Rafiki yangu mpendwa,

Utajiri ni kitu kizuri sana kwenye maisha, kwa sababu unakupa uhuru wa kuishi aina ya maisha ambayo mtu unayataka.

Uzuri wa utajiri hauishii kwako wewe unayeupata, bali pia unakuwa na manufaa kwa watu wengine. Njia unazokuwa umetumia kupata utajiri zinakuwa na manufaa kwa wengine, kupitia thamani unayokuwa umewapa na hata ajira unazotengeneza.

Pamoja na manufaa hayo makubwa ya utajiri, bado wengi hawapendi kusikia kuhusu utajiri na kuona ni kitu kibaya. Hiyo ni kwa sababu ya mtazamo mbaya ambao wengi wanao kuhusu utajiri.

Watu wengi hawajawa matajiri siyo kwa sababu hawawezi, bali kwa sababu hawajui. Na ambacho hawajui vizuri ni njia za uhakika za kuwafikisha kwenye utajiri.

Wengi wamekuwa wanahangaika na njia ambazo haziwezi kuwapa utajiri kwa uhakika. Chukua michezo ya kubahatisha, watu wengi huwa wanaicheza kwa matamanio ya kupata utajiri mkubwa. Lakini wanaoshinda ni wachache sana na hata hao hawapati utajiri.

Bilionea na Mwandishi Ken Fisher aliona changamoto hiyo ya watu kutokujua njia sahihi za kujenga utajiri na hivyo akashirikisha uzoefu wake kupitia miaka ambayo amekuwa kwenye uwekezaji na kufanya kazi na matajiri wengi.

Kupitia uzoefu wake na utafiti mpana aliofanya kwa matajiri, aliweza kuona zipo njia kumi tu za kujenga utajiri. Njia hizo ndizo zimetumiwa na matajiri wengi na yeyote anayeweza kuzitumia vizuri, lazima na yeye atakuwa tajiri.

Kwenye kitabu chake kinachoitwa THE THE ROADS TO RICHES, Ken Fisher ametushirikisha njia hizo na hatua za kuchukua kwenye kila njia ili kuweza kujenga utajiri.

Njia hizo 10 za kujenga utajiri ni kama ifuatavyo;

1. Kuanzisha biashara yenye mafanikio – njia bora zaidi.

2. Kuwa CEO wa kampuni kubwa – inataka kazi sana.

3. Kuwa msaidizi wa mwenye maono makubwa – kutoa thamani kubwa.

4. Kugeuza umaarufu kuwa utajiri – au utajiri kuwa umaarufu.

5. Kuoa au kuolewa na mwenye utajiri – njia inayotaka umakini mkubwa.

6. Kuiba bila kuvunja sheria – kesi za madai.

7. Kutumia pesa za wengine – inazalisha utajiri mkubwa.

8. Kugundua njia mpya za kipato – hata kama siyo mgunduzi.

9. Kutumia vizuri ardhi – kuongeza thamani.

10. Kuweka akiba na kuwekeza kwa muda mrefu – njia ya wengi.

Mwandishi anasema katika njia hizo, kuna ambazo utakubaliana nazo na kuna ambazo hutakubaliana nazo. Lakini zote ni njia ambazo watu wengi wamezitumia kujenga utajiri.

Wajibu wako ni kuchagua njia ipi inakufaa wewe kisha kuitumia hiyo kwa usahihi kujenga utajiri. Unaweza kutumia njia moja kwa maisha yako yote, au ukaanza na njia moja kisha nyingine au ukatumia njia zaidi ya moja kwa wakati mmoja. Yote ni juu yako na utayari wako wa kuweka kazi kubwa.’

Mwandishi pia anasema kuna njia zaidi ya hizo 10 ambazo watu wanatumia kujenga utajiri. Lakini njia hizo nyingine siyo za uhakika, ndiyo kuna ambao wanaweza kuwa wametajirika nazo, lakini ni kwa bahati tu. Mfano kushinda bahati na siku au kurithi utajiri. Njia 10 alizoshirikisha ni ambazo mtu yeyote, kwa kuweka juhudi anaweza kuzitumia na yeye akajenga utajiri.

Kwenye mfululizo wa masomo kutoka kwenye kitabu hiki tutajifunza njia hizo 10 na jinsi ya kuzitumia kujenga utajiri. Masomo yote ya kitabu cha THE TENO ROADS TO RICHES yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.

NJIA YA 1; KUJENGA BIASHARA – NJIA TAJIRI ZAIDI.

Kama una maono makubwa, ujuzi wa uongozi na mwenza mwelewa, unaweza kutumia njia hii kujenga utajiri mkubwa.

Kuanzisha na kumiliki biashara yako mwenyewe ndiyo njia tajiri kuliko zote. Matajiri wengi wamejenga utajiri wao kupitia kuanzisha na kumiliki biashara zenye mafanikio.

Njia hii haina ubaguzi wa aina yoyote ile, mtu yeyote anaweza kutumia njia hii na kujenga utajiri.

Lakini pia siyo njia rahisi, kwa sababu ina vikwazo na changamoto nyingi sana. Biashara nyingi zinazoanzishwa huwa zinakufa, ambazo zinasalia huwa zinajiendesha kawaida. Ni biashara chache sana ambazo zinapata mafanikio makubwa.

Mafanikio kwenye biashara yana vitu vingi vyuma yake, mtu anapaswa kuwa na ujasiri mkubwa, nidhamu kali, ngozi ngumu, maono ya kimkakati, watu sahihi na labda bahati.

Ili kujenga biashara yenye mafanikio, kuna maeneo matano ya kuzingatia.

Eneo la kwanza; tasnia.

Ili biashara iweze kufanikiwa, unapaswa kuchagua tasnia ambayo una msukumo wa kuleta mabadiliko fulani. Angalia kile ambacho unapenda au uko vizuri na ujenge biashara hapo.

Eneo la pili; bidhaa.

Unapoingia kwenye biashara, kuna njia mbili za kuchagua, kuja na bidhaa ambayo ni mpya sokoni au kuboresha ile ambayo tayari ipo. Kwa urahisi, boresha ile iliyopo ili kuiuza kwa thamani zaidi.

Eneo la tatu; umiliki.

Unapaswa kujua umiliki wa biashara kwa mbeleni utakuwaje, kama unaijenga ili kwenda nayo milele au unaijenga ili kuiuza. Biashara zinazojengwa ili kuuzwa zinakuwa tofauti na zinazojengwa ili kudumu. Wewe jenga biashara utakayodumu nayo.

Eneo la nne; mtaji.

Chanzo cha mtaji wa kuanzisha na kukuza biashara ni kitu unachopaswa kujua tangu awali. Unaweza kuchagua kutumia akiba zako mwenyewe, njia inayohitaji muda mrefu. Au ukachagua kuchukua mitaji ya wawekezaji, njia ya haraka lakini inayopunguza umiliki wako. Njia bora ni ya akiba zako mwenyewe, kwa sababu haiathiri umiliki na hata utajiri wako.

Eneo la tano; hatima.

Hatima ya biashara inaweza kuwa ni kubaki kwenye umiliki binafsi au kwenda kwenye soko la hisa. Chagua kubaki na umiliki binafsi kwa sababu soko la hisa lina changamoto zake nyingi.

Unapoanzisha biashara, mwanzo utakuwa unafanya kila jukumu, lakini kadiri unavyokua unapaswa kujifukuza kazi kwenye majukumu ya chini na kuajiri watu wayafanye. Mwisho unabaki na jukumu la kiongozi wa biashara, ambalo kazi yako ni kuongea na wafanyakazi na wateja kuona biashara inawezaje kuwasaidia kuyafanya maisha yao kuwa bora.

SOMA; Sheria Za Fedha; Sheria Za Kutunza Utajiri.

NJIA YA 2; KUWA CEO (MKURUGENZI MTENDAJI MKUU) WA KAMPUNI KUBWA.

Kama upo tayari kuwajibika, unapenda kuendesha vitu lakini huna maono ya kuanzisha biashara yako mwenyewe, njia hii inakufaa.

Hii ni njia ya kuwa kiongozi wa biashara ambayo hujaianzisha wewe mwenyewe. Kwa njia hii, unaweka kazi kwenye kuikuza sana biashara na wewe kunufaika kupitia ukuaji ambao umesababisha.

Njia hii siyo rahisi, kwa sababu kuwa kiongozi, hasa wa kampuni kubwa ni nafasi ambayo imekaa kisiasa zaidi kuliko kiutendaji.

CEO ndiyo kioo cha kampuni au taasisi. Yote yanayotokea kwenye taasisi yanahusishwa naye. Makosa ya wengine yanakuwa makosa yake. Hivyo CEO anapaswa kuwa mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuendana na watu wa kila aina.

Mafanikio kwenye njia ya kuwa CEO yanahitaji ujuzi wa uongozi na utendaji. Pia inahitaji muda mrefu mpaka mtu kuweza kujijenga na kuaminika kama CEO na kupata nafasi ya kuongoza kampuni au taasisi kubwa.

Njia hii ni ngumu kwa sababu hakuna kitu cha uhakika. CEO unapaswa kuleta ukuaji wa taasisi, lakini kama njia utakazotumia hazitaleta matokeo yanayotarajiwa, inaweza kuharibu nafasi yako kabisa.

Malipo makubwa ya CEO yanapatikana kwa mshahara anaopokea, ambao huwa ni mkubwa na kifurushi cha kutoka, mafao anayoyapata baada ya kazi yake kuisha. Unapotumia njia hii, unapaswa kupatana vizuri kwenye eneo hilo la malipo.

Kwa ujumla, kuwa CEO bora kunahitaji vitu vitatu;

Moja ni kuonekana, hakikisha wale unaowaongoza wanakuona, ni kwa njia hiyo ndiyo unakuwa na ushawishi kwao.

Mbili ni kujali, unapaswa kuwajali sana wafanyakazi na wateja, wajibu wako mkubwa ni kuhakikisha wote wanakuwa kwenye hali nzuri. Kwa kuwajali watu nao wanajali kuhusu kampuni au taasisi unayoongoza.

Tatu ni kuwa mstari wa mbele, kwa kuonyesha kwa mfano yale unayotaka wengine wafanye. Usiwaambie watu wafanye kitu ambacho wewe mwenyewe huwezi kufanya.

HATUA ZA WEWE KUCHUKUA.

Kupitia njia hizi mbili tulizojifunza, hatua za wewe kuchukua ni kutumia njia hizi mbili kwa pamoja kwenye safari yako ya kujenga utajiri. Chagua kuwa mwanzilishi wa biashara yenye mafanikio (njia ya kwanza) na kuwa CEO bora kwenye kuijenga biashara hiyo ifanikiwe (njia ya pili).

Kwa kuwa CEO mwanzilishi wa biashara na ukaweka juhudi kubwa, utaweza kujenga utajiri mkubwa. Kupitia masomo ambayo tumekuwa tunaendelea kuyapata, ukichukua hiyo hatua utaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.

Kwenye somo hili tumeona njia ya kwanza na ya pili ya kujenga utajiri kwa uhakika. Masomo ya njia zote kumi za kujenga utajiri kutoka kitabu THE TEN ROADS TO RICHES yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.

Tumekuwa na mjadala mzuri wa somo hili kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA. Karibu uweze kusikiliza kipindi hicho ujifunze mengine mengi ambayo yapo kwenye kitabu ila hapa hayajapata nafasi. Pia usikie maoni ya wengine juu ya njia hizi za kujenga utajiri.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.