Habari Matajiri Wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya uwekezaji kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU. Hii ni programu maalumu ya kujifunza na kufanya uwekezaji kwa vitendo ili kujenga utajiri mkubwa kwa kutumia fedha ndogo ndogo tunazokuwa nazo.
Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza dhana ya RIBA MKUSANYIKO (COMPOUND INTEREST) na nguvu yake kwenye uwekezaji. Hii ni moja ya dhana muhimu sana ambayo kila mwekezaji anapaswa kuielewa ili afanye uwekezaji wake akiwa na amani.

Kuelewa vizuri dhana hii, tutakwenda kupata hadithi fupi.
Mkulima mmoja alifanya jambo la kishujaa na mfalme alifurahishwa sana na kujitoa kwa mkulimo huyo. Kwa umuhimu na ukubwa wa jambo alilofanya mkulima, mfalme alimtaka achague zawadi yoyote anayotaka na atampatia.
Mkulima alitafakari kwa kina na kisha kumwambia mfalme zawadi ambayo amechagua. Alimwomba mfalme ampe punje moja ya mchele, halafu kila siku azidishe mara mbili kwa siku 30. Yaani siku ya kwanza ampe punje moja, siku ya pili punje 2, siku ya tatu punje 4, siku ya nne punje 8 na kuendelea kuzidisha mara mbili hivyo kwa siku 30.
Mfalme alicheka sana, aliona amechagua zawadi ndogo, lakini akakubali kumpa zawadi aliyochagua. Ilipofika siku ya 20, mfalme alijutia maamuzi yake, kwani mkulima alikuwa anapewa kiasi kikubwa cha mchele kuliko ulivyokuwa unapatikana. Na ilipofika siku 30, mkulima yule alikuwa anamiliki mchele wote kwenye ule ufalme.
Hadithi hiyo fupi inaonyesha nguvu ya hatua ndogo ndogo ambazo zinaenda zikikua kadiri muda unavyokwenda. Na hivyo ndivyo riba mkusanyiko inavyofanya kazi.
Riba mkusanyiko ni dhana ya uwekezaji ambapo riba ambayo mtu anaipata inazalisha riba pia.
Kwenye riba ya kawaida, ukiwekeza fedha, unapata rejesho kulingana na kiwango cha riba kilichowekwa.
Kwa mfano kama umewekeza elfu 10 na riba ni asilimia 10, ina maana utapata rejesho la elfu 1. Kwa kuwekeza elfu 10, unapata rejesho la elfu 1, yaani elfu 10 yako imezaa elfu 1. Hiyo ndiyo riba ya kawaida.
Kwenye riba mkusanyiko, mambo hayaishii hapo, bali yanaendelea. Ile riba ambayo imetokana na uwekezaji wako wa awali nayo inazaa riba. Hata sasa ni mtaji wako unazaa riba na ile riba nayo pia inazaa.
Tukirudi kwenye mfano wa elfu 10, umewekeza na kupata rejesho la asilimia 10 ambayo ni elfu 1. Usipotoa hiyo elfu moja, rejesho linalofuata halitakuwa tena elfu 1, bali litakuwa elfu 1 na mia moja. Ile elfu 10 uliyokuwa umewekeza awali inakupa rejesho la elfu 1 na ile elfu 1 uliyokuwa umepata kama rejesho ila hukuitoa nayo inaleta rejesho la asilimia 10 yake ambayo ni mia moja.
Hivyo kwa kuwekeza 10,000/= kwa riba ya ailimia 10, hivi ndivyo ukuaji utakavyoenda.
Msingi unaoanza nao = 10,000/=
Mwisho wa mwaka wa kwanza; msingi + riba; 10,000 + 1,000 = 11,000/=
Mwaka wa pili unaanza na msingi wa 11,000/= kwa sababu hujatoa hilo rejesho.
Mwisho wa mwaka wa pili; msingi + riba; 11,000 + 1,100 = 12,100/=
Mwanzo wa mwaka wa tatu unaanza na msingi wa 12,100/= kwa sababu bado hutoi rejesho.
Mwisho wa mwaka wa tatu; msingi + riba; 12,100 + 1,210 = 13,310/=
Mwaka wa nne unaanza na msingi wa 13,310. Utaenda hivyo kwa miaka yote ambayo utaendelea na uwekezaji wako bila kutoa msingi au rejesho.
Unajionea hapo jinsi ambavyo thamani ya uwekezaji inavyoongezeka kila mwaka, kwa sababu hutoi rejesho linalopatikana. Hivyo ndivyo dhana ya riba mkusanyiko inavyofanya, kila rejesho linazalisha rejesho zaidi.
Hapo ni kama umeweka kiasi hicho na kutokuweka tena. Mambo yanakuwa mazuri zaidi pale unapokuwa unaendelea kuwekeza msingi zaidi na zaidi. Kwa hiyo mtaji unaendelea kuongezeka na riba inaendelea kuongezeka.
SOMA; TABIA ZA KITAJIRI
RIBA MKUSANYIKO NA NGUVU YA BUKU.
Kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU tunawekeza kiasi kidogo kidogo cha fedha. Kwa hesabu za kawaida, unaweza kuona kwa muda mrefu bado uwekezaji huo utakuwa mdogo.
Kwa mfano ukiwekeza elfu 1 kila siku, kwa mwaka ni Tsh 360,000/= na kwa miaka 10 ni tsh 3,600,000/= Ukipiga kwa riba ya kawaida, asilimia 10 kwa mwaka itakuwa 36,000/= na kwa miaka 10 riba ya kawaida ya asilimia 10 italeta rejesho la 360,000/=
Hivyo kwa hesabu za riba ya kawaida, kuwekeza elfu moja kwa miaka kumi, itafika 3,600,000/= na kukupa rejesho la 360,000/=. Hizo ni namba ndogo sana na ambazo ni kichekesho kabisa, ni kama zitakosa maana kabisa.
Lakini tukienda kwa kanuni ya riba mkusanyiko, A = P( 1 + r/n)nt – P ambapo A ni kiasi kinachokuwa kimefikiwa, P ni msingi uliowekezwa, r ni kiasi cha riba, n idadi ya marejesho kwa mwaka na t ni muda.
Kwa kanuni hiyo, kuwekeza elfu 1 kila siku, ambayo ni sawa na elfu 30 kila mwezi, kwa miaka 10 inazalisha kiasi cha 6,145,349.37 ambayo ni karibu mara 2 ya kiasi ambacho ungepata kwa riba ya kawaida. (unaweza kutumia kikokotozi hapa; https://www.uttamis.co.tz/tools/monthly-calculator).
Nguvu ya Riba Mkusanyiko ndiyo inafanya programu hii ya NGUVU YA BUKU kuwa na manufaa kwetu. Kwa sababu ni kama tunachuma hela za bure, kwa sababu ya nidhamu yetu na uvumilivu kwenye uwekezaji.
RIBA MKUSANYIKO NA MIFUKO YA UTT.
Mifuko yote ya UTT inao ukuaji wa riba mkusanyiko ndani yake. Uzuri wa riba mkusanyiko ya UTT haipigiwi kwa mwaka au mwezi tu, bali inapigiwa kila siku na ongezeko kuonekana kwenye thamani ya vipande.
Ndiyo maana kila wakati tunaona mabadiliko kwenye thamani ya vipande, inakuwa inatokana na nguvu hii ya riba mkusanyiko. Hivyo kwa mfuko wowote wa UTT unaokuwa unawekeza, jua tayari nguvu ya riba mkusanyiko iko ndani yake, lakini hiyo ni kama tu hutavuruga uwekezaji wako kwa kutoa fedha ulizowekeza.
Kitu kitakachovuruga riba mkusanyiko ni wewe kutoa uwekezaji unaokuwa umefanya. Ndiyo maana kwenye programu ya NGUVU YA BUKU tumejipa angalau miaka 10 ya kuwekeza bila ya kutoa. Tukizingatia hilo, tutapata manufaa makubwa sana.
MJADALA WA SOMO.
Karibu ushiriki mjadala wa somo hili kama ushahidi wa kulisoma na kuelewa. Jibu maswali yafuatayo;
1. Riba mkusanyiko inafanyaje kazi? Nini kinafanya ongezeko kwenye riba mkusanyiko kubwa kubwa kuliko kwenye riba ya kawaida?
2. Kwenye programu ya NGUVU YA BUKU, riba mkusanyiko inatunufaishaje? Nini tunapaswa kufanya ili tusivuruge riba mkusanyiko?
3. Ukiambiwa uchague moja kati ya haya mawili; A. Uchukue milioni 1 kwa mkupuo au B. upewe elfu 1 inayozidishwa mara 2 kila siku kwa siku 12. Je utachagua A au B? Eleza kwa namba kwa nini umechagua jibu ulilochagua.
4. Kama una swali lolote kuhusu somo hilo au programu ya NGUVU YA BUKU kwa ujumla karibu uulize.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.