Rafiki yangu mpendwa,

Kila binadamu aliye hai, anao uwezo wa kupata mafanikio makubwa sana kuliko yale aliyonayo.

Hata wale ambao wanaonekana kufanikiwa sana, bado wanaweza kufanikiwa zaidi ya hapo.

Lakini hapa tuanze na wale ambao hata mafanikio madogo hawana, wale ambao wapo chini kabisa na maisha yao ni duni.

Je ni kweli wanao uwezo wa kujenga mafanikio makubwa? Vipi hali zao duni, mazingira magumu na vikwazo wanavyokabiliana navyo? Hivyo si vinawazuia kabisa kufanikiwa?

Rafiki, nataka tuanze na mfano mmoja ambao lazima utakuwa unaujua kabla hatujaendelea na somo hili.

Umewahi kuona kwenye familia ambayo ni ya kimasikini kabisa, ambayo ina watoto mbalimbali, baadhi wanabaki kwenye umasikini na wengine wanaweza kutoka kwenye huo umasikini na kujenga utajiri? Watoto hao wanakuwa wamezaliwa na kulelewa kwenye familia moja, lakini kwenye mafanikio wanatofautiana.

Pia umewahi kwenda eneo la kazi au biashara, ukakuta watu ambao wanafanya kazi au biashara zinazofanana na wameanzia ngazi sawa kwa muda mmoja, lakini baada ya muda mmoja anapata mafanikio na mwingine anabaki kawaida? Watu hao wanakuwa eneo moja na wanafanya kitu kimoja, lakini matokeo yanatofautiana.

Rafiki, kwa hiyo mifano tuliyoiona, ni dhahiri kwamba tofauti ya kufanikiwa na kushindwa haitokani na hali za nje ambazo watu wamekuwa wanazisingizia. Badala yake kutakuwa na hali fulani ya ndani ambayo ndiyo inaamua mtu afanikiwe au ashindwe.

Je hali hiyo ya ndani ni ipi? Na mtu anawezaje kuijenga ndani yake ili afanikiwe kwa uhakika?

Rafiki, hicho ndiyo nipo kukushirikisha hapa, kwa sababu nataka sana wewe rafiki yangu ufanikiwe.

Kitu kitakachoweza kukupa mafanikio makubwa ni KUWA NA MATAMANIO MAKUBWA.

Ndiyo rafiki, ili uweze kupata mafanikio makubwa ni lazima uwe na matamanio makubwa sana. Ni lazima utake kutoka hapo ulipo na kufika mbali zaidi. Ni lazima uchukie sana hapo ulipo, usiridhike nako kwa namna yoyote ile.

Matamanio makubwa ni moto unaopaswa kuuwasha ndani yako ambao utaunguza kila aina ya kikwazo kinachokuzuia kufanikiwa. Moto huo una nguvu ya kuunguza mitazamo hasi ambayo unayo, unaangusha kila kikwazo kinachosimama mbele yako.

Kwa jinsi safari ya mafanikio ilivyo ngumu, kama mtu huna matamanio makubwa, huwezi kuyavuka magumu na kufanikiwa. Ni matamanio makubwa ndiyo yanayokufanya uwe tayari kuteseka bila kukata tamaa, kwa sababu unajua ni nini hasa unachotaka.

Matamanio makubwa yanakufanya uwahi kuamka asubuhi na mapema kabla ya wengine, uweke kazi siku nzima na uchelewe kumaliza kazi na hata kulala. Pamoja na kuchelewa kulala, huku umechoka, bado unaamka tena mapema ukiwa na nguvu ya kwenda kufanya makubwa zaidi.

SOMA; 2963; Imani na matamanio makubwa.

Rafiki, ukiweza kuwasha huo moto wa matamanio makubwa ndani yako, dunia haiwezi kukuzuia kwa namna yoyote ile. Badala yake itakupisha uende kupata kile unachotaka.

Hivyo ndivyo watu wawili, wanaofanana kabisa kwa nje wanavyoweza kutofautiana kwenye matokeo, kwa sababu ya kutofautiana kwa ule moto wa ndani.

Kwenye jamii nyingi, matamanio makubwa yamekuwa yanaonekana kama kitu kibaya. Watu wenye matamanio makubwa wamekuwa wanaonekana kama wasiojali wala kutosheka. Lakini huo ni mtazamo ambao wenye matamanio makubwa wanaupuuza, kwa sababu wanajua hauna mashiko kwao.

Wao wamechoshwa na pale walipo na wapo tayari kulipa gharama yoyote kutoka hapo. Wengine wanawachukuliaje hilo ni jambo ambalo haliwasumbui. Kilicho muhimu kwao ni kupata kile wanachotaka na kwa moto mkubwa wa mafanikio ndani yao, huwa wanakipata kweli.

Rafiki, anza kwa kuwasha moto wa matamanio makubwa ndani yako. Tayari moto huo umekuwepo, lakini umefifia kwa sababu uliupuuza. Sasa ni wakati wa kuuchochea ili uweze kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yako.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimekushirikisha hatua za kuchukua ili kuwasha huo moto wa matamanio makubwa ndani yako. Jifunze kwenye kipindi hicho na uchukue hatua ili upate mafanikio makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.