Rafiki yangu mpendwa,

Ukiwaangalia watu wanaojenga utajiri na wale wanaobaki kwenye umasikini, hawatofautiani sana kwa nje.

Unakuta wengi wanatokea eneo moja, wanafanya kazi au biashara zinazofanana, lakini matokeo yao ni tofauti kabisa.

Hilo limekuwa linawashangaza wengi, kwa kushindwa kuelewa hizo tofauti zinatokana na nini. Na kwa kuwa wengi hawana uelewa, huwa ni rahisi kuamini nguvu za kishirikina.

Lakini ukweli ni kwamba hakuna utajiri mkubwa wa kudumu unaojengwa ka nguvu za kishirikina. Kila unayemwona ameweza kujenga utajiri mkubwa, kuna vitu vya ndani ambavyo anatofautiana na wale walioshindwa.

Mwandishi Chris Hogan kwenye kitabu chake kinachoitwa EVERYDAY MILLIONAIRES ameonyesha jinsi watu wa kawaida kabisa walivyoweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yao na jinsi hata wewe unaweza kufanya hivyo.

Kitabu hicho ni matokeo ya utafiti uliofanywa kwa mamilionea zaidi ya elfu 10 na kuweza kupata taarifa nyingi sana kuwahusu. Utafiti huo uligusa kila eneo la matajiri, kuanzia mitazamo, fikra, shughuli wanazofanya, mahusiano, familia n.k.

Kupitia matokeo ya utafiti huo, Hogan aliweza ameweza kuainisha SIFA KUU SITA ambazo matajiri wanazo ila masikini wamekuwa hawana. Kupitia masomo haya utajifunza sifa hizo na hatua za kuchukua ili na wewe uweze kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

SURA YA 5; ACHA VISINGIZIO NA ANZA KUAMINI.

Swali la kwanza na muhimu kabisa unalopaswa kujiuliza kama unataka kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako ni hili; Je ninaamini nina kile kinachohitajika na ninaweza na kupaswa kuwa tajiri?

Mabadiliko yoyote yale huwa yanaanza na imani kali na isiyoyumbishwa. Kama mtu huamini, bila ya shaka yoyote kwamba unastahili na unaweza kitu, hutakipata.

Jamii imetujenga kwa namna ambayo hatuamini tunaweza kufanya makubwa. Inatulinganisha na wengine na kufanya tupuuze upekee wetu wa ndani. Tunaaminishwa mambo mengi ya uongo kuhusu mafanikio na utajiri.

Lakini pia huwa tunakuwa wepesi kulalamika na kuwasema wengine vibaya, kuliko kuchukua hatua na kubadili hali ya mambo. Tunajisikia vizuri pale tunapowashutumu wengine na kujiona sisi hatuna hatia. Lakini hayo yote huwa hayasaidii.

Hatua ya kwanza ya kujenga utajiri ni kuamini kwamba unaweza kujenga utajiri huo kwenye maisha yako. Kuamini kwamba kwa pale ulipo sasa, na vile ulivyo, tayari umekamilika kwa ajili ya kujenga utajiri. Huna unachopaswa kusubiri na wala hakuna kingine kinachokuzuia isipokuwa wewe mwenyewe.

Hatua za kuchukua.

Amini bila ya shaka yoyote kwamba utajiri unawezekana kabisa kwako na unaweza kujenga utajiri mkubwa kwa kuanzia hapo ulipo sasa. Kisha weka juhudi kubwa kuhakikisha hilo linatokea.

Acha kutoa sababu na visingizio kwa nini hujawa tajiri na anza kuchukua hatua za kujenga utajiri, kwa sababu tayari uwepo upo ndani yako.

SOMA; Vunja Imani Hizi Potofu Sita (6) Kama Unataka Kujenga Utajiri Mkubwa Kwenye Maisha Yako.

SURA YA 6; CHUKUA UWAJIBIKAJI BINAFSI.

Kuna tatizo kubwa sana la uwajibikaji kwenye zama tunazoishi sasa. Ni rahisi sana kwa watu kulaumu na kulalamika badala ya kutatua matatizo yao.

Matajiri wana uwajibikaji binafsi na huo ndiyo unaowawezesha kujenga utajiri mkubwa.

Kujenga utajiri mkubwa ni lazima uwe tayari kuwajibika kupitiliza. Hiyo ina maana kwamba unapaswa kupokea kila kinachotokea kwenye maisha yako kama wajibu wako wewe mwenyewe.

Hata pale wengine wanapokuwa wamefanya mambo ambayo yamekuathiri, bado unachukulia ni wajibu wako wewe. Ni pale unapowajibika kwa viwango vya juu kabisa ndiyo unakuwa tayari kujenga utajiri mkubwa.

Unachopaswa kujua ni kwamba hapo ulipo sasa ni wewe mwenyewe umejifikisha hapo. Na kama unataka kutoka hapo, ni wewe mwenyewe unayeweza kujitoa. Hakuna mwingine anayeweza kufanya hivyo.

Katika kujenga uwajibikaji utakaokupa utajiri, kuna mahusiano ya aina 4 unayopaswa kuyajenga.

1. Kocha; Huyu anakusukuma kufanya zaidi ya vile unavyofanya sasa na hivyo kuweza kufikia makubwa zaidi. Kocha anakuambia ukweli ambao wengi wanaokuzunguka hawapo tayari kukuambia. Kwa kila hatua ambayo umefika, kocha anakutaka kwenda hatua ya juu zaidi.

2. Menta; Huyu ameshafanya kile unachotaka kufanya au kufika kule unakotaka kufika. Anakupa ushauri sahihi wa jinsi unavyoweza kufika kama yeye. Anakueleza mambo ya kuzingatia na ya kuepuka kwenye safari yako. Menta anaweza kuwa wa moja kwa moja au siyo wa moja kwa moja.

3. Mshangiliaji; Huyu anakuamini na kukutia moyo ili uweze kuendelea bila kukata tamaa. Mshangiliaji anakuwa upande wako bila ya kujali unapitia nini na kukuamini kwake kunakufanya uweze kuendelea.

4. Rafiki; Huyu anakukumbusha maisha nje ya safari ya mafanikio. Rafiki anakuwa mtu anayekukubali wewe vile ulivyo bila ya kujali una nini au uko wapi. Rafiki anakufanya usijisahau mwenyewe.

Jenga mahusiano hayo ambayo yatakuwajibisha kwenye safari yako ya kujenga utajiri.

Hatua za kuchukua;

Tambua kwamba maisha yako ni wajibu wako, pale ulipo umejifikisha mwenyewe na kama unataka kwenda mbali zaidi utajipeleka mwenyewe.

Jenga mahusiano sahihi kwa kuwa na watu kwenye maeneo manne uliyojifunza hapa ili uweze kushauriwa vyema na kusukumwa kujenga utajiri mkubwa.

Hapa tumejifunza sifa mbili kati ya sita walizonazo matajiri na zinawatofautisha na masikini. Karibu upate UCHAMBUZI KAMILI wa kitabu hiki cha EVERYDAY MILLIONAIRES kwa kubonyeza MAANDISHI HAYA.

Tumekuwa na mjadala mzuri wa uchambuzi wa kitabu hiki cha EVERYDAY MILLIONAIRE ambapo watu wameshirikisha yale waliyojifunza na hatua wanazochukua. Fungua hapo chini kujifunza zaidi kutoka kwenye kitabu na michango ya wengine.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.