3365; Unawapa nafasi ya kukusumbua.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kile ambacho watu wengi wanalalamikia kwamba ushindani umewasumbua, tatizo huwa halipo sana kwenye ushindani, bali kwa watu wenyewe.
Yaani kama biashara inapitia changamoto kutokana na ushindani, chanzo kinakuwa siyo huo ushindani, bali biashara yenyewe.
Kwa mfano, kama ungeweza kujenga mshindani wa biashara yako mwenyewe, ambaye anatoa ubora kuliko unaotoa wewe na kwa gharama nafuu zaidi, je ungefanya hivyo?
Unajua hilo linawezekana, lakini hulifanyi na matokeo yake ni kutoa mwanya kwa washindani kufanya hivyo na kuweza kukusumbua.
Biashara yoyote ambayo inasumbuliwa na ushindani, iliona kabisa mwanya wa kufanya kwa tofauti na ambavyo imekuwa inafanya, lakini haikufanya hivyo. Na hapo ndipo ilipoacha mwanya ambao umetumiwa vizuri na ushindani.
Wajibu wako mkubwa kwenye biashara ni kuwa mshindani wako mwenyewe. Kila wakati jiulize kama ungekuwa wewe ndiye mshindani wako mwenyewe, ni maeneo gani ungeyatumia kujishinda?
Kama unaifuatilia biashara yako kwa kina, utaona wazi maeneo yote yenye madhaifu.
Kama utayafanyia kazi maeneo hayo yenye madhaifu, utaweza kujenga biashara imara na inayoweza kuhimili kila aina ya ushindani.
Kila fursa unayoiona ya kuifanya biashara yako kubwa bora zaidi, anza kuifanyia kazi mara moja. Usijicheleweshe kwa sababu unaona bado una nafasi ya kuendelea na vile unavyofanya. Unapotoa mwanya kwa ushindani kupata nguvu ya kukusumbua, utasumbuliwa kweli.
Unapaswa kuwa mbele yako mwenyewe kiasi cha ushindani kuona upo kila mahali. Hilo litafanya ushindani uwe na hofu ya kukabiliana na wewe kwa namna unavyoonekana kuwa mbele kuliko pale wenyewe wanapotaka kuingilia.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti na kipekee tunayoijenga, tunakuwa washindani wetu wenyewe kabla ya ushindani mwingine wowote.
Kwa kila tunachofanya, tunaangalia madhaifu yetu yako wapi na kuhakikisha tunayafanyia kazi kabla hayajatumika na wengine.
Kila wakati tunaweka juhudi kubwa kama vile kuna wengine wanafanya kazi masaa 24 kutuondoa kwenye nafasi tuliyopo, na huo ndiyo ukweli.
Hatuachi kuweka juhudi kubwa kwa sababu tunajua kufanya hivyo ni kutoa mwanya kwa wengine kutusumbua.
Kila tunapojishawishi tunapaswa kupumzika na kupata starehe, tunajikumbusha kwamba muda tutakaofanya hivyo ni muda ambao utatumiwa na wengine kwenda mbele yetu zaidi.
Kwenye jamii hii, ni dhambi kubwa sana kukubali kuacha wengine kuwa mbele yetu. Wajibu wetu mkubwa ni kuwatimulia vumbi kiasi kwamba hawaoni hata tumepita wapi.
Hatufanyi hayo yote kushindana na hao wengine, bali tunafanya ili kuwaacha nyuma na kutokuwapa nafasi ya kutusumbua.
Tunajisumbua sisi wenyewe ili tusiweze kusumbuliwa na wengine.
Tunafanya kila tunachofanya tukiwa tumefungua macho na masikio yetu.
Tunaangalia na kusikiliza kwa makini ili kuona fursa nzuri za kwenda mbele yetu wenyewe na kuzitumia kufanya hivyo.
Hilo linatufanya kuwa mbele ya washindani mara zote.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe