3353; Uliyokamilisha kufanya.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kile kinachoitwa siri za mafanikio, huwa siyo siri, bali ni mambo yaliyo bayana na kila mtu anayajua.
Kinachofanya mambo hayo yaliyo bayana kuitwa siri ni wengi kutokuwa tayari kuyafanya.
Watu wanayakwepa mambo hayo ambayo ni ya uhakika kabisa na kwenda kuhangaika na mengine mengi ambayo hayana uhakika kwao.
Moja ya vitu vinavyoweza kuonekana kama siri ya mafanikio, wakati ni kitu ambacho kipo bayana kabisa ni mambo ambayo mtu amekamilisha kufanya.
Matokeo yoyote ambayo mtu anayapata, yanaanzia kwenye utekelezaji. Ni yale ambayo mtu amekamilisha kufanya, ndiyo yanayoleta matokeo.
Kutaka, kila mtu anataka.
Kupanga, wengi wanapanga.
Kuanza kufanya, wachache wanaanza.
Lakini kukamilisha kufanya, ni wachache sana ambao wanafanikisha hilo.
Na hao wachache sana ndiyo wanaopata mafanikio makubwa.
Unaweza kuwa na mikakati bora kabisa.
Unaweza kuwa na mbinu za kila aina.
Lakini kama hutaweza kukamilisha mambo, hakuna matokeo ya tofauti utakayoyapata.
Weka nguvu zako kubwa kwenye kukamilisha mambo na utaweza kupata matokeo makubwa na ya tofauti.
Waache watu wakimbizane na kutafuta siri za mafanikio.
Wewe kazana kukamilisha mambo na matokeo utakayoyapata yatakuwa bora sana.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, kukamilisha mambo ndiyo msingi mkuu.
Kanuni tunayoiishi mara zote ni MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO.
Tunajua wazi kabisa kwamba bila vitendo, bila kuchukua hatua kwa uhakika kwenye yale yote tunayojifunza na kupanga, hatutaweza kuzalisha matokeo ya tofauti na tunayokuwa tumezoea kupata.
Kwenye jamii hii tunawajibishana kwa yapi uliyokamilisha kufanya.
Siyo mipango wala nia, bali yale uliyokamilisha.
Unaweza kuwa na hadithi nyingi kuhusu kushindwa kuchukua hatua. Lakini zitakosa kabisa maana kama hakuna mambo unayoyakamilisha.
Kila siku hakikisha kuna mambo yenye tija ambayo unakuwa umekamilisha kuyafanya. Ni mkusanyiko wa mambo hayo uliyokamilisha ndiyo unaoleta mafanikio makubwa.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe