3407; Ni kurudia rudia kusema.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Tumekuwa tunajifunza kwamba kwenye mafanikio, hakuna kitu utafanya mara moja kikawa kimetosha.
Badala yake unapaswa kurudia rudia kufanya kwa muda mrefu.
Hivyo ndivyo mafanikio makubwa yanavyojengwa.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mawasiliano.
Chochote unachowaambia watu, unapaswa kurudia rudia kusema bila ya kuchoka.
Usiwaambie watu kitu mara moja au chache na ukadhani umemaliza kazi yako.
Bado hakuna kitu umefanya kama utaacha kuwakumbusha mara kwa mara.
Watu wamezungukwa na usumbufu mwingi na mkubwa, hivyo inawachukua muda sana kuelewa kile unachotaka wakijue.
Na hata wakijua na kuelewa, wanasahau haraka sana kwa sababu ya huo usumbufu unaowazunguka.
Hivyo ni lazima urudie rudie kuwaambia bila ya kuchoka.
Ni kuwakumbusha kwa msimamo na bila ya kuchoka kile unachotaka waelewe.
Ni bora watu wasikie kitu mara nyingi na kuchoshwa na hilo, kuliko kusikia mara chache na wasielewe.
Unapokuwa kiongozi wa biashara, unakuwa na cheo cha afisa mtendaji mkuu (CEO – Chief Executive Officer).
Kuna cheo cha pili kinaongezeka hapo, ambacho ni afisa mkumbushaji mkuu (CRO – Chief Reminding Officer).
Majukumu yako kwenye cheo cha afisa mkumbushaji mkuu ni kurudia rudia kuwakumbusha wale unaowaongoza kwenye biashara yako kusudi, maono, misingi, mikakati na vipaumbele vya biashara.
Wajibu wako ni kila aliye kwenye biashara aweze kuelewa hayo na kuyaimba kabisa, kwa sababu ameyasikia mara kwa mara mpaka yamemkaa.
Mtoto mdogo, ambaye hata hajui kusoma na kuandika, anaweza kukuimbia wimbo fulani mpaka ukashangaa.
Sababu ya kuweza hivyo ni kwa sababu wimbo huo anakuwa ameusikia kwa kurudia rudia kwa muda mrefu.
Hivyo kipimo cha utekelezaji wa jukumu lako la kukumbusha ni kama kila aliye kwenye biashara anayaelewa yale yote ya msingi kuhusu biashara yako.
Kama watu hawawezi kurudia kusema kwa maneno yao wenyewe na kwa usahihi, basi jua hujafanya kazi yako vizuri.
Kuna vitu unaweza kuwa unavisema, lakini bado watu wakafanya kinyume na vile unavyosema.
Unaweza kudhani watu hao wana dharau, iweje wafanye tofauti na ambavyo umekuwa unaelekeza?
Lakini nikuambie tu, kwa sehemu kubwa watu hao hawajasikia au kuelewa ulichokuwa unasema.
Kwa kifupi ni unakuwa hujarudia rudia kusema kwa msimamo kiasi cha kueleweka kwa uhakika.
Hivyo unapaswa kurudi kwenye kurudia kuelekeza, tena na tena na tena.
Utalazimika kuwa kama kanda mbovu, ambayo inarudia pale pale bila ya kuacha.
Huhitaji hata kuwa unasema mambo mengi, bali machache ya msingi na kuyarudia rudia bila ya kuchoka.
Kwenye mawasiliano yako yote unayofanya na watu, unapaswa kuwa na ujumbe wako mkuu ambao unarudia rudia kuutoa ili watu wauelewe na kuchukua hatua unazotaka wachukue.
Piga kelele sana na ujumbe huo, endelea kuutoa kwa kurudia rudia bila kuacha.
Jua wengi bado hawajausikia,
Waliousikia hawajaelewa,
Na walioelewa watasahau haraka.
Suluhisho; RUDIA RUDIA KUSEMA.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe