Utajiri kimekuwa ni kitu kisichoeleweka kwa wengi, japo kila mtu kwa ndani anaupenda utajiri. Kwa nje kuna ambao wanajaribu kuonyesha kwamba hawataki au hawapendi utajiri, lakini ni vigumu sana kuendesha maisha ambayo mtu anayataka bila ya kuwa na utajiri.

Wengi wanataka utajiri, ila wanaoupata ni wachache sana. Hiyo ni kwenye kila aina ya jamii, kila aina ya kazi na hata kila aina ya biashara. Kwenye kila eneo, huwa kuna watu ambao wameweza kujenga utajiri na kuna ambao wamebaki kwenye umasikini.

Mwandishi Wallace D. Watles kwenye kitabu chake alichokiita The Science Of Getting Rich anaeleza kwamba kujenga utajiri ni sayansi kama zilivyo sayansi nyingine. Kwamba zipo kanuni ambazo zikifuatwa basi matokeo yanapatikana. Maana huo ndiyo msingi wa sayansi, kwamba kanuni inapofuatwa na yeyote aliye popote, anapata matokeo.

Kupitia kitabu hicho mwandishi anaonyesha jinsi ambavyo tofauti ya tajiri na masikini haianzii nje, bali ndani yao. Kwa kuwa kila eneo kuna matajiri na masikini, ni dhahiri kwamba kinachochangia utajiri au umasikini ni vitu vya ndani na siyo nje.

Kupitia mifano mbalimbali inayoanzia kwenye miili na uwezo wetu binadamu ndiyo mwandishi alifikia hitimisho kwamba sayansi ya kujenga utajiri inajenga na vitu viwili.

Kitu cha kwanza ni NAMNA YA KUFIKIRI.

Mwandishi anaeleza kwamba matajiri huwa wana namna ya kufikiri ambayo ni tofauti kabisa na masikini. Namna hiyo ya kufikiri inahusisha kuweka kwenye fikra zao kwa muda mrefu kile wanachotaka na siyo wanachotaka. Wanalinda fikra zao kuhakikisha zinabeba kile tu wanachotaka na siyo kingine chochote.

Pia kwenye namna ya kufikiri kuna jambo muhimu la shukrani ambalo mwandishi amelielezea sana. Kwamba matajiri huwa ni watu wa shukrani, kitu ambacho kinawaletea utajiri zaidi. Mtu anaposhukuru anakuwa amekithamini kitu na hivyo kuvutia kije kwake kwa wingi zaidi.

Kitu cha pili ni NAMNA YA KUFANYA.

Mwandishi anaeleza matajiri huwa wana namna ya kufanya mambo yao ambayo ni tofauti kabisa na wanavyofanya masikini. Matajiri huwa wanafanya kwa kutoa thamani kubwa ya matumizi kwa wengine kuliko thamani ya fedha wanayochukua. Wanatoa thamani kubwa sana kiasi cha wengine kuvutiwa kujihusisha nao, kwa sababu hakuna asiyependa thamani.

Kitu kingine ambacho matajiri wanafanya tofauti na masikini ni ufanisi kwenye yale wanayofanya. Kila wanachofanya wanakifanya kwa usahihi kiasi kwamba kinakuwa na manufaa. Hawafanyi chochote ambacho hakina tija na wala hawafanyi juu juu na kwa kuharakisha. Wanafanya kitu kwa kina na kuleta matokeo mazuri. Muhimu zaidi ni huwa hawaahirishi yale wanayopanga kufanya na hivyo kukamilisha kwa wakati.

Ni kwa kuleta vitu hivyo pamoja ndiyo mtu unakuwa umekamilisha kanuni yako kuu ya utajiri ambayo ukiifanyia kazi utajiri unakuwa ni wa uhakika kwako. Unachofanya ni kufikiri kwa usahihi, kwa kuweka mawazo yako kwenye kile unachotaka na kuwa mtu wa shukrani. Na pia unafanya kwa usahihi kwa kutoa thamani kubwa na ufanisi wa hali ya juu.

Kwa kufanya hayo manne, yote kwa pamoja, utaweza kujenga utajiri mkubwa bila ya kujali ni kazi au biashara gani unafanya. Kwa sababu hata mwandishi amesisitiza kwamba mtu yeyote atakayefuata mafundisho ya kitabu kama yalivyo, kufanikiwa ni uhakika.

Kuna tahadhari ambayo mwandishi ameitoa, kwamba hupaswi kuchanganya mafunzo haya na mengine yanayokinzana nayo. Ukianza kufikiria kutajirika kwa kuwanyang’anya wengine au ukiona kuna uhaba wa vitu, utaharibu kabisa kanuni uliyoitengeneza.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza mengi na kwa kina kutoka kwenye kitabu hicho. Karibu usikilize kipindi hicho, ujifunze na kwenda kuchukua hatua sahihi ili uweze kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.