Rafiki yangu mpendwa,

Huwa kuna kauli inasema majuto ni mjukuu.

Hiyo inamaanisha kwamba majuto huwa yanatokea wakati ambapo mtu anakuwa hawezi tena kufanya kile ambacho alikuwa anataka.

Na kwa bahati mbaya sana, hivyo ndivyo wengi wamekuwa wanayapoteza maisha yao. Wakati wanaweza kufanya yale wanayotamani kufanya, wamekuwa hawafanyi. Ni mpaka pale ambapo wanakuwa hawawezi tena kufanya ndiyo wanajutia kwa nini hawakufanya.

Huwezi kukuta kijana ana majuto, kwa sababu anakuwa anajidanganya atafanya, muda bado upo. Lakini haanzi kufanya. Ni mpaka mtu anapofika uzeeni ndiyo anakuwa na majuto, akiona alikosea kutokuanza mapema.

Hilo ni jambo ambalo sitaki likutokee wewe rafiki yangu, sitaki uwe na majuto yoyote kwenye maisha yako. Badala yake nataka uwe na maisha ya kujivunia, hata kama hujapata ulichotaka, lakini unajivunia kwamba ulijaribu.

Watu wengi sana wamekuwa wanakwama kuchukua hatua kwa sababu ya hofu ya kushindwa wanayokuwa nayo. Hofu hiyo inawafanya waone bado hawajajiandaa vya kutosha na hivyo kusubiri. Muda unakwenda na hawaanzi.

Kikubwa kinachowazuia watu kuanza huwa ni uvivu. Hofu ya kushindwa inakuwa ni kitu tu cha kujificha nacho, lakini sababu halisi ni uvivu wa watu kutokuwa tayari kupambana kuweka juhudi zinazohitajika.

Ili uweze kuvuka hofu na uvivu huo, unapaswa kufanya kipaumbele chako cha kwanza kuwa ni kuchukua hatua. Jiweke kwenye hali ya kuchukua hatua mara zote bila ya kukwamishwa na kitu chochote.

Jiambie ni bora uchukue hatua na ushindwe kuliko kuwa mvivu wa kutokuchukua hatua. Kwa sababu ukichukua hatua na ukashindwa, kuna mambo unakuwa umejifunza. Ukiyafanyia kazi hayo uliyojifunza, unapochukua tena hatua unakuwa bora zaidi na hiyo inakupeleka kwenye ushindi zaidi.

Kwa kutokufanya, hakuna chochote unachojifunza, zaidi ya kukuza hofu na kuwa mvivu. Kadiri unavyochelewa kuchukua hatua ndivyo hofu inavyopata nguvu na kukuzuia kuchukua hatua. Kadiri unavyokuwa mvivu wa kuanza ndivyo unavyoshindwa kuanza.

Kuondokana na hizo hofu na uvivu, kuwa mtu wa kufanya mara zote. Unapopatwa na hofu wewe fanya, unaposikia uvivu fanya. Utajifunza mengi kwa kufanya kuliko kutokufanya.

Lakini zaidi, dawa ya hofu huwa ni kufanya kile unachohofia kufanya. Kama unahofia kushindwa, unatakiwa ufanye hicho unachohofia na matokeo yoyote utakayoyapata, yatakuwa yameishinda hofu. Kama utashinda, unakuwa umeishinda hofu. Na kama utashindwa, mambo hayatakuwa mabaya kama ulivyokuwa unadhania na hivyo hofu haipati tena nguvu kwako.

Uzuri ni ukishakuwa mtu wa kufanya, unaendelea kufanya. Hofu haikuzuii na uvivu haukuzoei. Jijenge kuwa mtu wa kufanya na mara zote chukua hatua, itakusogeza karibu zaidi na ushindi mkubwa unaotaka kuupata kwenye maisha yako.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina zaidi dhana hii ya kuwa tayari kushindwa kuliko kuzuiwa na hofu ili uweze kufanya makubwa. Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho hapo chini.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.