3369; Uongozi sahihi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Ukubwa wa mafanikio unayoweza kupata kwenye maisha yako unategemea sana uimara wako kama kiongozi.
Ni namna unavyoweza kuwaongoza watu vizuri ndiyo itaamua ni watu wengi kiasi gani watakaokufuata na kufanya yale unayowataka wafanye, ambayo yana manufaa kwa kila mmoja na wote kwa ujumla.

Kitu cha kwanza unachopaswa kujua ni kwamba watu wengi siyo viongozi bali wafuasi.
Wanachofanya ni kutafuta kiongozi ambaye anaendana nao na kumfuata kwa  sababu wanaona nafasi ya kufika kule wanakotaka.
Hivyo kiongozi hatengenezi wafuasi, bali anawaonyesha yeye ni mtu sahihi kwao.

Kazi kubwa ya kiongozi ni kuwa na maono makubwa ambayo anayaamini na kuyasimamia na kuwashawishi watu washirikiane naye katika kuyapambania maono hayo.
Na hapo ndipo kazi kubwa zaidi ya uongozi ilipo, ya kuwaongoza watu kuhakikisha wanafanya ambayo hawapendi kufanya, ila yana manufaa kwao.

Kitu kikubwa ambacho wafuasi wanataka kukiona ni kiongozi naye akiwa anafanya. Wanataka kiongozi awe mfano kwenye kufanya yale anayosimamia.
Haijalishi kiongozi anasema nini, wafuasi wanaangalia anafanya nini.

Na bahati mbaya sana kwa kiongozi ni kila wakati anaangaliwa na wafuasi wake. Kila anachofanya kinatafsiriwa kama ndiyo utaratibu unaopaswa kufuata. Na kile asichofanya kinaonekana siyo muhimu sana.

Pale ambapo watu hawafanyi yale wanayopaswa kufanya, inaweza kuwa rahisi kuwalaumu kwa kushindwa kwao kufanya. Lakini hizo ni lawama zinazotakiwa kwenda kwa kiongozi, kwa sababu yeye ndiye anayekuwa amewafanya watu wasifanye, kutokana na yale anayokuwa amefanya au kutokufanya.

Kwa sehemu kubwa, kile ambacho wafuasi wanafanya au kutokufanya inachochewa na kiongozi.
Kiongozi ndiye kioo chao, ambaye anaangaliwa kwenye mambo yote.
Bila ya kuwepo na uongozi sahihi, hata watu ambao ni wazuri kabisa wataishia kushindwa kufanikisha makubwa ambayo wangeyaweza.

Kwenye jamii ya tofauti ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo tunaijenga, kila mmoja ni kiongozi kwenye maisha yake na biashara anayojenga.
Hivyo tangu mapema anajijenga kama kiongozi bora kwa kuwa mfano mzuri kwenye mambo yote yanayopaswa kufanyika.

Kama kiongozi, kila mmoja wetu anapaswa kuchagua kwa usahihi wale ambao ataambatana nao kwenye safari yake ya mafanikio.
Na baada ya kuwachagua kwa usahihi, kinachofuata ni kuwapa uongozi mzuri ili kuhakikisha wote wanaleta ushirikiano mzuri kwenye safari nzima.

Kuwa na maono makubwa, unayoyaamini na kuyasimamia ni wajibu wako kama kiongozi.
Kuwa mfano kwenye kuyapambania maono hayo ni kitu ambacho wafuasi wanataka kukiona.
Kuweka viwango vya juu vya utendaji ambavyo kila mmoja anapaswa kuvizingatia ni hitaji muhimu kwenye kuhakikisha watu wanajisukuma zaidi.

Huwezi kuyapata mafanikio makubwa unayoyataka kama hutakuwa kiongozi sahihi kama ulivyojifunza hapa.
Waongoze watu kwa mfano na wafanye wawe tayari kufanya wasiyoyapenda, lakini yenye manufaa kwao.
Ni kadiri watu wanavyoona maisha yao yakiwa bora chini ya uongozi wako ndiyo wanaendelea kuwa wafuasi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe