Kufanya ni kitu endelevu, ambacho kinaweza kisiwe na mwisho. Kujenga ni kitu cha muda, ambapo baada ya kukamilisha huhitaji kuendelea tena.
Watu wengi huwa wanaingia kwenye biashara kwa lengo la kupata uhuru wa fedha, muda na maisha kwa ujumla. Lakini mwisho wake wanajikuta wakiwa wamenasa kwenye gereza ambalo hawana pa kutorokea.
Hilo la watu kuwa watumwa wa biashara zao, huwa linasababishwa na mambo mengi. Lakini moja la msingi ni mtazamo ambao mtu anakuwa nao kuhusu biashara.
Ipo mitazamo mikubwa miwili ya kibiashara ambayo inaamua uhuru au utumwa wa mtu kwenye biashara.
Mtazamo wa kwanza ni kufanya biashara. Hapa mtu anachukulia biashara kama kitu cha kufanya na hivyo kinakuwa endelevu kwenye maisha yake. Kwa kuwa lengo ni kufanya, basi mtu anahakikisha anakuwa na vitu endelevu vya kufanya kwenye biashara yake. Na hapo mtu anakuwa amejitengenezea aina nyingine ya ajira. Hivyo ndivyo watu wanavyojitengenezea utumwa kwenye biashara.
Mtazamo wa pili ni kujenga biashara. Hapa mtu anachukulia biashara kama kitu ambacho anakijenga na kikishakamilika anakiacha kiendelee chenyewe. Kwa kuijenga biashara mpaka kufikia ngazi ambayo haimhitaji tena mtu awepo, inampa mtu uhuru mkubwa kwenye maisha yake.

Je wewe upo kwenye upande upi? Kufanya au kujenga?
Sifa za wafanyaji wa biashara ni kama ifuatavyo;
1. Kuwa mfanyaji mkuu wa kile kinachofanywa kwenye biashara.
2. Kuwa peke yake au kuajiri watu lakini ambao lazima awapangie cha kufanya.
3. Kufanya kila kitu kwa mazoea.
4. Kuchanganya matumizi binafsi ya fedha na fedha za biashara.
5. Kutokuwa na namba zinazopimwa kwa usahihi kwenye biashara.
Sifa za mjengaji wa biashara ni kama ifuatavyo;
1. Kuwa na mfumo wa kuiendesha biashara ambao unaeleza utekelezaji wa kila kitu.
2. Kuajiri watu wenye uwezo wa kutekeleza majukumu wanayopewa bila ya kusumbua.
3. Kuwa na usajili wa biashara ambao unamtenganisha mtu binafsi na biashara yake.
4. Kuwa na namba ambazo zinapimwa kwa usahihi na kutumika kufanya maamuzi ya kukuza zaidi biashara.
5. Kutumia nyenzo mbalimbali ili kutumia rasilimali za wengine kwenye kujenga na kukuza biashara.
Rafiki, kama unavyoona sifa hizo za msingi, ni uchaguzi tu wa mtu. Haihitaji elimu kubwa wala gharama za ziada kwenye kutumia sifa hizo. Ni mtu kuamua kufanya kwa utofauti na kuweza kupata matokeo tofauti.
Karibu usikilize kipindi cha ONGEA NA KOCHA cha leo ili ujifunze kwa kina zaidi kuhusu dhana hii ya kufanya biashara na kujenga biashara ili uweze kukaa upande sahihi utakaokupa uhuru na mafanikio makubwa..
Sikiliza kipindi hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 2. KISIMA CHA MAARIFA, 3. CHUO CHA MAUZO na 4. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.