Ubunifu ni moja ya vitu vinavyohitajika ili mtu aweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yake. Lakini kwa bahati mbaya sana, wengi huwa wanajiona siyo wabunifu, kitu ambacho kinawazuia kufanya makubwa yanayohitajika.
Kitu ambacho nimekuwa nawaambia watu ni kwamba kila mmoja wetu ni mbunifu. Huwezi kukamilisha maisha yako ya kila siku bila kutumia ubunifu ambao unao. Ni vile vitu tunavyokuwa tunafanya tumevizoea kiasi cha kusahau kwamba ubunifu umehusika.

Chukua mfano wa mavazi ambayo tunayavaa. Huwa tunatumia muda kupangilia mavazi ambayo yanaendana kwa rangi na aina. Kuna rangi za mavazi mtu akizichanganya ataonekana kituko, hivyo kila mtu huwa anahakikisha mchanganyiko wake siyo wa ajabu.
Kadhalika mtu akiwa amechelewa mahali na njia anayotumia ni ndefu, huwa anatumia ubunifu kutafuta njia za mkato za kumfanya awahi kufika anakotaka kufika. Hiyo yote ni mifano ya jinsi ambavyo tayari tunao ubunifu ndani yetu na wajibu wetu ni kuutumia.
Ili kuweza kufikia ubunifu mkubwa ambao tayari upo ndani yetu, tunahitaji kutumia vizuri viungo viwili tulivyo navyo; AKILI na JICHO.
AKILI.
Ili kufikia na kutumia ubunifu ulio ndani yako, unapaswa kuiweka akili yako huru. Kuiweka akili huru maana yake ni kuiruhusu ifikirie kila kitu kwa uhuru badala ya kuiwekea vikwazo mbalimbali.
Hilo linakutaka mtu uachane na mitazamo na misimamo mikali uliyonayo juu ya vitu fulani. Unapaswa kujichukulia kama mtalii anayepita kwenye eneo na kutaka kujua kila kitu na maana yake.
Iruhusu akili yako iulize maswali na kujifunza, hata kama ni maswali ya kawaida na ambayo unaweza kujiambia ni ya kijinga, wewe jiulize maswali hayo na iruhusu akili itafute majibu.
Uzuri wa akili zetu ni kwamba zina taarifa nyingi sana zilizohifadhiwa na ambazo huwa hazipotei. Lakini inakuwa vigumu kwako kufikia taarifa hizo nyingi kwa sababu huzipi umakini wa kutosha.
Unaporuhusu akili yako kuwa huru, inaweza kugusa maeneo mengi na kupeleka umakini wa kutosha kwenye taarifa sahihi unazohitaji, kitu kinachochochea ubunifu.
Ifanye akili yako kuwa huru ili uweze kuhiji mambo mengi na kuibua ubunifu.
SOMA; Hivi ndivyo unavyojikwamisha kwenye ubunifu.
JICHO.
Jicho lako ndiyo mlango wa akili. Jicho linaona vitu vingi, lakini linapuuza vilivyo vingi, kwa sababu haliwezi kuchukua kila taarifa. Jicho linachuja yale ambayo akili inaona ni muhimu.
Ndiyo maana watu wawili wanaweza kuwa kwenye eneo moja, wakashuhudia tukio moja lakini kila mmoja akawa na maelezo yake ya tofauti. Kinachosababisha hali hiyo ni taarifa ambazo jicho la kila mmoja limekusanya ni tofauti.
Ili kuchochea ubunifu ndani yako, unapaswa kuwa na jicho lenye nidhamu ya hali ya juu sana. Jicho lenye nidhamu linahakikisha linaona kitu kwa uhalisia wake na siyo kwa mtazamo ambao mtu anao.
Kwa jinsi kuwa na nidhamu, linapeleka umakini kwenye mambo yote na hapo kuona mambo ya tofauti na yanayoweza kuchochea ubunifu.
Jicho lenye nidhamu linaona zaidi ya kile kilichopo na kuona yote yaliyojificha. Jicho lenye nidhamu linaleta mambo yasiyohusiana pamoja na kuzalisha kitu kipya ambacho hakikuwepo kabisa.
Ni pale unapochanganya akili iliyo huru na jicho lenye nidhamu ndipo nguvu ya ubunifu inapokuwa kubwa zaidi. Kwa akili kuhoji bila ya ukomo, huku jicho likitizama kwa umakini wa hali ya juu, vitu visivyoonekana kwa urahisi vinakuwa dhahiri.
Watu wengi wamefunga ubunifu wao kwa kufunga akili zao na kuachilia macho yao kuzurura hovyo na juu juu kwenye mambo mengi. Wewe usiwe hivyo, iache akili yako iwe huru na kuwa na nidhamu kwenye jicho lako. Hayo ni mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wako, ambayo ukiyafanya utaweza kuwa na ubunifu wa hali ya juu na utakaokuwezesha kufanya makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.