Rafiki yangu mpendwa,

Zama tunazoishi sasa ni zama za kipekee sana. Ni zama za maarifa na taarifa ambapo wenye maarifa na taarifa sahihi ndiyo wenye nguvu kubwa ya kujenga mafanikio. Lakini pia, maarifa na taarifa vinapatikana kwa urahisi kwa watu wote kuliko zama nyingine zozote.

Cha kushangaza sasa, bado watu wanaopata mafanikio makubwa kwenye kila jamii ni wachache sana. Wengi wanabaki kwenye hali duni au mafanikio ya kawaida, licha ya kila kinachohitajika ili kujenga mafanikio kuwa kinajulikana wazi kabisa.

Sababu kubwa inayopelekea watu wengi kuishia kwenye hiyo hali ya kukosa mafanikio makubwa, licha ya njia kuwa wazi ni kuhangaika na njia zisizokuwa sahihi za mafanikio. Watu wamekuwa wanahangaika na njia ambazo kwa nje wanaona kama zinawapa mafanikio, lakini kwa ndani zinawapoteza tu.

Watu hao huwa ni wagumu sana kujifunza njia zilizo sahihi, kwa sababu wanakuwa na tamaa ya mafanikio makubwa na kwa haraka. Tamaa hiyo wanayokuwa nayo inawapa upofu wasione jinsi wanavyojikwamisha.

Kwa mtu yeyote ambaye amehangaika na mafanikio kwa muda mrefu bila kuyapata, hatua ya kwanza anayopaswa kuchukua ni kufuta yale ambayo alikuwa anayajua kuhusu mafanikio na kujifunza mapya ambayo ni sahihi. Kwa sababu mtu huyo kinachomkwamisha siyo yale ambayo hajui, bali yale ambayo tayari anajua.

Kwa sababu ya hayo anayoyajua, ambayo siyo sahihi, yanamzuia kujua yale waliyo sahihi. Ndiyo maana hata akijifunza mambo mapya, bado anarudi kufanya yale ya zamani aliyoyazoea. Hivyo suluhisho la uhakika hapa ni kung’oa kwanza yale yasiyo sahihi ambayo ameyaamini na kuyafanyia kazi kwa muda mrefu, ili apande yaliyo sahihi na yatakayompa mafanikio kwa uhakika.

Hilo siyo zoezi rahisi, hasa pale mtu anapokuwa ameshaonja mafanikio kidogo kupitia njia zisizokuwa sahihi. Anakuwa na matumaini makubwa kwamba ameshayakaribia sana mafanikio. Kila mara matumaini ya aina hiyo yanakuwepo na ndiyo yanayozidi kumpoteza.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeshirikisha kwa kina kuhusu njia zisizo sahihi za mafanikio ambazo zimewapoteza wengi, ili wewe uweze kuziepuka na ujenge mafanikio makubwa na ya uhakika. Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho hapo chini na ukaachane na njia hizo ili ujenge zilizo sahihi na ufanye makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.