
Kwenye maisha, kila mmoja kuna eneo analolijua kwa ukubwa kuliko maeneo mengine. Hali hii ndiyo hufanya tuweze kuwa na utegemezi mkubwa katika kukamilisha baadhi ya mahitaji yetu.
Unaweza kuwa vizuri katika eneo la fedha, lakini eneo la mahusiano likakupa changamoto. Unaweza kuwa vizuri kwenye vifaa vya gari lakini ufundishaji wa lugha ya kiswahili au masuala ya kiafya yakakupa shida.
Kushindwa kujua vema eneo lingine hayo ndiyo mapungufu tuliyonayo. Hata kwenye biashara ipo hivyo, utakuwa vizuri kwenye nguo lakini spea huzijui. Ndiyo maana kuna biashara zinakua na baadhi zinadidimia. Hasa zile ambazo wahudumiaji wake hawataki kutumia madhaifu au mapungufu ya wateja kuwauzia.
Kuna mapungufu yanayooneka na moja kwa moja na yasiyoonekana moja kwa moja. Tuchukulie mfano wa nyumba. Tunajua kila nyumba lazima iwe na madirisha kwa ajili ya kupitishia hewa. Ikitokea ukajenga nyumba ambayo haina madirisha. Au umevaa suti mpya, chini kandambili. Automatically mtu atahisi kiakili aupo sawa.
Kadhalika kwenye ufuatiliaji wa wateja kuna mapungufu mengi tunayabaini kwa wateja hao. Ni wajibu wetu kuyatumia kuwauzia.
Mfano mzuri ni matapeli, wakigundua wewe ni mgeni mjini wanatumia mwanya huo kukuibia. Huku wakikuonyesha dollar na dhahabu bandia.
Baadhi ya mapungufu ya wateja ni kama yafuatayo;
Moja; Ukosefu wa taarifa za kutosha kuhusu bidhaa zako.
Hili lipo wazi, ni kwa sababu huwezi kujua kila kitu, hivyo mteja anapokuja kwako, na ukagundua hana taarifa za kutosha kazi yako ni kumshawishi kununua kupitia kumpatia taarifa sahihi. Mfano mzuri ni hospitali. Daktari atakupa taarifa sahihi kupitia vipimo husika, mwisho wa siku unalipia vizuri pesa kupata tiba.
Mbili; Kutojua matumizi ya baadhi ya bidhaa kisawasawa.
Hali hii humpatia nafasi mtu wa mauzo kukuuzia, hasa kupitia ufafanuzi mzuri anaokupa kuhusu bidhaa fulani. Unaweza kujua kidogo matumizi ya kitu, lakini ukipewa ufafanuzi mzuri ni rahisi kumshawishika kununua.
Namna nzuri ya kujua mapungufu hayo ni kupitia maswali na kukaa kimya. Watu wanapenda kuongelea vitu wanavyopenda na kuvithamini. Kwa lugha rahisi ngoma anavyoipiga na mteja ndivyo unavyopaswa kuicheza.
Kuuza ni vita, japo siyo ya umwagaji damu. Hivyo, unapokuwa katika vita hii ustaarabu pekee ni kukamilisha mauzo. Iwe jua au mvu, hakikisha unayajua mapungufu ya mteja na kutumia mwanya huo kumuuzia.
Tahadhari katika upande wa mapungufu, ukiona mapungufu kwa mteja epuka kumwambia wazi wazi kwamba hapa sio sawa au umekosea. Mteja yupo sahihi mara zote. Msifie, kisha mweleze katika namna rahisi pasipo yeye kugundua. Mfano, umegundua ramani yake imekosewa, usiseme hii ramani haifai. Mwambie sina uhakika kama itakufaa lakini kama ungeongeza na hiki au kufanya hivi kwenye hii ramani ingekuwa na mwonekano mzuri.
Muhimu zaidi ni kufanyia kazi kile ulichojifunza kutoka somo la leo.
Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.