Rafiki yangu mpendwa,
Mauzo ni kazi yenye kupanda na kushuka kihisia kwa wingi kuliko kazi nyingine yoyote. Fikiria umeongea na mteja na akaonekana kabisa amekubali kununua. Anakuahidi kwamba lazima atanunua na usiwe na wasiwasi. Lakini unapofika wakati wa kutimiza ahadi, anaanza kukuzungusha.

Lakini pia kuna kukataliwa kwa wingi sana kwenye mauzo kuliko kwenye kazi nyingine yoyote ile. Hata kama uwe umeshakataliwa mara ngapi, kukataliwa bado huwa kunauma sana kihisia.
Hayo na mengine mengi ndiyo yamekuwa yanafanya mauzo kuwa kazi ya kupanda na kushuka kihisia. Pale unapokamilisha mauzo unapata matumaini ya kuendelea na pale unapokataliwa unakata tamaa na kutaka kuacha.
Lakini licha ya yote hayo, bado una wajibu wa kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo ambayo ni makubwa. Hayo yatakutaka uweze kukabiliana na hiyo hali ya kupanda na kushuka kwa hamasa.
Ili uweze kufanya mauzo makubwa, ni lazima mara zote uwe na hamasa za juu kabisa. Hamasa ya kukufanya uendelee kuchukua hatua licha ya magumu na changamoto unazokuwa unakutana nazo.
Kuna njia moja ambayo ukiitumia utaweza kuchochea hamasa yako ya mauzo mara zote, hasa pale unapokuwa na hamasa ya chini. Njia hiyo ni ya kuchagua mteja bora kwako ndani ya mwezi mmoja uliopita kisha kupitia mambo yake ya msingi. Kupitia mteja huyo, kuna vitu ambavyo utajifunza na vitakupa msukumo wa kuendelea kuwafikia wateja wengi zaidi na kufanya mauzo makubwa.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekushirikisha mambo ya kujitafakari kuhusu mteja wako bora kwa kipindi cha mwezi mmoja. Angalia kipindi hicho na uweze kuyatafakari maswali hayo kwa kina ili uwe na hamasa kubwa ya kukamilisha mauzo makubwa mara zote.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.