Rafiki yangu mpendwa,
Kikwazo cha mtu kupata utajiri mkubwa kwenye maisha yake huwa ni utajiri kidogo anaoupata.
Kwani wengi wanapoanzia chini huwa wanakuwa na shauku ya kupiga hatua, hivyo wanashambulia sana.
Lakini wakianza kupiga hatua, wanaacha kushambulia na kuanza kulinda. Hapo ndipo wanajizuia kukua na hatimaye kuanguka.
Kama unataka kupata utajiri mkubwa kwenye maisha yako na ambao utakuweka huru, haitoshi tu kujua jinsi ya kujenga utajiri, bali pia kuukuza zaidi.

Kwenye kitabu cha THE RULES OF MONEY, mwandishi Richard Templar anatushirikisha sheria za kuzingatia ili tuweze kukuza zaidi utajiri tunaokuwa tumeanza kuujenga.
SEHEMU YA III; KUZA UTAJIRI.
Ukishaanza kupata pesa kidogo, mchezo wa kujenga utajiri unakuwa rahisi. Hiyo ni kwa sababu fedha huwa inavutia fedha zaidi.
Milioni ya kwanza huwa ndiyo ngumu zaidi kupata, baada ya hapo zinazofuata ni rahisi. Kadhalika bilioni ya kwanza.
Ukianza kujenga utajiri, hupaswi kubweteka, badala yake unapaswa kuongeza kasi kubwa zaidi ili kukuza utajiri huo.
Pia unapaswa kutafuta na kutumia fursa mbalimbali kukuza utajiri wako.
Hapa kuna sheria za kuzingatia ili kukuza utajiri.
Sheria ya 70; Jifanyie tathmini ya kifedha mara kwa mara.
Jifanyie tathmini yako ya kifedha angalau mara moja kila wiki. Tenga siku ya wiki ambayo utapitia hali yako ya kifedha. Kuanzia kwenye kipato, matumizi, akiba na uwekezaji. Unapofuatilia fedha zako kwa karibu, unaona mengi ambayo yanasaidia utajiri kukua.
Sheria ya 71; Kuwa na mamenta wa kifedha.
Tumia ujuzi na uzoefu wa wengine kwenye kufanya maamuzi bora kifedha. Unapaswa kuwa na mamenta upande wa fedha. Sifa za menta sahihi ni ambaye ameweza kujenga utajiri kwa njia sahihi na siyo kushinda bahati nasibu au kupata urithi. Pia asiwe ananufaika kwa kamisheni kwenye ushauri anaokupa.
Sheria ya 72; Sikiliza machale yako.
Kwa kila maamuzi unayofanya, huwa kuna sauti ya ndani ambayo huwa inakutahadharisha. Mara zote unapopuuza sauti hiyo, unaishia kufanya makosa yanayokugharimu. Isikilize sauti hiyo mara zote.
Sheria ya 73; Usibweteke.
Huwa kuna matamanio ya kupunguza juhudi na kupumzika pale mtu unapoanza kupata utajiri. Lakini huo ndiyo wakati hatari sana mtu kulegeza, unapaswa uendelee kukaza zaidi. Huo ndiyo wakati wa kuongeza kasi zaidi, kushambulia zaidi, kuweka kazi kubwa sana. Pale mambo yanapokwenda vizuri, ongeza kazi ili upate manufaa makubwa zaidi.
Sheria ya 74; Pata mtu wa kufanya usiyoweza kufanya.
Fanya yale ambayo uko vizuri kuyafanya na tafuta watu wengine wazuri wafanye yale ambayo haupo vizuri kuyafanya. Chagua watu wanaoweza kufanya kwa ubora na waache wafanye kazi yao kukujengea wewe utajiri. Unapopata watu sahihi, wajali na watunze vizuri ili waendelee kufanya kazi na wewe.
Sheria ya 75; Jijue ufanyaji kazi wako; binafsi, ubia au timu.
Unapaswa kujitambua wewe mwenyewe unafanya kazi bora katika hali gani. Kama ni ukiwa peke yako, ukiwa na mbia au ukiwa ndani ya timu. Watu wanatofautiana, jua unafanya vizuri kwenye hali gani na jitengenezee mazingira ya aina hiyo. Kama ni binafsi, endesha biashara yako mwenyewe, kama ni ubia kuwa na mbia ambaye mnashabihiana na kama ni timu, jenga timu kubwa.
Sheria ya 76; Angalia fursa zilizojificha.
Kila mahali huwa kuna fursa ambazo zimejificha na kuonekana kwa wale tu ambao wanazitafuta. Wale wanaoridhika haraka huwa hawazioni fursa hizo. Kila mara hoji na dadisi kile unachofanya ili uweze kuona fursa zilizojificha.
SOMA; Sheria Za Fedha; Sheria Za Kujenga Utajiri – Sehemu Ya Pili.
Sheria ya 77; Usijaribu kupata utajiri haraka.
Unapaswa kujenga msingi imara wa hekalu lako la utajiri la sivyo litaangushwa haraka. Utajiri unaopatikana haraka huwa ni dhaifu na unapotea haraka. Utajiri unaojengwa kwa muda mrefu huwa ni imara na unadumu. Jenga utajiri wako kwa muda mrefu.
Sheria ya 78; Mara zote jiulize; Wananufaikaje?
Watu wanapokuja kwako na kukuambia watakusaidia kupata utajiri, jiulize wao wananufaikaje kwenye hilo? Kila mtu huwa ana ajenda binafsi kwenye kile anachofanya, hivyo usipojua ajenda za watu, utaishia kuumizwa. Mara zote kuwa na wasiwasi na kitu chochote kinachogusa utajiri wako. Epuka yeyote anayekuambia ana njia ya haraka ya kupeta utajiri mkubwa, anataka kukuibia.
Sheria ya 79; Ifanye fedha ikufanyie kazi.
Usiache fedha yako ikakaa mahali popote bila ya kuzunguka na kukuingizia faida. Kila fedha unayokuwa nayo, hakikisha inakufanyia kazi na kukuingizia faida, hata kama ni kidogo. Fedha inayokaa tu inapoteza thamani yake.
Sheria ya 80; Jua wakati wa kuachana na uwekezaji.
Unapaswa kuwa na vigezo vya kuchagua uwekezaji ambao unafanya na pale vigezo hivyo vinapokuwa havipo tena, unakuwa tayari kuachana na uwekezaji. Kigezo kinaweza kuwa kasi ya ukuaji, mfano inachukua muda gani kwa uwekezaji kukua mara mbili. Kwa kutumia kanuni ya 72 na riba inayopatikana, unaweza kujua. Chukua 72 gawa kwa riba ya mwaka na jibu utakalopata ni muda ambao itachukua kwa uwekezaji unaofanya kukua mara mbili.
Sheria ya 81; Jua mtindo wako wa uwekezaji.
Kuna ambao wanapenda ushindani, hawa huingia kwenye kitu mapema na hivyo kuwa mbele ya wengine, lakini wana hatari ya kuingia kwenye vitu ambavyo siyo sahihi. Na kuna ambao wanapenda uhakika, hivyo huwa waangalifu na kuchelewa kuingia kwenye uwekezaji, hawa wana hatari ya kuchelewa kipindi kizuri cha kunufaika na uwekezaji. Jua mtindo wako kisha ufanyie kazi kwa manufaa.
Sheria ya 82; Jua jinsi ya kusoma hesabu za mizania (Balance Sheet).
Kama unafanya uwekezaji au biashara kubwa, hesabu za mizania ni picha nzuri sana ya thamani na uhai wa biashara. Hesabu hizo zinalinganisha mali na madeni kwenye biashara. Upande mmoja una madeni na mtaji wakati upande mwingine una mali. Pande hizo mbili lazima zilingane kama biashara ipo sawa. Kanuni ni; MTAJI + MADENI = MALI. Jua jinsi ya kusoma hesabu hizo na zisome kabla ya kufanya maamuzi juu ya uwekezaji au biashara.
Sheria ya 83; Kuwa mbele ya wakusanya kodi.
Kwenye safari yako ya kujenga na kukuza utajiri, kamwe usijaribu kukwepa kodi. Hilo ni kosa kisheria na litakugharimu sana. Badala yake tumia sheria na fursa zilizopo kupunguza kodi unayopaswa kulipa. Kwa mfano kwa kupunguza matumizi, hasa ya manunuzi ya vitu binafsi, inapunguza sana kodi ambazo mtu analipa. Pia kuna aina za uwekezaji ambazo zinatozwa kodi kidogo, zijue na wekeza huko.
Sheria ya 84; Fanya mali zako zikufanyie kazi.
Kila mali uliyonayo inapaswa kukuingizia manufaa ya aina mbili; kipato cha moja kwa moja na ukuaji wa thamani. Kwa mali zote ulizonazo, angalia jinsi ya kuzitumia kuzalisha kipato na kukua thamani. Usiache mali yoyote ikakaa tu, ni kujikosesha utajiri.
Sheria ya 85; Kamwe usiamini thamani yako ni sawa na unacholipwa.
Kama umeajiriwa au kujiajiri, kiasi chochote unacholipwa, siyo thamani yako. Thamani yako ni zaidi ya hapo na ili uweze kulipwa zaidi, lazima utoe thamani kubwa zaidi. Kataa kujilinganisha na kile unacholipwa, pata hasira ya kutoa thamani kukwa zaidi ili uweze kulipwa zaidi.
Sheria ya 86; Usifuate njia wanayofuata wengine.
Kufuata mkumbo ni sumu kubwa sana kwenye kupata na kukuza utajiri. Ukifuata njia ya wengine, utaishia kule wanakoishia, ambapo siyo pakubwa. Mara zote kuwa tayari kusimama peke yako kama unataka kujenga na kukuza utajiri wako.
Hizo ndiyo sheria za kuweza kukuza zaidi utajiri wako baada ya kuweza kuutengeneza. Zingatia sheria hizo ili uweze kufika hatua za juu zaidi badala ya kubweteka na hatua chache unazokuwa umeanza kupiga.
Masomo yote ya kitabu cha THE RULES OF MONEY kilichoandikwa na Richard Templar, ambayo yana sheria zote za fedha za kujenga na kutunza utajiri, yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.
Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala mzuri juu ya sheria hizi za kufikiri kitajiri. Fungua na ujifunze ili uweze kufikiri kwa usahihi hasa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.