Maisha ni hatua, kila wakati tupo kwenye mwendo wa kuelekea kwenye kile ambacho tunataka kupata au kufikia. Njia tunayopita haijanyooka, ina vilima na mabonde na pia ina kona kali.
Wengi wamekuwa wanachoshwa na jinsi njia ilivyo na kukata tamaa ya safari. Hilo limekuwa tatizo kubwa ambalo ndiyo chanzo cha wengi kushindwa kufika kule walikopanga kufika. Pamoja na hili kuwa tatizo, angalau watu wanakuwa wanajua kwamba hawapo tena kwenye safari au hawana mwendo ambao utawafikisha kwa haraka.

Kuna tatizo jingine kubwa zaidi kwenye hii safari, ambalo ni kwenda njia isiyo sahihi. Hii njia ya kuelekea kwenye mafanikio pia ina njia panda nyingi. Kila baada ya hatua fulani mtu anajikuta akiwa njia panda, na mbaya zaidi akiwa hajui ipi njia sahihi.
Wengi wanapofika njia panda huwa wanachukua njia inayoonekana kuwa rahisi na ya uhakika zaidi. Lakini siyo mara zote njia hiyo huwa ni sahihi. Na hapo ndipo wengi hupotea, kwa kukazana kuongeza mwendo wakati wapo kwenye njia isiyo sahihi.
Kuna ambao huwa wanakuja kushtuka wapo kwenye njia isiyo sahihi baada ya kuwa wameenda sana. Hawa huona kurudi kwenye njia sahihi itawachelewesha sana na hivyo kuendelea kwenda, kitu ambacho kinazidi kuwapoteza.
Hivi ndivyo watu wanavyoyapoteza maisha yao na kushindwa kufikia mafanikio makubwa ambayo wangeweza. Inaweza kuwa ni mtu kuingia kwenye kazi ambayo haikuwa sahihi kwake, lakini baada ya kuwa ameshaitegemea sana na ana madeni mengi ya kulipa kwa kazi hiyo, anaona hawezi kutoka tena.
Au mtu anakuwa ameingia kwenye biashara ambayo siyo sahihi kwake, lakini inakuwa inamwingizia kipato ambacho hawezi kukiacha. Mwingine anaweza kuingia kwenye mahusiano ambayo siyo sahihi kwake, lakini kutokana na hatua ambazo anakuwa ameshafikia, anaona hawezi tena kuvunja mahusiano hayo.
SOMA; 2987; Hatua tano za kutatua tatizo lolote.
Kila mmoja wetu kuna namna anajikuta kwenye hali hii kwenye jambo fulani maishani mwake. Unajikuta umeenda mbali sana, upande ambao siyo sahihi, lakini ukifikiria kurudi kwenye upande sahihi unaona ni mbali sana au huna nguvu na muda wa kutosha kurudi.
Ukweli ni kwamba, kama njia uliyopo siyo sahihi, hakuna kitu ambacho kitabadilika kwa wewe kugoma kubadilika. Mambo yataendelea kuwa magumu kwako na sehemu ya maisha yako yaliyobaki itakuwa ya mateso na changamoto. Hivyo hatua pekee ya kuchukua ni kurudi kwenye njia sahihi.
Kinachowazuia wengi kuchukua hatua hiyo ya kwenda kwenye njia sahihi ni kujiona kama wanarudi nyuma. Lakini ukweli ni kwamba, hatua moja unayorudi nyuma kutoka kwenye uelekeo usio sahihi, ni hatua moja mbele kwenye uelekeo sahihi.
Kile unachoona kwa kufanya unapoteza muda, kinakuwa ni kuokoa muda ambao ungeendelea kuupoteza kwa kuhangaika na mambo yasiyokuwa sahihi kwako. Hivyo badili mtazamo wako juu ya kile unachofanya na kule unakotaka kufika.
Kila mara jifanyie tathmini kujua kama upo kwenye uelekeo sahihi au la. Pale unapogundua kwamba haupo kwenye uelekeo sahihi, unapaswa kuchukua hatua hapo hapo ili kurudi kwenye uelekeo sahihi. Hatua unayorudi nyuma kutoka kwenye uelekeo sahihi siyo hatua ambayo umepoteza, bali ni hatua ambayo umenufaika.
Kuhakikisha hupotei parefu kabla ya kuchukua hatua, jifanyie tathmini kwenye vipindi vya muda mfupi. Kwenye kila tathmini angalia ulikotoka, ulipo sasa na kule unakotaka kwenda. Kisha jiulize kama njia uliyopo ndiyo iliyo sawa kwako kutimiza yale unayotaka. Unapofanya tathmini za aina hii kwa karibu karibu, unaona makosa mapema na kuyarekebisha kabla hujapotea sana.
Usihofie kuchukua hatua sahihi pale unapojikuta umekosea, unakuwa hujapoteza kwa hatua hizo, bali umefanya kilicho sahihi.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.