3418; Kununua matatizo.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wanaweza kukuuzia kitu chochote kile, kama tu utaonyesha uhitaji mkubwa ulionao.
Unaweza hata kuuziwa matatizo na ukayanunua, kama tu utaonyesha huo ndiyo uhitaji mkubwa ulionao.
Matapeli ni moja wa makundi ya watu wanaotumia vizuri sana mbinu za ukamilishaji wa mauzo wakati wa kufanya mambo yao.
Watu wameuziwa sabuni wakiambiwa ni siku, mawe wakiambiwa ni madini na makaratasi wakiambiwa ni fedha.
Yote hayo ni kwa sababu ya tamaa ambayo watu wanakuwa nayo.
Moja ya eneo ambalo watu wamelaghaiwa sana ni kwenye siri za mafanikio.
Watu ambao hawajafanikiwa, ila wana matamanio makubwa ya kufanikiwa, huwa wanaamini ipo siri ya mafanikio ambayo hawajaijuia.
Wanakuwa wanatamani sana kuipata siri hiyo ili nao waweze kufanikiwa.
Na hilo limekuwa linafungua firsa kwa wenye nia ya kuwatapeli wengine, kuja na kitu wanachoita siri za mafanikio na kuuza kwa wengine.
Wale wenye kutaka sana kufanikiwa bila ya kuweka kazi, huwa wananasa kirahisi kwenye hayo mauzo ya siri za mafanikio.
Ni baada ya kuhangaika na kununua siri za mafanikio ndiyo mtu hufunguka na kugundua hakuna siri za mafanikio, tena ambazo zinastahili kununuliwa kwa gharama kubwa ambayo watu wanalima.
Kama kweli ingekuwepo siri ya mafanikio, isingekuwa siri tena, kwani kila mtu angeijua na kuitumia.
Au kama ingekuwa ni siri ngumu sana kwa wengi kutumia, gharama yake ingekuwa kubwa sana kiasi kwamba wengi ambao bado hawajafanikiwa hawawezi kumudu.
Tatizo kubwa sana ni hisia za mtu zikishakuwa juu, uwezo wa kufikiri hushuka.
Mtu ambaye ameshawaka tamaa ya kupata kitu fulani, hawezi kabisa kutuliza tamaa hiyo na kufanya maamuzi sahihi.
Hivyo njia nyingine ya kujizuia kununua matatizo ni kusubiri kabla ya kufanya maamuzi ya kununua.
Hata kama umekielewa kitu na kuwa tayari kukinunua, jipe kwanza muda kati ya maamuzi hayo na utekelezaji.
Kwenye huo muda kama msukumo wa kununua ni wa tamaa, utaweza kupoa na ukafikiri kwa usahihi.
Kuwa makini na kila maamuzi ya manunuzi unayofanya, tamaa zako zimekuwa zinapelekea uuziwe matatizo ambayo yanaishia kukusumbua zaidi.
Dhibiti hisia zako ili ufanye maamuzi sahihi kwako.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe