Rafiki yangu mpendwa,
Watu huwa wanadhani utajiri ni kitu ambacho kinaweza kutokea tu kwa mtu kwa sababu anakitaka sana. Au kwa sababu ana mtazamo chanya juu ya fedha na utajiri.
Kutaka na kuwa na mtazamo chanya, ni sehemu ndogo sana ya kujenga utajiri, sehemu kubwa zaidi ipo kwenye hatua ambazo mtu anachukua kwenye kuujenga utajiri.
Kujenga utajiri ni kazi ambayo imekamilika, kazi ambayo inakutaka uweke juhudi kubwa sana ili kuweza kufanikiwa. Unapowaona walioweza kujenga utajiri, ni kwa sababu walichukulia hiyo kama kazi na kuifanya kwa viwango vikubwa.

Kwenye sehemu ya pili ya kitabu cha THE RULES OF MONEY kilichoandikwa na Richard Templar, ametupa sheria za kuzingatia kwenye kujenga utajiri ili tuweze kupata utajiri mkubwa.
SEHEMU YA PILI; KUPATA UTAJIRI.
Sehemu ya kwanza ya kitabu ilikuwa kuhusu kufikiri kitajiri. Sasa tunaingia kwenye sehemu ya vitendo ambayo ni kujenga utajiri.
Ili kujenga utajiri lazima uwekeze muda na nguvu kwenye kufanya yale yanayoleta utajiri.
Sheria ya 20; Unapaswa kujua ulipo kabla ya kuanza.
Kufika kule unakotaka kwenda, lazima ujue ni wapi unapoanzia. Jifanyie tathmini ya pale ulipo sasa kwa upande wa kipato, matumizi, mali, madeni na mengine. Hiyo itakuwezesha kujua ni kazi kiasi gani iko mbele yako.
Sheria ya 21; Unapaswa kuwa na mpango.
Mpango ndiyo njia ya kuyafikia malengo uliyonayo kwenye utajiri, bila ya mpango hutaweza kupata matokeo mazuri. Weka mpango ambao utaufanyia kazi ili kujenga utajiri.
Sheria ya 22; Dhibiti fedha zako.
Kuna matundu mengi ambayo yamekuwa yanapoteza fedha zako kama matumizi yasiyo ya msingi, riba na gharama nyingine unazokuwa unaingia kwenye yale unayofanya. Ziba matundu yote yanayopoteza fedha ili upate utajiri.
Sheria ya 23; Kuwa na bima sahihi kwako.
Bima ni nzuri kwenye kuokoa gharama mbalimbali, lakini kuwa na bima nyingi na zisizo za msingi ni kikwazo kwenye kujenga utajiri. Kuwa na bima sahihi na za msingi kama bima ya afya na mali na kwa vitu vingine, kuwa na akiba ya dharura badala ya kulipia bima.
Sheria ya 24; Kuwa na mwonekano wa kitajiri.
Mwonekano wako una mchango kwenye utajiri unaojenga. Ili kujenga utajiri, kuwa na mwonekano wa kitaji, hiyo haimaanishi uwe na matumizi makubwa, bali uwe na mavazi safi na nadhifu na uwe unajiamini.
Sheria ya 25; Bahatisha ili kukusanya utajiri.
Kabla mtu hajapata utajiri, watu hawajihangaishi naye. Lakini mtu akipata utajiri, anaonekana kama amepata bahati fulani. Nyuma ya kila bahati ni juhudi kubwa sana ambazo watu wanakuwa wameweka. Weka juhudi bila kuchoka na utajiweka kwenye nafasi ya kupata bahati.
Sheria ya 26; Amua mtazamo wako kwenye hatari.
Ili kujenga utajiri ni lazima uchukue hatua ambazo ni za hatari. Lakini hupaswi kuchukua hatari za kila aina, bali zile ulizokokotoa na kuona unaweza kuzihimili. Chukua hatari ambazo hata ukipoteza, hupotezi kila kitu.
Sheria ya 27; Fikiria mbadala wa hatari.
Kwa kila hatua ya hatari kuchukua, fikiria nini mbadala wake. Linganisha hatari unayopaswa kuchukua na mbadala wake kisha amua kwa usahihi.
Sheria ya 28; Kama humwamini mtu, usifanye naye biashara.
Sikiliza machale yako na sauti ya ndani, kama kuna wasiwasi unao juu ya mtu, jiridhishe kwanza kabla ya kushirikiana naye.
Sheria ya 29; Hujachelewa kuanza kujenga utajiri.
Haijalishi umri wako ni mkubwa kiasi gani, safari ya utajiri ni wakati wowote unapoianza, hakuna kuchelewa. Kuwa tayari kuianza safari hiyo wakati wowote na kuweka kazi inayohitajika.
Sheria ya 30; Anza kuweka akiba mapema na wafundishe watoto wako pia.
Kuweka akiba ni msingi muhimu kwenye kujenga utajiri. Anza mapema na pia wafundishe watoto wako waanze kuweka akiba mapema.
Sheria ya 31; Elewa mahitaji yako ya kifedha yanabadilika kwenye hatua tofauti za maisha.
Kila hatua ya maisha inakuwa na mahitaji yake tofauti. Usibweteke kwa mahitaji madogo ya sasa, wakati yajayo yanakuwa makubwa zaidi.
Sheria ya 32; Inabidi ufanye kazi kwa juhudi kujenga utajiri ili usilazimike kufanya kazi kwa juhudi.
Juhudi unazoweka sasa kwenye kazi, unafanya baadaye usilazimike kuweka juhudi kubwa sana. Maana ukishajenga utajiri, unaweza kuendeleza bila ya juhudi kubwa.
Sheria ya 33; Jifunze sanaa ya kufanya dili nzuri.
Utajiri unajengwa kwa kufanya dili nzuri, ambapo kunatokana na kujua kile unachotaka kutoka kwa wengine na kile ambacho uko tayari kuwapa.
Sheria ya 34; Jifunze sanaa ya majadiliano.
Katika kushirikiana na wengine, kuna mambo mbalimbali yatakayohitaji majadiliano. Kuwa bora kwenye majadiliano kwa kuhakikisha kila upande unapata ushindi.
SOMA; Sheria Za Fedha; Kufikiri Kitajiri.
Sheria ya 35; Uchumi mdogo hautakutajirisha.
Ni muhimu kudhibiti matumizi yako, hasa ambayo ni madogo madogo. Lakini hilo pekee halitoshi kukupa utajiri. Ni lazima uingize kipato kikubwa.
Sheria ya 36; Utajiri wa kweli unatokana na dili na siyo ada.
Kulipwa kwa muda au kazi ni kikwazo kwenye kujenga utajiri mkubwa. Utajiri unajengwa kwa kufanya dili, yaani kuuza na kununua kwa namna ambayo ina manufaa kwako.
Sheria ya 37; Elewa kuajiriwa hakutakupa utajiri, ila ni njia ya kuelekea kwenye utajiri.
Tatizo la ajira ni ukomo wa kipato, lakini ni mahali pazuri pa kuanzia kuweza kupiga hatua zaidi. Japo pia biashara huwa zina changamoto na za wengi huwa zinakufa.
Sheria ya 38; Usipoteze muda kuahirisha, fanya maamuzi ya fedha haraka.
Kadiri unavyochukua muda mwingi na kusita kufanya maamuzi, ndivyo maamuzi hayo yanavyokuwa ya hovyo. Fanya maamuzi yoyote kuliko kutokufanya maamuzi kabisa.
Sheria ya 39; Fanya kazi kama vile huhitaji fedha.
Ifanye kazi yako kwa uhuru mkubwa kwa kujiondoa kwenye mtego wa kuonekana unahitaji sana fedha. Kadiri unavyoonekana kutaka sana fedha, ndivyo unavyotawaliwa zaidi na wengine na kushindwa kujenga utajiri.
Sheria ya 40; Tumia pungufu ya kipao chako.
Sheria kuu ya kujenga utajiri ni matumizi kuwa chini ya kipato. Hivyo mara zote hakikisha fedha inayoingia ni kubwa kuliko inayotoka.
Sheria ya 41; Usikope fedha, labda kama una uhitaji mkubwa sana na huna namna nyingine.
Tatizo la mikopo ni riba inayotozwa na hiyo huwa inaleta gharama kubwa na kupunguza utajiri wa mtu. Ondoka kwenye madeni uliyopo na usichukue mikopo binafsi, inakukwamisha sana.
Sheria ya 42; Unganisha madeni uliyonayo.
Kama una madeni mengi na maeneo mbalimbali, unaweza kuyaunganisha yakawa deni moja ambalo utalilipa kwa unafuu.
Sheria ya 43; Jenga ujuzi utakaokulipa milele.
Ujuzi unaokulipa milele una sifa hizi; unahitajika, ni adimu na mgumu kwa wengi kuwa nao. Tumia uwezo na vipaji vyako kujenga ujuzi wa tofauti na utakaokulipa sana.
Sheria ya 44; Kipaumbele cha kwanza kiwe kulipa madeni.
Kama una madeni, angalia riba zake, pale riba ya deni inapokuwa kubwa kuliko faida unayoweza kupata, lipa kwanza madeni ili uache kupoteza fedha kwenye riba.
Sheria ya 45; Usitingwe na kupata pesa ya kula na kushindwa kujenga utajiri.
Usiwe mtu wa kuridhika haraka pale unapotimiza mahitaji yako. Badala yake endelea kujisukuma zaidi ili ujenge utajiri mkubwa.
Hii ni sehemu tu ya sheria za kujenga utajiri kutoka kwenye kitabu cha RULES OF MONEY. Kwenye somo linalofuata tunapata sheria nyingine zaidi.
Masomo yote ya kitabu cha THE RULES OF MONEY kilichoandikwa na Richard Templar, ambayo yana sheria zote za fedha za kujenga na kutunza utajiri, yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.
Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala mzuri juu ya sheria hizi za kufikiri kitajiri. Fungua na ujifunze ili uweze kufikiri kwa usahihi hasa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.