Rafiki yangu mpendwa,

Maisha ni mchezo mmoja mkubwa sana, ambao ndani yake kuna michezo mbalimbali.

Kuna michezo ya mahusiano, michezo ya fedha, michezo ya biashara, uwekezaji n.k.

Wanaofanikiwa kwenye maisha ni wale wanaoelewa michezo wanayocheza na kuweka sheria na masharti ambayo yanawapa ushindi wa uhakika.

Kwa kuwa michezo ambayo utacheza kwa kipindi chote cha maisha yako ni mingi, unahitaji kanuni ya jumla ambayo ukitumia kwenye mchezo wowote ule, ushindi unakuwa uhakika kwako.

Kwa bahati nzuri sana, kuna sheria tatu ambazo ukizijua na kuzibobea, kisha kuzitumia kwenye kila mchezo wa maisha, ushindi unakuwa wa uhakika kwako.

Sheria Ya Kwanza; Amua Sheria Za Mchezo.

Wewe ndiye unayepaswa kuamua zipi sheria za mchezo ambao unaucheza. Na hapa ina maana unachagua mchezo wewe na kuweka sheria ambazo utazifuata kwenye mchezo huo.

Kwenye safari ya mafanikio hapa ni kutengeneza mchakato wako wa mafanikio ambao utaufuata mara zote bila ya kuuvunja. Mchakato wa mafanikio ndiyo sheria kuu ambayo ukiifanyia kazi, unapata ushindi kwa uhakika.

Pale unapoiga michezo ya wengine, ambapo huelewi michakato yao, unaishia kushindwa vibaya. Usikubali kuingia kwenye mchezo ambao hujaweka sheria wewe mwenyewe.

SOMA; 1587; Mchezo Wa Maisha Ni Kugeuza Kila Kitu Kuwa Zawadi…

Sheria Ya Pili; Hakikisha Unakuwa Na Upendeleo.

Michezo yote unayocheza kwenye maisha yako, hakikisha wewe una upendeleo wa kupata ushindi. Kwenye maisha bila ya upendeleao ni vigumu kupata ushindi na mafanikio makubwa. Lazima utafute upendeleo ambao wengine hawana.

Kwenye safari yako ya mafanikio upendeleo ni kufanya vitu ambavyo una vipaji na uwezo wa kipekee, ambao wengine hawana. Kuna vitu ambavyo wewe unaweza kuvifanya vizuri kuliko watu wengine. Hivyo ndiyo vitu ambavyo ukijenga mafanikio yako hapo, hakuna anayeweza kukushinda.

Kwa kutumia vipaji na upekee wako kufanikiwa, wengine watahangaika sana lakini hawataweza kukufikia. Kwa sababu kile ambacho kwao ni kazi kubwa, kwako ni kama mchezo tu ambao unaufurahia.

Hakikisha pia huingii kwenye mchezo wa wengine, ambapo wao tayari wana upendeleo kuliko wewe. Usiingie kwenye kufanya kitu kwa sababu umeona wengine wananufaika nacho, angalia kwanza kama wana upendeleo ambao wewe huna. Utashinda kwa uhakika pale upendeleo unapokuwa upande wako.

Sheria Ya Tatu; Amua Wakati Wa Kuacha Kucheza.

Tatizo la michezo mingi kwenye maisha ni kusogeza magoli mbele baada ya kupata ushindi. Hakuna ubaya wowote kwenye kuongeza malengo ya ushindi, lakini lazima ujue ni mchezo tu. Usiache kuyaishi maisha yako kwa kumezwa na michezo ya maisha. Unapaswa kujua wakati sahihi wa kuacha kucheza mchezo wowote ule na kwenda kwenye mchezo mwingine, wa juu zaidi au ambao ni bora zaidi.

Tabia ya kuishi kwa mazoea ndiyo imekuwa inawafanya wengi kuchelewa kuondoka kwenye michezo ambayo walianza nayo. Wewe kuwa mbele ya muda mara zote kwa kujua wakati sahihi wa kuacha mchezo kwa sababu mbalimbali unazokutana nazo.

Zingatia sheria hizo tatu na utaweza kuicheza michezo yako yote ya maisha kwa ushindi wa uhakika.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimefafanua zaidi kuhusu sheria hizi tatu na jinsi ya kuziishi kwa uhakika kwenye maisha yako na kunufaika. Karibu uangalie kipindi na kujifunza.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.