Tupo kwenye dunia ambayo huwezi kufanya kila kitu au kuwa na kila kitu mwenyewe. Unahitaji msaada wa baadhi ya maeneo kukamilisha vitu fulani kwenye utendaji wako.

Moja ya eneo muhimu kulikamilisha kwenye siku yako ni mauzo kupitia kupitia kuomba msaada kwa wateja unaowafuatilia.

Iko wazi kwamba, kuomba msaada ni sehemu ya maisha yetu, hii ni kwa sababu pale unapoona mwenzako yuko bora katika eneo fulani, omba msaada akusaidie na wewe uwe bora.

Kwenye mauzo, ukishindwa kuuza kwa sababu ya kukosa msaada ni kama vile kufa na kiu huku ukiwa kisimani. Usipoomba hupati. Wewe hujiulizi kwa nini Mungu alisema ombeni nanyi mtapewa?

Maeneo muhimu kuomba msaada;

Moja; Wateja wa rufaa

Mbili; Mawasiliano

Tatu; Maeneo fulani ambayo hatuyajui.

Nne; Kuomba kuonana na bosi au mkurugenzi

Tano; Mkutano unaofuata

Sita; Mauzo ya ziada.

Haya ni baadhi tu ya maeneo unayoweza kuomba usaidizi wakati wa ufuatiliaji.

Chochote kile unachotaka, usione aibu kuomba. Kila binadamu anaomba msaada na watu siyo wachoyo pale unapokuwa unawaomba juu ya kitu fulani halafu wakaasha kukusaidia.

Wewe mwenyewe unajijua, ni eneo gani ambalo linakusumbua lakini kuna watu ambao unawajua wanafanya vizuri na unaweza ukawaomba msaada na wakakusaidia.

Umuhimu wa kuomba usaidizi;

Moja; Kukuza mahusiano
Sisi binadamu ni viumbe wa mahusiano. Tupo tayari kutoa msaada pale anapotuomba.Rejea mfano wa msafiri anayeuliza barabara ya kwenda eneo fulani, mtu yupo tayari kuacha shughuli zake na kukusaidia.

Mbili; Kukuza mauzo.
Kuna wakati katika ufuatiliaji wa mteja unaona wazi unaenda kukosa mauzo, badala ya kumuacha mteja aondoke unamuomba mteja kuchukua angalau achukue bidhaa ndogo au moja kwa ajili ya majaribio.

Tatu; Kujifunza zaidi
Kwenye mauzo kupitia kuomba msaada kwa watu tofauti utaelewa vema mwitikio wa wateja, maamuzi na mengine mengi. Hii itakufanya kuboresha sikripti yako.

Nne; Kupata unachotaka
Kujitegemea ni kuzuri, lakini siyo kujitosheleza. Usiogope kuomba msaada, omba msaada na utapata kile unachotaka kutoka kwa wengine.

Kumbuka; Mwili wetu wenyewe, umeumbwa katika utegemezi wa viungo vingine. Jicho linategemea zaidi moyo kuwa na ufanisi mzuri, miguu inategemea macho na mikono kadhalika na viungo vingine, japo kila kimoja kinafanya kazi kwa wakati wake.

Hatua ya kuchukua leo; usiogope kuomba msaada, ombeni nanyi mtapewa, usiache kuomba msaada pale unapokuwa katika hali ya kuhitaji kitu kutoka kwa mteja.

Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi msaidizi wa Chuo Cha Mauzo. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.