3423; Kasi na Subira.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Mambo mengi kwenye mafanikio huwa yanaonekana kama kukinzana hivi.
Na ndiyo maana watu wengi huwa wanaona mafanikio kama yanawavuruga hivi, kwa sababu yanakuwa hayaendi kwa utaratibu wanaokuwa wanautaka wao.

Ili kufanikiwa, unahitajika kushikilia kwenye fikra zako, mawazo mawili yanayokinzana, kwa wakati mmoja.
Mfano mzuri wa mawazo ya aina hiyo ni kasi na subira.
Vipi kama nikikuambia ili ufanikiwe, unahitaji vyote kwa pamoja, kasi na subira?
Hilo linaweza kukuchanganya, vitu viwili vinavyokinzana vinawezaje kwenda pamoja?

Hapo ndipo ufanyaji wa maamuzi sahihi unapohitajika na unavyowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa.

Ili kufanikiwa, unahitaji kasi na subira.

Kasi inahitajika kwenye utekelezaji wa mipango na majukumu ambayo yapo.
Bila ya kuwa na kasi kubwa ya utekelezaji, mambo mengi ambayo ni muhimu hayataweza kufanyika.

Kasi inafanya utekelezaji wa mambo kwenda bila ya kukwama. Kwa sababu kasi huwa inajichochea yenyewe na kuzalisha matokeo makubwa zaidi.

Subira inahitajika kwenye matokeo ya hatua ambazo zimechukuliwa.
Licha ya hatua kuchukuliwa kwa kasi kubwa sana, matokeo huwa hayaji kwa kasi hiyo hiyo.
Matokeo huwa yanachelewa, kwa sababu yanasubiri mkusanyiko wa kutosha wa juhudi zinazowekwa.

Subira inatoa nafasi ya juhudi zilizowekwa kujikusanya na kuweza kuzalisha matokeo ambayo ndiyo yanahitajika. Watu wanapokosa subira kwenye matokeo, huwa wanaacha kufanya na kuwa wamejizuia kabisa kuyapata mafanikio.

Hivyo kasi na subira vinapaswa kwenda pamoja.
Kasi yako kwenye kutekeleza yale uliyopanga iwe kubwa sana. Ni kasi ya utekelezaji ndiyo inawazidi wengi ambao hawana kasi kama hiyo. Wengi wana ghairisha hata kufanya na hivyo kuwa nyuma zaidi.

Subira yako kwenye matokeo inapaswa kuwa kubwa sana. Ni subira ndiyo inakutofautisha na wengi wanaotaka matokeo ya haraka. Wengi wanaacha kufanya pale matokeo yanapokuwa tofauti na walivyotarajia.

Uwezo wako wa kwenda na hayo mawili kwa pamoja na yasikuvuruge wala kukuchanganya ndiyo utakuwezesha kujenga mafanikio makubwa sana, ambayo wengi hawawezi kuyafikia.
Na hiyo haiwi kwa sababu wewe una uwezo mkubwa sana kuliko wengine, bali kwa sababu unakuwa na uelewa mkubwa kuliko wengine.

Elewa yale ya msingi ambayo yanawasumbua wengi au wanayapuuza na utaweza kufanya makubwa ambayo wengi hawayawezi.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe