3318; Visingizio na matokeo.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Huwa kuna kauli inayosema kimtokacho mtu ndiyo kilichomjaa.
Na nyingine inayosema mtu anatoa kile alichonacho.

Kauli hizo mbili zinatuonyesha kwamba kile ambacho watu wanafanya au wanatoa, ndicho walichonacho au wanachoweza.

Kwenye safari ya mafanikio, watu wanaweza kutoa moja kati ya hivi viwili; visingizio au matokeo.
Hakuna anayeweza kutoa vyote viwili kwa pamoja.

Ni labda mtu atatoa matokeo ya kile anachotaka kufikia.
Matokeo huwa yanatolewa na wale wanaochukua hatua.

Au mtu atatoa visingizio vya kwa nini hajapata matokeo.
Visingizio huwa vinatolewa na wale wasiochukua hatua.

Jambo moja la kushangaza ni kwamba nguvu inayotumika ni ile ile.
Nguvu inayotumika kutoa matokeo ni sawa kabisa na nguvu inayotumika kutoa visingizio.

Tofauti ni mtu tu amechagua kutumiaje nguvu zake.
Kutoa matokeo kunataka nguvu ziende kwenye ufanyaji.
Na kutoa visingizio kunataka nguvu ziende kwenye kutunga hadithi ya uongo inayofanana na ukweli.
Zote ni kazi kubwa na ngumu.

Watu ambao ni watoaji wa matokeo, huwa wametingwa na ufanyaji kiasi kwamba hawana muda wa kutengeneza visingizio kwa nini hawajafanya au hawana matokeo.

Watu ambao ni watoaji wa visingizio, huwa wametingwa na kuandaa na kutetea visingizio vyao kiasi kwamba hawana muda wa kufanya na kuzalisha matokeo.

Anakopeleka mtu nguvu ndiko kunakozalisha matokeo anayopata.

KISIMA CHA MAARIFA ni jamii ya wazalishaji wa matokeo na siyo visingizio.
Ni jamii ambayo wanachama wake wametingwa sana na kufanya kiasi kwamba hawana visingizio kabisa.
Kila mara wanakuwa wanaonyesha matokeo waliyozalisha.

Na pale matokeo yanapokuwa ni tofauti na matarajio, huwa hawana muda wa kutoa visingizio.
Badala yake wanakuwa wametingwa sana na kufanya kwa ubora zaidi ili kuzalisha matokeo ya tofauti.

Kwa sababu ya utamaduni wa ufanyaji na kuzalisha matokeo badala ya visingizio, jamii ya KISIMA CHA MAARIFA ni tofauti kabisa na jamii nyingine.
Mtu anapoteleza, hatumii muda mwingi kutoa visingizio kwa nini ameteleza.
Badala yake anatoa ahadi ya matokeo ya tofauti atakayozalisha na kwenda kuchukua hatua mara moja.

Je upo tayari kuachana kabisa na visingizio na kuzalisha matokeo?
Je unachagua kushirikiana na wale th wanaotoa matokeo na siyo visingizio?
Hilo ni hitaji la msingi kabisa kwenye kujenga mafanikio makubwa kadiri ya mtu unavyokuwa unataka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe