KCM2324086; Kukubalika.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumanneYaKujikubali

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

 Neno la leo; Kukubalika.

Leo ikiwa ni #JumanneYaKujikubali tunaona jinsi ambavyo kukubalika na wengine ndiyo hitaji kuu kwetu binadamu na jinsi ya kutimiza hilo.

Sehemu kubwa ya mambo ambayo watu wanayafanya kwenye maisha yao ni kwa ajili ya kukubalika na wengine.

Ni hali ya kutaka kukubalika ndiyo inawasukuma watu kufanya hata mambo yasiyokuwa na tija kabisa.

Ukichukua mfano wa mambo ambayo watu wanafanya ili kupata umaarufu au ‘kiki’, huwa ni ya hovyo kabisa.
Lakini kwa sababu yanawafikia watu wengi, basi watu hufanya bila ya kujali madhara yake.

Ipo njia ya kuwafikia wengi na kukubalika nao ambayo haina madhara makubwa kwa mtu.
Njia hiyo ni kwa mtu mwenyewe kuanza kujikubali sana ndani yake.
Ile hali ya mtu kujikubali yeye mwenyewe inaleta hali ya kuaminika na kukubalika na wengine.

Mtu anapokuwa na wasiwasi juu yake mwenyewe, huwa anawakosa wengi kwa sababu wanakosa imani kwake.

Chochote unachotaka watu wakupe, hebu anza kwa kujipa wewe mwenyewe kwanza.
Unapojipa yale unayotaka, unawafanya watu nao wakupe hicho.

Usihangaike kuwafanya watu wakupe kitu ambacho wewe mwenyewe huwezi kujipa.
Kuhangaika hivyo ni kupoteza muda na kujinyima matokeo unayoyataka.

Jikubali sana wewe mwenyewe na wengine hawatakuwa na namna bali kukukubali.
Ukitaka ukubalike kwa mambo mengine, utahangaika sana na matokeo hayatakuwa mazuri.

Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MWONGOZO WA MAISHA YA MAFANIKIO na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu msukumo wa kufanya. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2024/01/23/3310

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kujikubali wewe mwenyewe kwanza ili wengine nao waweze kukukubali.

Kocha.