Watu wengi kwenye maisha yao hawapati utajiri, licha ya kuutaka sana, kwa sababu wanakuwa hawajui jinsi ya kujenga utajiri. Wanaweza kuwa na shughuli zinazowaingizia kipato, lakini inapokuja kwenye kujenga utajiri, wanashindwa kabisa kwa sababu hakuna mahali wanafundishwa.

Halafu kuna wachache ambao kwa bahati au kupata nafasi fulani huwa wanajikuta wameweza kujenga utajiri kwenye maisha yao. Lakini kwa bahati mbaya sana, huwa wanaishia kupoteza utajiri huo wanaokuwa wameujenga.

Wengi wanapoteza utajiri wao wakiwa bado hai na wachache wanaoweza kuutunza kipindi cha uhai wao, utajiri huo hupotea pale wanapokufa. Kinachopelekea wengi wapoteze utajiri wao ni kutokujua jinsi ya kuutunza uweze kudumu kwa muda mrefu.

Kwa ambao bado hawajajenga utajiri, swala la kutunza utajiri kwao linaweza kuonekana halina umuhimu. Hivyo waliopo kwenye hatua hiyo huwa wanapambana zaidi na kujenga utajiri, kwa namna wanavyoona inafaa kwao.

Ni pale wanapopata utajiri ndiyo wanakuwa wamekaribisha hatari ya wao kupoteza utajiri wao, bila hata ya kujua. Kwa kuwa wameweza kutengeneza utajiri, huwa wanadhani utajiri huo utadumu.

Siri kubwa sana ambayo wengi hawaijui na imepelekea utajiri wa wengi kupotea ni kwamba ujuzi wa kutengeneza utajiri na ujuzi wa kutunza utajiri ni tofauti kabisa. Kwa kauli nyingine ni kwamba kile kinachomfanya mtu kuwa tajiri, siyo kitakachomfanya abaki kwenye utajiri huo.

Hiyo ina maana kwamba baada ya mtu kuweka kazi na kujenga utajiri, anahitajika kuweka kazi nyingine kubwa zaidi kutunza utajiri huo usipotee. Hilo ndilo ambalo wengi huwa hawalijui na huwa linawagharimu, kwa kuishia kupoteza utajiri wao wote.

Kuna mambo mengi ya kufanya ili kutunza utajiri baada ya kuutengeneza, lakini lililo muhimu zaidi ni kuhakikisha kwamba hufi. Wakati wa kutengeneza utajiri mtu anachukua hatua za hatari, kwa sababu anakuwa hana cha kupoteza. Lakini wakati wa kutunza utajiri, mtu anapaswa kuchukua hatua zenye hatari kubwa ya kupoteza. Bado atahitajika kuchukua hatua za hatari, lakini hazipaswi kuwa hatari mbaya kama za kipindi bado hawajajenga utajiri.

Kutokuridhika na kuendelea kuweka kazi kwenye shughuli ambazo mtu anafanya ni njia nyingine muhimu ya kutunza utajiri. Watu wengi huwa wanaacha kuweka juhudi baada ya kujenga utajiri, kitu ambacho kinawaingiza kwenye usumbufu ambao unawakosesha umakini kwenye utajiri wao na kuanza kuupoteza.

Unyenyekevu ni kitu kingine muhimu cha kufanya ili kutunza utajiri ambao mtu ameujenga. Utajiri una hali ya kuwapa watu kiburi na kuwapelekea kufanya maamuzi ambayo yanapoteza utajiri ambao wameshaujenga. Wengi huona baada ya kujenga utajiri wamemaliza kila kitu, hawahitaji tena kujifunza wala kumsikiliza yeyote. Halafu kuna ambao wanaona kwa kujenga utajiri kwenye eneo moja, wanaweza kujenga utajiri kwenye kila eneo. Matokeo yake ni wanajikuta wakihangaika na mambo ambayo hawana ujuzi wala uzoefu nayo kitu ambacho kinawaletea anguko kubwa.

Kuepuka hatari mbaya, kuendelea kuweka juhudi na kuwa mnyenyekevu ni vitu muhimu kuzingatia ili kuweza kutunza utajiri ambao mtu amekazana kuujenga kwa muda mrefu. Hivi ni vitu vigumu sana kuvijenga baada ya kuwa umeshajenga utajiri. Hivyo wakati mzuri wa kujijengea vitu hivyo ni wakati unaendelea kujenga utajiri. Kwa njia hiyo utabaki kwenye safari yako ya utajiri bila ya kuyumbishwa na kitu chochote.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina kuhusu kujenga utajiri na kutunza utajiri ili kila aliye kwenye safari ya utajiri aweze kuwa na tahadhari ya kutosha. Karibu usikilize kipindi hicho hapo chini na kuchukua hatua ili ujenge na kutunza utajiri wako kwa muda mrefu.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.