Rafiki yangu mpendwa,
Maisha huwa yana kupanda na kushuka mara zote. Kwa bahati mbaya sana, tumekuwa tunachukulia hali hizo tofauti na uhalisia wake.
Pale mambo yanapokuwa mazuri, huwa tunajisahau na kuona yataenda hivyo milele. Matokeo yake ni kuja kupata anguko kubwa baadaye tukiwa hatuna maandalizi yoyote.
Lakini pia pale mambo yanapokuwa magumu, huwa tunakata tamaa kwa kuona yataendelea hivyo milele. Matokeo yake ni tunajizuia kupiga hatua na hata pale fursa ya mambo kuwa mazuri inapojitokeza, tunashinda kuitumia kwa manufaa.

Rafiki, unachopaswa kujua ni kwamba chochote unachopitia kwenye maisha yako ni kwa muda tu. Hakuna chochote ambacho kinadumu milele, maana hata wewe mwenyewe hutadumu milele.
Wajibu wako kwenye maisha, ili yawe ya mafanikio, ni kukabiliana na kila linalokuja mbele yako, kwa wakati ambao linakujia. Kamwe usiangalie kesho ikiwa kama leo, bali ione kesho ikiwa tofauti kabisa kulingana na juhudi unazoweka leo.
Unapokuwa unapitia nyakati nzuri, usijisahau wala kufanya kwa mazoea. Badala yake chukulia kesho mambo yatakuwa tofauti kabisa, hivyo fanya kwa ubora zaidi leo na jiandae hata kama kesho mambo yatakuwa mabaya, basi uwe na mahali pa kuanzia.
Wengi sana ambao wanaonja mafanikio kidogo na kuanguka ni kwa sababu walijisahau pale mambo yalipokuwa yanawaendea vizuri. Hawakujua mambo hubadilika na hivyo kutokuwa na maandalizi ya kutosha. Pale mambo yalipobadilika, wakaishia kupoteza kila kitu.
Pale unapokuwa unapitia magumu na changamoto na maisha kuonekana kama hayawezekani, tambua hali haitakuwa hivyo milele. Jua ni kipindi cha mpito tu hicho na wajibu wako ni kukivuka salama ili mambo yanapokuwa mazuri uweze kuzitumia fursa zinazojitokeza.
Hata kama unapitia mambo magumu kiasi gani, kama tu upo hai, endelea kupambana bila ya kukata tamaa. Mafanikio ya kwanza ni kuendelea kufanya bila kuacha na kufanya kwako kwa msimamo ndiyo kunaleta mafanikio ya pili ambayo ni matokeo.
Haijalishi magumu unayopitia umeenda nayo kwa muda mrefu kiasi gani, usikate tamaa. Lakini pia usikae na kusubiri mambo yawe mazuri yenyewe. Mambo huwa hayawi mazuri yenyewe, badala yake huwa yanafanywa kuwa mazuri, kwa juhudi ambazo zinawekwa.
Kila wakati wa maisha yako unapaswa kuwa unaweka juhudi kubwa zaidi kuyafanya mambo kuwa bora zaidi ya yanavyokuwa. Kama unafanya vizuri, weka juhudi kubwa ili kufanya vizuri zaidi. Na kama unafanya vibaya, weka juhudi kubwa ili uweze kufanya vizuri.
Pale utakapoacha kufanya, ndiyo utakuwa umekaribisha anguko kubwa na litakalokuondoa kabisa kwenye mchezo wa mafanikio. Maana mafanikio ni sawa na kuendesha baiskeli, kadiri unavyokuwa kwenye mwendo ndivyo inavyosimama, ukiacha kuchochea inayumba na kuanguka.
Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini uendelee kujifunza kwa kina zaidi dhana hii ya mambo kuwa ya mpito na hatua sahihi kuchukua ili ufanikiwe.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.