Rafiki yangu mpendwa,

Watu wengi wamekuwa wanajikwamisha kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yao kwa sababu kubwa mbili.

Sababu ya kwanza ni kuiga kile ambacho wengine wanafanya. Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii na hivyo huwa ni rahisi kwetu kuiga yale ambayo wengine wanayafanya. Huwa tunaona ni bora kukosea kwa kufuata kile kinachofanywa na wengi kuliko kufanya kitu cha peke yetu.

Sababu ya pili ni kufanya kile ambacho umezoea kufanya. Unafanya leo kile ulichofanya jana na kesho kile ulichofanya leo. Kwa sababu kile ulichozoea kufanya kimekuwa kinakupa matokeo ambayo unaona ni ya uhakika, hata kama ni madogo, unakuwa tayari kuendelea kufanya hicho kuliko kujaribu vitu vipya.

Matokeo yake yanakuwa ni kupata matokeo yale yale ambayo umekuwa unayapata na kushindwa kupiga hatua kubwa kimafanikio.

Mwandishi na mbobezi wa masoko, Seth Godin kwenye kitabu chake cha PURPLE COW anasema ukiwa unaendesha barabarani na kukutana na ng’ombe wa rangi nyeusi na nyeupe, hautashangaa sana. Kwa kuwa unawaona ng’ombe hao hao, unazoea na kuanza kuwapuuza. Lakini ukikutana na ng’ombe wa rangi ya zambarau, anashika umakini wako, utamshangaa na kumzungumzia kwa wengine.

Hivyo ndivyo maisha yetu yalivyo, kwenye mambo yote tunayofanya, iwe ni kazi, biashara na hata mahusiano. Pale unapofanya vitu vya kawaida na vilivyozoeleka, watu wanakuzoea na kukupuuza, hawakupi umakini mkubwa. Lakini unapofanya kitu cha tofauti na kipekee, watu wanakupa umakini na kukuzungumzia, kwa sababu inakuwa haijazoeleka.

Anachotushauri Seth Godin ni tusikubali kuwa ng’ombe wa kawaida, badala yake tuwe NG’OMBE WA ZAMBARAU ili tuwashangaze watu na kunasa umakini wao.

Nitakushirikisha dhana hii ya NG’OMBE WA ZAMBARAU kwenye maeneo matatu na hatua za kuchukua.

Eneo la kwanza ni kwenye biashara.

Kama upo kwenye biashara, acha mara moja kufanya mambo kwa kuiga au kwa mazoea. Watu wengi huwa wanaingia kwenye biashara baada ya kuona wengine wakiwa kwenye biashara hizo. Na hata ukianza biashara ya kibunifu, bado kuna ambao watakuja kukuiga. Watu wanapofanya biashara zinazofanana au kwa namna inayofanana, wanaishia kugawana wateja wachache wanaokuwepo na kushindwa kupata mafanikio makubwa.

Kuondokana na hili, endesha biashara yako kama NG’OMBE WA ZAMBARAU, kwa kujitofautisha na wengine. Unajitofautisha kwa kuja na vitu vipya na vya kipekee ambavyo wateja hawawezi kuvipata pengine. Lakini pia unapaswa kujitofautisha na wewe mwenyewe kwa kutokufanya kwa mazoea, hata kama ni kitu unachofanya mwenyewe.

SOMA; Njia 10 Za Uhakika Kupata Mpenyo Ambazo Zitakusaidia Sana Kufanikiwa Kwenye Kazi au Biashara Yoyote Unayoifanya.

Eneo la pili ni kwenye kazi.

Kama umeajiriwa, usikubali kabisa kufanya kazi yako kwa mazoea, hasa kwa kuiga wale ambao umewakuta kazini au unafanya nao kazi. Badala yake fanya kazi zako kwa upekee kabisa, nenda hatua ya ziada, jitume na tatua changamoto ambazo ni ngumu. Hakikisha kukosekana kwako kunafanya mambo yakwame na hapo utathaminiwa zaidi. Na hata inapofika wakati unatafuta kazi nyingine, huhitaji hata kufanya maombi, bali waajiri wanakutafuta wenyewe.

Kama upo kwenye ajira, kuwa NG’OMBE WA ZAMBARAU kwa kuhakikisha unatekeleza majukumu yako kwa upekee wa hali ya juu sana. Usifanye kwa mazoea wala usiige wengine, jitume sana na utaacha alama ya tofauti na kupata fursa nyingine kubwa zaidi.

Eneo la tatu ni kwenye mahusiano.

Umewahi kujiuliza kwa nini mwanzo wa mahusiano watu huwa wanakuwa na kupendana na kujaliana sana, lakini muda unavyokwenda upendo unapungua? Sababu kuu ni kuzoeana na mazoea yakishaingia, mapenzi yanafifia na hata kuishia kuvunjika. Ili mapenzi yastawi na kuvuka changamoto mbalimbali, lazima waliopo kwenye mahusiano hayo wawe NG’OMBE WA ZAMBARAU. Kila wakati wafanye vitu vipya na vya kuwashangaza na kuwafurahisha wenza wao. Ni kwa njia hiyo ndiyo penzi linakuwa moto moto wakati wote.

Rafiki yangu, najua katika hayo maeneo matatu, angalau mawili yamekugusa moja kwa moja, hivyo basi chukua hatua sasa ya kuwa NG’OMBE WA ZAMBARAU na ufanye kwa utofauti ili kujenga mafanikio makubwa.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimeshirikisha kwa kina zaidi uchambuzi wa kitabu hicho cha PURPLE COW pamoja na mjadala wa kitabu hicho ambapo washiriki wa kipindi wameweza kushirikisha uzoefu wao binafsi. Ni kipindi muhimu sana kwako kujifunza na kuwa bora. Fungua sasa uweze kujifunza.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.