3448; Kilicho rahisi zaidi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu huwa tunapenda urahisi kwenye mambo mengi.
Pale kunapokuwa na njia mbili mbele yetu, moja rahisi na nyingine ngumu, huwa tunachukua ile ambayo ni rahisi.

Lakini kumbe urahisi tunaoangalia siyo wa kitu chenyewe, bali wingi wa watu wanaochukua njia hiyo.
Yaani tunaona njia ni rahisi kama watu wengi wanaituata njia hiyo.
Hata kama kuna njia nyingine bora zaidi, huwa tuna amani zaidi kuwa kwenye njia ya wengi.

Kukosea ukiwa peke yako inauma kuliko kukosea ukiwa ndani ya kundi kubwa. Mkikosea wengi mnaonekana tatizo siyo lenu. Lakini ukikosea peke yako, unaonekana ujuaji wako ndiyo umekuponza.

Hilo limekuwa chanzo cha wengi kukosea kwa kufuata mkumbo kuliko kuwa sahihi wakiwa peke yao.
Imefanya wengi kuchagua njia ngumu inayofuatwa na wengi, kuliko njia rahisi ambayo mtu angekuwa peke yake.

Tuangalie mfano mmoja rahisi sana,
Unadhani kipi ni rahisi kati ya kupata ajira mpya au kupata mteja mpya?
Vyote hivyo ni vyanzo vya kipato, lakini havilingani kwenye ugumu na urahisi wake.

Utakubaliana na mimi kwamba kupata mteja mpya ni rahisi kuliko kupata ajira mpya. Lakini bado watu wengi wanahangaika na kutafuta ajira kuliko kujenga biashara au kufanya mauzo.

Tukiwa kwenye mfano huo huo, kipi rahisi kati ya kuwa na watu wengi wanaokulipa kidogo kidogo na kuwa na mtu mmoja anayekulipa kiasi kikubwa?
Iko wazi, wengi wanaokulipa kidogo ni rahisi na bora kuliko mmoja anayekulipa kikubwa.

Unakuwa kwenye hatari kubwa zaidi kwa kutegemea mmoja au wachache kwenye kuingiza kipato kuliko kuwategemea wengi.

Mifano ni mingi, kipi rahisi kati ya kufanya unachopenda au usichopenda?
Mara zote inakuwa rahisi wewe kufanya kile unachopenda.
Lakini wengi wanafanya vitu wasivyopenda, kwa sababu wamelaghaiwa na wengine kuamini hivyo ndiyo sahihi zaidi.

Ukijisikiliza wewe mwenyewe, maisha yako yanakuwa rahisi na utaweza kufanya makubwa zaidi.
Ukiwasikiliza wengine  maisha yako yatakuwa magumu na utashindwa kufanya makubwa zaidi.
Maisha ni yako na uchaguzi ni wako, chagua kwa usahihi.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe