3397; Ziba kwanza panapovuja.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kama unaweka juhudi kubwa lakini matokeo unayopata ni madogo kuliko ulivyotarajia, anza kwa kuangalia ni wapi pana upotevu.

Ni sawa na kuwa na ndoo unayotaka kuijaza maji, unaweka maji mengi lakini bado haijai.
Hapo ni lazima uangalie ndoo yako kwanza kujihakikishia kwamba haivuji na kama inavuja basi iweze kuzibwa.

Ili juhudi unazoweka ziweze kuleta matunda, ni lazima ziweze kujikusanya kwa pamoja kwa muda mrefu.
Hivyo kuhakikisha hakuna juhudi zinazovuja ni zoezi muhimu kuliko hata hata kuziweka juhudi zenyewe.

Kwenye fedha, ili kujenga utajiri mkubwa, ni lazima kwanza udhibiti matumizi yako. Kama matumizi yanaendelea kuongezeka kadiri kipato kinavyoongezeka, huwezi kujenga utajiri, hata kama kipato chako kitakuwa kikubwa kiasi gani. Lakini pia unapaswa kuepuka madeni ambayo yanazidi kunyonya utajiri wako.
Kwa kuleta hayo pamoja, ili kujenga utajiri, tumia kidogo kuliko ulivyopata, wekeza kiasi hicho cha ziada na epuka madeni.

Kwenye kujenga biashara, unapaswa kuwa na timu nzuri ya kuendesha biashara hiyo. Timu nzuri ni matokeo ya kuajiri vizuri na kutoa mafunzo sahihi kwa wote.
Kuajiri vizuri kunaanza na kuchagua watu wenye sifa zinazohitajika ili kukamilisha majukumu yaliyopo.
Na mafunzo yanahusisha kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao.
Kama biashara kila wakati itakuwa inapoteza watu kwenye timu, kila wakati itakuwa ni kama inaanza upya.
Unapaswa kuziba matundu yanayowavujisha watu ambao bado wanahitajika kwenye biashara.


Kwenye mauzo, unapaswa kuwabakisha wateja kwenye biashara kwa muda mrefu zaidi. Kuuzia wateja ambao wamewahi kununua ni rahisi kuliko kuwauzia ambao ni wapya kabisa.
Kama biashara kila wakati inahangaika kutafuta wateja wapya, maana yake inavujisha wateja ambao wameshanunua.
Kazi kubwa inapaswa kufanyika ili kuziba matundu yote yanayowapoteza wateja kwenye biashara.
Kutoa thamani kubwa na huduma bora, huku ukijenga na kuimarisha mahusiano na wateja, itapunguza sana wateja wanaopotea.

Kupata matokeo yoyote makubwa unayoyataka kwenye maeneo yote ya maisha yako, hakikisha juhudi unazoweka hazipotei bure.
Unapaswa kujua matundu yanayovujisha juhudi unazoweka kisha kuyaziba ili juhudi ziweze kujikusanya na kukupa matokeo makubwa unayoyataka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe