Rafiki yangu mpendwa,
Tunaendelea kukumbushana kwamba kinachotutofautisha sisi binadamu na viumbe wengine ni uwezo wetu wa kufikiri na kufanya maamuzi.
Kila kiungo ambacho tunacho, kinapatikana kwa wanyama wengine kama mbuzi na kondoo. Tuna macho na wao wana macho, tuna ubongo na wao wana ubongo.
Tofauti pekee ni sisi binadamu tunaweza kufikiri na kufanya maamuzi, wakati wanyama wengine huwa wanafanya mambo kwa mazoea na kufuata mkumbo.

Kwa mfano kukiwa na kundi la mbuzi ambao wanapita eneo fulani na ukafunga kamba pale wanapopita, mbuzi walio mbele wakizuiwa na kamba wataruka. Mbuzi wanaofuata nao wataruka kwa sababu wameona wenzao wanaruka. Hata kama utaondoa kamba hiyo, mbuzi wanaofuata bado wataruka. Siyo kwa sababu kuna kamba, bali kwa sababu wameona waliowatangulia wameruka.
Hivyo ndivyo maisha ya wengi yanavyokuwa na matatizo makubwa, kwa sababu ya kuiga yale ambayo wengine wanayafanya, bila ya kufikiri na kufanya maamuzi.
Unaona wengine wameanzisha biashara ya aina fulani na inawalipa na wewe unakimbilia kuanzisha biashara kama hiyo kwa kudhani itakulipa pia. Unashindwa kufikiria kwanza kama ni biashara inayoendana na wewe, kwa uwezo, vipaji na haiba yako.
Falsafa ya Ustoa inatuonyesha kwamba matatizo mengi tunayokutana nayo kwenye maisha, chanzo chake ni kupuuza fikra zetu. Na tunapopuuza fikra, huwa tunaongozwa na vitu viwili ambavyo vyote ni majanga.
Kitu cha kwanza ni kuiga na kufuata mkumbo. Hapa tunaangalia yale ambayo wengine wanafanya na sisi tunafanya hayo. Tunaishia kwenye matatizo ambayo yanatusumbua sana.
Kitu cha pili ni kuongozwa na hisia tunazokuwa nazo. Pale hisia zinapokuwa huu, fikra huwa zinakuwa chini na hivyo maamuzi tunayoyafanya hayawezi kuwa bora.
Mstoa Marcus Aurelius kwenye kitabu cha kumi cha MEDITATIONS ametushirikisha jinsi ya kutumia fikra zetu ili kufanya maamuzi sahihi kwetu.
Yapo mengi aliyoshirikisha, lakini ya msingi kabisa unayopaswa kuondoka nayo hapa na kwenda kuyafanyia kazi ni kama ifuatavyo;
1. Kuwa na mchango mzuri kwa wengine.
Wajibu wako kama mwanadamu ni kuwa na mchango mzuri kwa wengine. Kufanya yale ambayo yanafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Unapofanya chochote kinyume na hilo ni kuacha kuwa binadamu na kutengeneza matatizo kwako na kwa wengine.
2. Tenda wema kwa wote.
Watu wanapofanya mambo yanayokukwaza, ni rahisi kuchukia na kuumizwa. Lakini unapaswa kwa nini uwape wengine ruhusa ya kukuumiza. Wengi wanaofanya mambo yanayokukwaza, hawajui hata kama wanafanya hivyo. Unapaswa kuwaonea huruma wale wote wanaokukosea kwa sababu wengi hawajui wanayofanya au madhara yake. Wajibu wako ni kutenda wema kwa watu wote na utapunguza matatizo mengi unayoingia.
SOMA; Falsafa Ya Ustoa; Dhambi Ni Kwenda Kinyume Na Asili.
3. Kila kitu kinapita.
Huwa tunajihangaisha na vitu tukidhani ni muhimu, lakini tunakuja kuvipoteza. Kila kitu hapa duniani kinapita, ikiwepo sisi wenyewe. Kwa hiyo tusikubali kukipa kitu chochote umuhimu ambao hakistahili kuwa nacho. Tusiruhusu kitu chochote kutuvuruga, kwa sababu hakuna kinachodumu. Hata matatizo makubwa unayoona unayo, hayatadumu milele, hivyo usiyape nafasi ya kukusumbua.
4. Wanajiumiza wenyewe.
Pale watu wanapofanya mambo ya kuwaumiza wengine, huwa wanajiumiza wao wenyewe zaidi kuliko wanavyowaumiza wengine. Hivyo usikubali kuumizwa na chochote ambacho kinafanywa na wengine, kwa sababu tayari wanajiadhibu wao wenyewe kwa hicho wanachofanya.
5. Usiombe kuondolewa matatizo, omba uimara wa kuyakabili.
Unapomwomba Mungu kwenye maisha yako, usimwombe akuondolee matatizo unayokutana nayo, bali mwombe akupe uimara wa kuweza kukabiliana na kila aina ya matatizo unayoweza kukutana nayo. Kwa kuwa imara, hakuna chochote kitakachoweza kukuyumbisha.
Ukitumia fikra zako vizuri, mambo mengi yanayokusumbua sasa yatakosa nguvu kabisa kwako na utaondokana na matatizo na mateso mengi unayokabiliana nayo.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumejifunza mambo mengi zaidi ya kuzingatia kutoka kwenye falsafa ya Ustoa ili kutumia fikra zetu vizuri na kuishi maisha bora. Karibu usikilize kipindi hapo chini, ujifunze na kuweka kwenye maisha ili yawe bora.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.