Rafiki yangu mpendwa,
Unapokuwa unaanzia chini kabisa, yaani kwenye umasikini, kujenga utajiri unaiona ni kazi kubwa sana.
Unaweza kupambana kweli kuhakikisha unajenga utajiri. Na kwa ujuzi na juhudi sahihi, unafanikiwa kupata utajiri.
Hapo sasa ndiyo unakuja kugundua kutunza utajiri ni kazi kubwa kuliko hata kuujenga. Hiyo ni kwa sababu ukishakuwa tajiri, unakuwa unawindwa na watu wengi, wote wakitaka kunufaika na utajiri huo.
Ili uweze kudumu na utajiri unaoujenga kwa muda mrefu, lazima uwe na njia sahihi za kutunza utajiri huo.

Kwenye kitabu cha THE RULES OF MONEY, mwandishi Richard Templar ameshirikisha sheria muhimu za kuzingatia ili kuweza kutunza utajiri ambao mtu umejenga. Na pia ameshirikisha sheria za kutawanya utajiri wako ili uweze kuwanufaisha wengine.
Karibu kwenye somo hili uzijue sheria hizo na kuzizingatia na uweze kufanikiwa.
SEHEMU YA IV; KUTUNZA UTAJIRI
Baada ya kupata utajiri, hupaswi kuupoteza. Hapa unakwenda kujifunza jinsi ya kutunza utajiri.
Unapaswa kujua jinsi ya kutunza, kulinda, kufurahia na kuboresha utajiri wako.
Sheria ya 87; Nunua ubora.
Ni bora ununue vitu vichache ambavyo ni bora kwa bei ya juu, kuliko kununua vingi visivyo bora kwa bei ya chini. Kuokoa bei kwa kununua vitu visivyo na ubora huwa kuna gharama kubwa zaidi.
Sheria ya 88; Soma maandishi madogo.
Kwenye kila kitu unachonunua au makubaliano unayoingia, soma maandishi yaliyoandikwa kwa herufi ndogo. Hayo ndiyo huwa yanakuwa na tahadhari kubwa unayopaswa kujua kabla ya kufanya maamuzi. Jua vigezo na masharti ya kila kitu kabla ya kufanya maamuzi.
Sheria ya 89; Usitumie kabla ya kupata.
Usitumie fedha ambayo bado hujaipata, hata kama una uhitaji kiasi gani. Kukopa kwa ajili ya matumizi inakugharimu sana kwa sababu unakuja kulipa kwa riba, wakati matumizi uliyofanya huenda siyo ya kuzalisha.
Sheria ya 90; Weka pembeni kwa ajili ya uzee.
Kadiri muda unavyokwenda, nguvu za kufanya kazi zinapungua, lakini gharama za maisha zinapanda. Hivyo unapaswa kufanya maandalizi ya uzee wako mapema kwa kuweka akiba na kufanya uwekezaji ambao uzeeni utakulipa pesa ya kuendesha maisha bila kulazimika kufanya kazi.
Sheria ya 91; Kuwa na akiba ya dharura.
Unapaswa kuwa na akiba ya dharura, ambayo inakuwezesha kuendesha maisha yako kwa angalau miezi sita hata kama huna kipato kabisa. Hilo litakuwezesha kuvuka changamoto mbalimbali unazokutana nazo. Pia kuwa na bima kwenye maeneo muhimu ya maisha kama mali na afya.
Sheria ya 92; Jinsi ya kupata bei nzuri wakati wa kununua.
Japo unanunua kwa kuangalia ubora, haimaanishi ulipe bei kubwa kuliko inavyostahili. Hivyo unapopanga kununua kitu, hakikisha unapata bei sehemu tatu tofauti kisha kulinganisha na kufanya maamuzi ambapo bei siyo kubwa na ubora ni wa juu.
Sheria ya 93; Usikope fedha kwa ndugu au marafiki, ila unaweza kuwaruhusu kuwekeza.
Usikope fedha kwa watu wa karibu, ambao una mahusiano nao. Kwani mwisho wake huwa ni kuharibika kwa mahusiano hayo pale unaposhindwa kulipa fedha. Kama unafanya kitu ambacho kinahitaji fedha ambazo huna, badala ya kuwakopa watu wa karibu, wape fursa ya kuwekeza, wakijua kuna hatari ya kupoteza. Kwa njia hiyo hawatakulaumu sana kama watapata hasara.
Sheria ya 94; Usigawe hisa za biashara yako.
Kuwapa wengine sehemu ya umiliki wa biashara yako, kupitia kuwapa hisa ni kupunguza umiliki na nguvu yako. Ni bora kuchukua mkopo utakaoulipa kwa riba kuliko kuleta wawekezaji utakaowapa umiliki. Na kama unalazimika kuwapa watu umiliki, basi hakikisha unapata zaidi ya fedha, pata uzoefu ambao huna na msaada kwenye uendeshaji wa biashara.
Sheria ya 95; Jua wakati wa kuacha.
Kila jambo huwa lina mwisho wake, ni lazima ujue upi utakuwa mwisho kwako kwenye safari yako ya kujenga utajiri. Mwisho siyo kuacha kabisa kufanya, bali kupunguza ule umakini ambao unaweka kwenye kujenga utajiri na kuwa na maisha mengine. Lakini pia kama unafanya unachopenda na unataka kuendelea nacho, huna haja ya kuacha.
Zingatia sheria hizi ili kulinda utajiri wako usipotee hovyo.
SOMA; Sheria Za Fedha; Sheria Za Kukuza Utajiri.
SEHEMU YA V; KUGAWA UTAJIRI
Baada ya kuweka juhudi kubwa kujenga na kutunza utajiri, hatua muhimu inayofuata ni kugawa utajiri huo kwa wengine.
Hapa siyo kwamba unagawa utajiri wako kwa wavivu ambao hawapo tayari kuweka juhudi kujenga utajiri, bali unawasaidia wale ambao wanapitia hali au mazingira magumu yanayowafanya washindwe kujenga utajiri.
Kwa kufanya hivyo utajiri wako unakuwa na manufaa kwa watu wengine.
Sheria ya 96; Tumia utajiri wako kwa hekima.
Huwa kuna tamaa ya kutumia hovyo fedha baada ya mtu kuteseka kuzipata. Lakini kwa njia hiyo utajiri hupotea haraka. Unapaswa kutumia utajiri wako kwa hekima ili uweze kuwa na manufaa kwa wengine. Matumizi bora ya utajiri ni kuwafundisha watoto jinsi ya kutengeneza kipato, kuweka akiba, kuwekeza na kuwa na matumizi mazuri.
Sheria ya 97; Usiwakopeshe fedha ndugu na marafiki, labda kama upo tayari kupoteza.
Unaweza kuwashirikisha watu wako wa karibu utajiri wako, ila siyo kwa kuwakopesha ukitegemea kulipwa. Wakopeshe kama upo tayari kupoteza, maana ukweli ni hutalipwa. Kukopesha watu wa karibu huwa inaharibu mahusiano kwa sababu watu wanaposhindwa kukulipa wanakukwepa na wewe unakasirika. Kuepusha hilo, usikopeshe watu wa karibu, pale wanapokuja kwako kwa ajili ya kukopa, angalia kile unachoweza kuwasaidia na wasaidie hicho.
Sheria ya 98; Usikopeshe, bali pata umiliki kwa kuwekeza.
Pale watu wanapokuja kwako wakitaka uwakopeshe fedha kwa ajili ya biashara au mradi wowote, usiwakopeshe, badala yake watake wakupe umiliki kwenye kitu hicho. Kwa njia hiyo, kama wakishindwa unakuwa huwadai na kama wakifanikiwa unanufaika. Hiyo inakuwa nafuu kuliko kukopesha ambapo utapoteza tu. Kama anayetaka umkopeshe atakataa wazo la kuwekeza, hawezi kuwa sahihi hata kwa kukopesha.
Sheria ya 99; Hutaondoka na utajiri wako.
Utakapokufa, utaondoka bila kitu chochote, utaacha utajiri wako wote hapa duniani. Hivyo unapaswa kuutawanya vizuri utajiri wako kabla hujafa, kwani ukiuacha bila ya maelekezo mazuri, utaleta mafarakano makubwa. Unapaswa kuandika wosia wa jinsi utajiri wako utakavyogawanywa baada ya kufa kwako.
Sheria ya 100; Jua wakati na jinsi ya kusema HAPANA na NDIYO.
Ukishakuwa tajiri, kila mtu anatafuta njia ya kujinufaisha na utajiri wako kupitia kuomba, kukopa, kuiba, kulaghai n.k. Unapaswa kuwa makini ili kuepuka yote hayo. Anza kwa kusema HAPANA kwa wote wanaotaka kukukopa, hivyo watu wajue wazi kwamba hukopeshi. Kwa wale wanaokuja na miradi yao na kutaka uwasaidie fedha, waambie waandike maombi yao kisha utayapitia pamoja na washauri wako na kama wataona ni sahihi basi utawekeza. Hilo litawapunguza wengi ambao hawapo makini. Na kwa wale wanaoweza kuandika vizuri mpango wao na ukawa na ushawishi, unaweza kuwekeza. Wengine wote sema HAPANA. Na usiwape watu matumaini kama huna mpango wa kukubaliana nao, waambie HAPANA mapema ili waendelee na mipango yao mingine. Usiwe na hatia kwenye kusema HAPANA, pesa ni zako, umezitafuta kwa jasho lako na unaweza kuzitumia vile unavyotaka wewe.
Sheria ya 101; Tafuta njia za kuwapa watu fedha bila kujiona wana deni.
Changamoto ya kuwa tajiri ni mahusiano yako na wengine yanaathirika sana. Hata unapotaka kumsaidia mtu, anaweza kujiona ana deni kwako hivyo hamuwezi kuwa sawa. Kuondoa hali hiyo, waeleze watu wazi kwamba unawapa fedha ili waweze kujijenga na kutoka pale walipokwama na siyo kwa ajili ya wao kukurudishia. Hilo hupunguza ile hali ya watu kujiona wana deni.
Sheria ya 102; Usiwalinde sana watoto wako kupitia uzoefu wa umasikini ambao ni wa thamani.
Kwa kuwa una utajiri haimaanishi watoto wako hawapaswi kupata shida kabisa. Kufanya hivyo siyo kuwasaidia, bali kuwaharibu. Wafundishe watoto misingi ya fedha na pale wanapofanya makosa, acha waadhibiwe na makosa hayo ili wajifunze kuliko kuwasaidia. Njia nzuri ni kuwaambia wakupe bajeti yao, ambayo lazima waitete, kisha wewe unawapa fedha kuendana na bajeti hiyo. Unawataka waweke akiba na kuwekeza kwenye hiyo fedha. Kama watamaliza fedha kabla ya muda, usiwape fedha, mpaka muda uishe. Kama bajeti ni ya mwezi na wao wamemaliza fedha kabla mwezi haujaisha, usiwape tena fedha nyingine mpaka mwezi uishe, mateso watakayopitia yatawapa funzo la kuwa na nidhamu ya fedha. Lakini kama utakuwa unawapa fedha pale wanapoenda nje ya bajeti, watakuwa wanafanya hivyo kila wakati. Kama una mpango wa kuwapa watoto wako fedha nyingi, usifanye hivyo mapema, bali waache kwanza waweze kutengeneza fedha zao wenyewe ndiyo uje kuwapa. Kwa njia hiyo zitawasaidia badala ya kuwapoteza.
Sheria ya 103; Jua jinsi ya kuchagua mfuko wa kutoa misaada.
Unapokuwa tajiri, utashawishiwa kutoa misaada kwenye maeneo mengi. Wewe chagua yale maeneo ambayo unajali zaidi, chagua mifuko ambayo inasaidia eneo hilo, pitia taarifa za kila mfuko kisha chagua ule ambao umevutiwa nao zaidi.
Sheria ya 104; Tumia pesa zako mwenyewe kwa sababu hakuna atakayezitumia kwa hekima kuliko wewe.
Watu huwa ni rahisi sana kutumia pesa ambazo hawajazitafuta kwa jasho. Hivyo haijalishi una utajiri kiasi gani, hakikisha wewe ndiye unayeidhinisha matumizi yote ya fedha zako. Hilo litaleta nidhamu kwenye matumizi. Ukiwapa watu wengine ruhusa ya kuidhinisha matumizi, watafanya matumizi ambayo hayana tija.
Sheria ya 105; Wajibika kabla ya kuchukua ushauri.
Watu wengi hudhani kupata ushauri ndiyo kutawasaidia kupata matokeo wanayoyataka. Lakini ukweli ni kupata matokeo lazima mtu uwajibike wewe mwenyewe. Hivyo wajibika ili ushauri unaochukua ukusaidie.
Sheria ya 106; Ukishatajirika, usitake kujionyesha.
Hakuna kitu cha kijinga ambacho watu huwa wanafanya kama kujionyesha kwamba wana utajiri pale wanapotajirika. Kwa njia hiyo wanawakaribisha wale wanaotaka kujinufaisha kupitia utajiri wao. Kama unataka kufurahia utajiri wako na kuepuka kusumbuliwa, endelea kuwa na maisha yako ya kawaida hata baada ya kutajirika.
Sheria ya 107; Kifuatacho?
Kuna njia nyingi za kupata utajiri ambazo zimekuwa zinafundishwa. Kujiambia kauli chanya, kubeba vitu vinavyoashiria utajiri na imani za aina nyingine. Kila kitu huwa kinafanya kazi kama kikifanyiwa kazi. Hivyo kama umeipata njia sahihi na inayofanya kazi kwako, itumie. Weka juhudi hasa na jenga utajiri wa uhakika.
Hizo ndizo sheria za kugawa utajiri wako kwa watu wako wa karibu bila ya kuathiri mahusiano yako na wao. Zingatia sheria hizi ili utajiri wako uweze kuwa na manufaa kwa watu wengine.
Masomo yote ya kitabu cha THE RULES OF MONEY kilichoandikwa na Richard Templar, ambayo yana sheria zote za fedha za kujenga na kutunza utajiri, yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.
Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala mzuri juu ya sheria hizi za kufikiri kitajiri. Fungua na ujifunze ili uweze kufikiri kwa usahihi hasa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.