3355; Kuanza na kumaliza.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Matokeo unayoyapata kwenye maisha yako, yanategemea sana jinsi unavyochukulia kuanza na kumaliza.

Wale wanaofanya makubwa huwa ni watu wa kuanza kufanya haraka na kuendelea kufanya mpaka kumaliza.
Hawapotezi muda kwenye kuanza na wala hawaishii njiani kwenye yale ambayo ni muhimu.

Wanaoishia kuwa kawaida huwa wanachelewa kuanza, lakini hawafanyi  mpaka kumaliza. Huwa ni rahisi kwao kuacha pale wanapokutana na magumu au changamoto.
Hivyo kupata kwao kunategemea kama njia itakuwa rahisi kwao.
Hivyo inakuwa ni kama bahati zaidi.

Wanaoshindwa huwa hawaanzi kabisa. Wanaweza kuchukua muda kupanga na kutathmini kitu, lakini hawafiki hatua ya kuanza kabisa.
Kwa njia hiyo hawapati hata nafasi ya kuendelea kufanya. Hivyo hakuna matokeo yoyote wanayoyapata.

Kwa kuanzia upande ambao upo, unaweza kupiga hatua kwenda mbele ili kupata matokeo mazuri.
Kama umekuwa huanzi kabisa, chukua hatua ya kuanza kila kitu mara moja. Bila ya kupanga na kutathmini kwa kina, wewe anza.
Hata kama umekosea kuanza, unaweza kuacha wakati wowote.
Lakini kumaliza kitu ambacho hujaanza kabisa, haipo.
Hivyo unachokuwa unataka ni kuweza kuanza, maana hapo ndipo kikwazo kikubwa kinapokuwepo.

Kama umekuwa unaanza lakini unaishia njiani, chagua kitu kimoja ambacho utaenda nacho mpaka mwisho bila kujali matokeo gani unayopata.
Lengo lako liwe ni kwenda na jambo hilo mpaka kulikamilisha kabisa, kulingana na kile unachofanya.
Kitendo tu cha kukamilisha chochote ulichoanza kufanya, kinapelekea ujisikie vizuri na tofauti kabisa.

Anza, na ukishaanza, maliza.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, kufanya ni msingi wetu mkuu.
Kwa sababu tunathamini sana kufanya, kuanza na kumaliza inakuwa tayari ndani yake.
Tunaanza kufanya haraka kwa sababu tayari tunayo maarifa tunayohitaji.
Na tunaendelea kufanya kwa sababu kwa kila hatua tunaboresha zaidi.
Kwa kwenda hivyo tunakamilisha mengi na kuweza kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yetu, kitu kinachotuhakikishia kupata mafanikio makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe