawa kwa njia nyingine, kama kodi ya matumizi.”

76. “Sijali kama mtu anapata fedha nyingi na kuwa bahili. Watu wengi wana matumizi makubwa ya fedha ambayo ni upotevu, wakisaidiwa na wenza na watoto wao.”

77. “Sidhani kama unaweza kuwaamini mabenki kujidhibiti wao wenyewe. Wanafanana na wateja wa dawa za kulevya.”

78. “Kama tunataka kupata mafanikio makubwa, ni lazima tufanye kazi. Lazima watu wasukumwe kwa zawadi na adhabu. Kama utaondoa adhabu, mfumo mzima hauwezi kufanya kazi. Huwezi kutajirika kwa kupiga kura. Ni wazo la kijinga.”

79. “Wakorea walikuja kwenye biashara ya magari wakiwa hawana kitu. Walifanya kazi masaa 84 kwa wiki kwa zaidi ya miaka kumi bila malipo ya ziada. Wakati huo kila mtoto wa Kikorea alipotoka shule alikuwa na mwalimu wa kumfundisha masoko ya ziada kwa masaa yasiyopungua manne, wakisukumwa na mama zao wakali. Je itakushangaza pale watu wa aina hiyo wanapokuzidi? Labda ukiwa mjinga kabisa.”

80. “Popote penye kamisheni kubwa, panakuwa na uwezekano mkubwa wa kuibiwa.”

81. “Ni asili ya soko la hisa kushuka. Hivyo watu huteseka na hilo. Kuwekeza kwa uangalifu na kuweka akiba kwa msimamo bila miujiza ndiyo njia sahihi. Baadhi ya watu wanaweza kujua jinsi ya kuongeza marejesho mara mbili. Siwezi kufundisha watu jinsi ya kufanya hivyo. Ni vigumu sana.”

82. “Mafanikio kwenye uwekezaji yanahitaji muunganiko wa shauku na subira, na kisha kuwa tayari kuchukua hatua kwa haraka pale fursa inapojitokeza, kwa sababu kwenye hii dunia fursa nzuri huwa hazikai kwa muda mrefu.”

83. “Hakuna kanuni moja. Unahitaji kujua sana kuhusu biashara na asili ya binadamu na namba …. Ni ujinga kutegemea kuna mfumo wa miujiza utakaofanya hayo.”

84. “Kama watu wasingekuwa wanakosea mara nyingi kama wanavyofanya, tusingekuwa na utajiri mkubwa ambao tunao.”

85. “Angalia hisa kama umiliki wa biashara na pima ubora wa biashara kudumu kwa kuangalia manufaa yake kiushindani.”

86. “Chukua hatua pale manufaa yanapokuwa upande wako – unapaswa kujua manufaa yalipo na kuwa na nidhamu ya kuweka dau pale unapokuwa na nafasi kubwa ya kushinda.”

87. “Sijawahi kuweza kutabiri kwa usahihi. Sipati fedha kwa kutabiri kwa usahihi. Huwa tunaingia kwenye biashara nzuri na kukaa hapo.”

88. “Uwekezaji wa kukaa na kutulia. Unalipa kidogo kwa madalali, unapunguza kusikiliza ujinga, na kama itafanya kazi, mfumo wa kodi unakupa manufaa zaidi.”

89. “Mchezo wa maisha ni kujifunza kusikokuwa na ukomo, kama unataka kupata ushindi.”

90. “Bila ya kuwa na mfumo mzuri wa kujifunza, unakuwa huna tofauti na kiwete anayeshiriki shindano la kupigana mateke. Mwisho wake hauwezi kuwa mzuri.”

91. “Pata hekima ya dunia na badili tabia yako kuendana na hekima hiyo. Kama tabia yako mpya haitapendwa na wale wanaokuzunguka, achana nao.”

92. “Tuna akili ya kutosha pale kitu kinapofanya kazi vizuri tunaendelea kukifanya. Naweza kusema tunatumia kanuni ya msingi ya maisha – rudia kinachofanya kazi.”

93. “Milili kazi yako na kuza zaidi uaminifu wako.”

94. “Nataka kufikiria kuhusu vitu ambavyo nimewazidi wengine. Sitaki kucheza mchezo ambao wengine wamenizidi uwezo. Sichezi mchezo ambao wengine wana hekima na mimi ni mpumbavu. Naangalia mchezo ambao mimi nina hekima na wao ni wapumbavu. Na niamini kwenye hilo, inafanya kazi vizuri. Mungu awabariki washindani wetu wapumbavu. Wanatufanya kuwa matajiri.”

95. “Hakuna mwalimu mzuri kwenye kuijua kesho kama historia… Kuna majibu yenye thamani ya mabilioni ya dola kwenye kitabu cha historia cha dola 30.”

96. “Wekeza kwenye biashara ambayo hata mpumbavu anaweza kuiendesha, kwa sababu kila biashara kuna wakati itaendeshwa na mpumbavu. Kama biashara haiwezi kuhimili usimamizi mbovu, hiyo siyo biashara.”

97. “Watu wengi wanafikiri kama wakiwa na hisa za makampuni 100 basi wanawekeza kitaalamu kuliko wakiwa na hisa za makampuni manne au matano. Nachukulia huo kama wendawazimu.”

98. “Nafikiri watu wanaofanya zaidi ya jambo moja kwa wakati wanalipa gharama kubwa.”

99. “Nakula ninachotaka kula. Sijawahi kufikiria sana kuhusu afya yangu. Sijawahi kufanya mazoezi ya kujilazimisha. Mafanikio yoyote niliyopata ni kwa sababu nimekuwa nasimamia kufikiri kwa usahihi. Hao watu wote wanaofikiria watafanikiwa kwa kufanya mazoezi ya kukimbia au mengine, nawatakia heri.”

Ni imani yangu kuna mengi ambayo umejifunza kutoka kwenye hekima hizi za Charlie Munger. Sasa nenda kayaweke yale uliyojifunza kwenye matendo ili maisha yako yazidi kuwa bora. Kwa sababu hekima ni pale unapoweka kwenye matendo yale uliyojifunza.

Kwangu binafsi nitazidi kujifunza kupitia maisha ya Charlie Munger na kujipima naye kwa kila ninachofanya ili mara zote nifanye kilicho sahihi na kuepuka makosa yanayoweza kunigharimu sana.
Kila ninapojifunza kupitia Munger, naona jinsi ambavyo malengo makubwa niliyonayo yanawezekana kabisa.

Kupitia kujifunza na kuishi kama Charlie Munger, nina uhakika wa; kuwa Bilionea, kuwa Rais wa Tanzania na kuishi miaka isiyopungua 100 huku nikiwa nafanya shughuli zangu mpaka nakufa.

Kama na wewe rafiki yangu una ndoto na malengo makubwa kwenye maisha yako, karibu tuambatane pamoja kwenye hii safari. Kwani kwa kushirikiana pamoja, malengo hayo makubwa yanakuwa rahisi.
Sehemu pekee ya kushirikiana pamoja ni kwenye jamii ya tofauti ambayo tunaijenga, jamii ya KISIMA CHA MAARIFA.
Hakikisha unakuwa ndani ya jamii hii kwa kipindi chote cha maisha yako.

Huhitaji makubwa kuwa kwenye jamii hii, kitu pekee kinachohitajika ni uwe unapenda hekima. Kwa sababu kanuni yetu kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA ni MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO.
Hivyo tunapata maarifa kwa pamoja, tunayaweka kwenye vitendo kwa kushirikiana na kwa pamoja tunapata mafanikio makubwa.

Kujiunga na jamii hii ya KISIMA CHA MAARIFA, bonyeza maandishi haya (au fungua kiungo hiki; https://t.me/+gR6xX_DvF3c3NmZk)

Karibu sana twende pamoja kwenye hii safari ya kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

Rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr Makirita Amani,
Daktari wa binadamu, Mwandishi, Kocha na Mkufunzi.
http://www.kisimachamaarifa.co.tz

0678 977 007 kupata vitabu
0678 977 007 kupata vitabu