Njia mojawapo nzuri ya kumhudumia mteja ni kuonyesha unamjali. Yaani, mteja anaona wazi kuwa anapendwa kulingana na namna unavyompokea na unavyomsikiliza.

Sisi binadamu tunayo hisia ya sita ambayo huwa inaona namna gani tunapenda au mtu anatujali. Kupitia kugusa hisia zetu, kulingana na mahitaji tunayotaka. Ndiyo maana utakuta wateja wanasema;

Unajua siku hizi muuzaji fulani, aongei kama zamani!

Hivi sivyo mlivyokuwa katika utoaji wa huduma zenu!

Mh! Leo umepoa sana, sio kawaida yako!

Hii ina maana kwamba, wateja waona utofauti fulani ikilinganishwa na siku za nyuma.  Unapomjali mteja anaona na anajua kabisa kuanzia kwenye hisia hata kama ni mara ya kwanza. Hapa chini nimeelezea baadhi ya mambo yanayofanya mteja aone kama unamjali;

Moja; Ukaribisho Mzuri
Moja ya utofauti wa midoli na binadamu. Yaani mtu wa mauzo dukani ni ule ukaribisho au namna ya kuongea. Midoli haiongei na haiwezi kumshawishi mteja, wala kumkaribisha lakini binadamu tunaweza kufanya hivyo. Kwa hiyo, jukumu la kwanza kufanya unapokutana na mteja ni kumkaribisha vema. Kisha kumuuliza juu ya hitaji lake huku ukionyesha tabasamu mbele yake.

Mbili; Lugha Inayoeleweka
Mara baada ya kumkaribisha mteja iwe mazungumzo ya ana kwa ana au simu, lugha nzuri ni muhimu sana. Hasa lugha inayoeleweka na kusikika vema. Hii ni kwa sababu mteja pia, anahitaji kueleweka. Kama haelewi lugha yako ni ngumu kuongea hitaji lake. Hivyo, epuka kutumia lugha zenye misamiati migumu.

Tatu; Bidhaa Bora
Pamoja na ukaribisho mzuri kwa mteja wako, bado ubora wa bidhaa una nguvu kubwa sana. Wateja wamechoka na kuuziwa vifaa vilivyo chini ya kiwango. Lakini unapompatia kitu kizuri ni rahisi yeye kuona thamani yake na kujisikia vizuri. Ubora wa bidhaa zako ndio hukutofautisha na washindani wako.

Nne; Kumsikiliza
Kusikiliza ni sanaa iliyosahaulika sana. Hasa katika zama ambazo mambo yanazidi kuwa mengi na muda mchache. Unapoonyesha kumsikiliza mteja anafurahi na kujisikia vizuri. Hii ni kwa sababu saikolojia ya mteja mara zote huwa ipo kwenye kusikilizwa yaani kile anachozungumza kinatiliwa maanani. Na udhahifu wa wateja upo kwenye kusikilizwa. Mara zote wanatamani suala lao litiliwe maanani na kufanyiwa kazi.

Tano; Thamani
Thamani ya mteja inaanzia pale anapofika Katika biashara au huduma yako. Kuanzia namna unavyompokea na unavyomsikiliza na kumjibu kulingana na mahitaji yake. Usiishie tu hapo msifie huone namna anavyojiona wa thamani sana. Kingine katika hili ni kumpatia mfano au ushuhuda mteja wako. Usiishie tu kuelezea bidhaa juu kwa juu. Mfanye ashike kama kuna uwezekano, inasaidia pia kupunguza mapingamizi.

Sita; Kumshukuru mteja .
Mteja akishanunua kwako au kufika katika huduma yako mshukuru angalau kwa kumpa mkono au kutumia ujumbe wa shukurani ndani ya saa 24.  Unaweza kuona ni kitu kidogo lakini kinamfanya mteja kujisikia vizuri. Hakuna asiyependa kushukuriwa. Kumbuka, kushukuru ni kuomba au kukaribisha tena.

Weka akilini kwamba mtaji wa kwanza ulionao ni watu. Watu hao ni wateja wako, ukiwajali utakuwa unawaweka karibu yako na kuongeza mauzo yako.

Muonyeshe mteja kwamba haupo pale kwa sababu unataka pesa, bali upo kunamsaidia kutatua matatizo yake. Atajisikia vizuri na kutoa pesa yake huku moyo wake akiwa ameufungua.

Muhimu: Fanyia kazi kitu kimoja ulichojifunza katika somo hili.

Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo Na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.