Rafiki yangu mpendwa,

Hilo ni swali ambalo nakuuliza wewe rafiki yangu, nikikutaka unijibu, kwa sababu nashindwa kabisa kukuelewa rafiki.

Tayari maisha yako ni magumu, kuanzia kwenye kazi au biashara unayofanya, kwenye kipato, kwenye mahusiano na maeneo mengine ya maisha yako.

Kuna mengi ambayo unataka kuyapata kwenye maisha yako, unayapambania hasa, lakini bado unakwama kuyapata.

Unajua ndani yako una uwezo mkubwa na unapambana uweze kuufikia, lakini bado matokeo hayajawa kama unavyotegemea.

Watu uliowategemea wakupe vitu fulani au kuwa msaada kwako wameishia kukusaliti.

Halafu sasa, pamoja na hayo yote, unachagua kuongeza ugumu kwenye hayo maisha yako.

Ugumu ambao unauongeza ni wa kuwaahidi watu vitu halafu huvitimizi. Wewe mwenyewe, kwa utashi wako, unawaahidi watu kwamba utafanya vitu fulani.

Wakati wa kuleta mrejesho kwa watu hao, ambao wanakuwa wanasubiri kwa hamu matokeo ya ulivyofanya, unawaletea hadithi. Unakuja na sababu kwa nini umeshindwa kufanya.

Unaweza kuwa na sababu ambazo wewe unaziona ni za msingi sana. Watu wanaozisikiliza sababu hizo wanaweza hata kukuonea huruma. Lakini kuna kitu kikubwa unakuwa umepoteza kwao, watu hao wanakuwa hawakuamini tena kama ilivyokuwa kabla.

Kwenye fikra zao wewe ni mtu ambaye huaminiki, kwa sababu unatoa ahadi lakini unashindwa kuzitekeleza. Hivyo hawatakua tayari kukupa fursa ambazo zinahitaji sana umakini mkubwa kuzikamilisha.

Sasa hebu fikiria ni kwa watu wangapi ambao umekuwa unawaahidi vitu kirahisi, lakini huvitekelezi? Unajionea mwenyewe rafiki yangu jinsi ambavyo umevunja imani yako kwa wengi na ndiyo maana hawakupi fursa ambazo ulikuwa unazitegemea.

Je una mtu yeyote wa kumlaumu na huo ugumu wa maisha ambao umetokana na watu kukosa imani na wewe? Jibu unalijua.

Rafiki, ninachotaka kukuambia ni kimoja, ukitaka kuacha kuyafanya maisha yako kuwa magumu zaidi ya yalivyo, kanuni ni moja tu; AHIDI KISHA TEKELEZA. Sema utafanya kitu, halafu kifanye kweli.

Kama kuna kitu kimekuzia ushindwe kutimiza kama ulivyoahidi, hupaswi kukimbilia kuja na sababu, badala yake unapaswa kuwa unapambana na huo ugumu uliokutana nao.

Kwa kifupi ni ukishaahidi, unatakiwa uje na matokeo au usionekane kabisa. Uwe umetingwa sana na kutimiza au uje na matokeo, kuja na maneno ni kitu rahisi ambacho yeyote anaweza kukifanya.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina jinsi ya kuacha kuyafanya maisha yako kuwa magumu kwa ahadi hewa unazowapa wengine kirahisi. Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho hapo chini.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.