Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.

Lengo kuu la usakaji kwenye biashara ni kuwafikia wateja kule walipo na kupata njia ya kuwashawishi kuja kwenye biashara. Mahali popote penye watu, pana fursa ya kufanya usakaji.

Fursa ya usakaji haiishii tu mahali penye watu, bali inaenda mpaka kwa watu wenye watu. Na hapo ndipo tunaweza kutumia njia ya watu wenye ushawishi kuwafikia wengi na kutengeneza wateja tarajiwa.

Watu wenye ushawishi ni watu ambao wanakubalika na kundi kubwa la watu wenye sifa za aina fulani. Watu hao wanakuwa wamejijengea sifa fulani inayowafanya waaminike na kufuatwa na watu wa aina fulani.

Kwa aina ya wateja ambao unawalenga, kunapokuwa na mtu mwenye ushawishi ambaye anaaminika na watu hao, ni fursa nzuri ya kumtumia yeye kuwafikia watu hao.

Karibu kwenye somo hili ujifunze jinsi ya kutumia watu wenye ushawishi kufikia wateja wengi zaidi.

AINA ZA WATU WENYE USHAWISHI.

Watu wenye ushawishi wanaweza kugawanyika kwenye makundi mawili kulingana na njia kuu wanayotumia kuchangamana na wafuasi wao.

Kundi la kwanza ni watu wenye ushawishi mitandaoni. Hawa ni watu ambao wana wafuasi wengi kwenye mitandao wanayotumia. Watu hao huwa wanaaminika na wafuasi hao wengi wanaowafuata.

Kundi la pili ni wenye ushawishi wa ana kwa ana. Hawa ni ambao wana wafuasi wengi kwenye maeneo wanayoishi au kufanya shughuli zao. Wanakuwa na nguvu na ushawishi mkubwa wa kufanya watu wakubaliane nao.

Unapaswa kutumia watu wenye ushawishi kwa maeneo yote kama wanaendana na biashara yako na kukuwezesha kuwafikia wateja unaowalenga.

MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE KUTUMIA WATU WENYE USHAWISHI.

Ili kuwatumia watu wenye ushawishi kufikia wateja wengi zaidi, zingatia mambo haya ya muhimu.

1. Chagua kwa usahihi.

Kuchagua watu sahihi wenye ushawishi ni hatua muhimu kuzingatia ili kunufaika na njia hii. Siyo kila mtu mwenye wafuasi wengi anafaa kutumika kufikia watu wengi. Unapaswa kuchagua mtu ambaye wafuasi wake ndiyo aina ya wateja unaowalenga.

Kama biashara yako inalenga vijana, unahitaji mtu mwenye ushawishi zaidi kwa vijana. Kadhalika wanawake na makundi mengine.

Kwa aina ya wateja unaowalenga, angalia watu wenye ushawishi ambao wafuasi wao wengi ni aina ya wateja unaowalenga.

2. Chagua njia ya ushawishi.

Njia za kuwashawishi watu kwa kutumia watu wenye ushawishi huwa zinatofautiana. Mtu mwenye ushawishi anaweza kuonekana anatumia kile unachouza au kukitangaza moja kwa moja. Njia ya kutumia huwa na nguvu ya kuwafanya watu wajue uwepo wa kitu wakati njia ya kutangaza moja kwa moja inaleta mauzo zaidi.

Chagua njia ya ushawishi kulingana na matokeo unayotaka kupata kwenye kutumia njia hiyo.

SOMA; Tumia Vyombo Vya Usafiri Kufikia Wateja Wengi Zaidi.

3. Amua njia ya malipo.

Watu wenye wafuasi wengi huwa wana gharama pale unapowatumia kuwafikia watu wengi zaidi. Malipo yanaweza kuwa ya moja kwa moja au ya kamisheni kulingana na mauzo. Njia ya malipo ya moja kwa moja ni nzuri pale lengo linapokuwa ni kujulikana. Lakini njia ya kamisheni ni nzuri pale lengo linapokuwa kufanya mauzo zaidi.

Kulingana na matokeo unayokuwa unataka kupata na bajeti unayokuwa nayo, chagua aina ya washawishi na njia sahihi ya malipo ili kuleta matokeo yenye tija zaidi.

4. Kuwa na njia ya kuwakusanya wateja tarajiwa.

Watu wengi wanapotumia watu wenye ushawishi, huwa hawakusanyi wateja tarajiwa na kuwaingiza kwenye biashara. Hilo linawafanya mara zote kuendelea kuwategemea hao wenye ushawishi na gharama kuwa kubwa.

Unapotumia njia hii ya watu wenye ushawishi hakikisha unakuwa na njia ya kukusanya taarifa za wateja wanaopatikana kupitia wao ili kuendelea kuwafikia hao moja kwa moja bila ya kuendelea kutegemea hao wenye ushawishi.

5. Tumia watu wanaokutana na watu wengi.

Japokuwa hawa siyo wenye ushawishi wa moja kwa moja, bali ni watu ambao shughuli zao zinawakutanisha na watu wengi. Kukutana kwao na watu wengi huwa wanaulizwa maswali mbalimbali na wale wasiojua. Unachotaka ni pale wanapoulizwa maswali yanayohusiana na biashara yako basi wawaelekeze watu hao kwako. Kisha wewe unawapa zawadi au kamisheni kulingana na mauzo yaliyofanyika.

Popote ulipo, jenga mahusiano mazuri na watu wanaokutana na watu wengi kama watu wa saluni, hoteli na migahawa, vyombo vya usafiri kama teksi, bajaji na bodaboda n.k.

Usakaji unahusisha watu hivyo popote penye watu ni fursa ya kupatumia kujulikana na wengi zaidi. Kwa chochote unachouza, tafuta watu wenye ushawishi kwa wateja unaowalenga kisha shirikiana nao kuweza kuwafikia watu wengi zaidi.

Zingatia haya uliyojifunza kwenye somo hili ili kutumia vizuri watu wenye ushawishi na kuwafikia watu wengi zaidi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.