Rafiki yangu mpendwa,

Tasnia ya elimu ya maendeleo binafsi imetawaliwa na maarifa chanya juu ya mafanikio.

Imekuwa inafundishwa na kusisitizwa watu kufikiri chanya ili kuweza kuchukua hatua na kupata mafanikio makubwa. Hiyo ni kwa sababu mtazamo hasi ndiyo kikwazo namba moja kwa watu kufanikiwa.

Lakini licha ya msisitizo huo wa watu kufikiri chanya na hata watu kufikiri chanya kweli, bado mafanikio makubwa yamekuwa ni kitu kigumu kwa walio wengi.

Wengi wanaianza safari ya mafanikio wakiwa na chanya, wenye shauku kubwa sana. Wanaanza kuchukua hatua kubwa, lakini haiwachukui muda wanakata tamaa na kuishia njiani.

Hapo ndipo unapojiuliza ule uchanya ambao watu wanakuwa wameanza nao unakuwa umepotelea wapi?

Ukichunguza kwa ndani, unagundua ule uchanya ambao watu wamekuwa nao ndiyo umepelekea washindwe. Hiyo ni kwa sababu kwa kuwa chanya, wanaamini kwamba mafanikio yatakuwa rahisi kwao.

Lakini uhalisia ni tofauti kabisa, mafanikio ni magumu sana. Kusema mafanikio ni magumu siyo kuwa hasi, bali ni kukubaliana na uhalisia ambao upo.

Lakini tukienda mbele zaidi, kwenye safari ya mafanikio lazima mtu atashindwa sana. Mtu atakutana na maanguko mbalimbali kabla hajafanikiwa. Hilo tunaliona kwa wote ambao wameshafanikiwa na litatokea kwa wale ambao hawajafanikiwa.

Watu wamekuwa wanakwepa huu uhalisia wa kwamba mafanikio ni magumu na watashindwa na kuamua kujificha kwenye kivuli cha kufikiri chanya.

Haijalishi unafikiri chanya kiasi gani, hutabadili uhalisia kwamba mafanikio ni magumu na utashindwa.

Kikubwa ambacho kukataa kwako uhalisia kitakuathiri ni kukata tamaa haraka pale unapokutana na magumu. Kwa sababu wewe ulishachukulia mafanikio ni rahisi na hakuna kushindwa, unapokutana na huo uhalisia unaona siyo njia sahihi kwako na hivyo unaacha.

SOMA; Tahadhari! Mafanikio Siyo Kile Kinachoonekana.

Yaani iko hivi, kama unaamini mafanikio ni rahisi na hakuna kushindwa, unapochukua hatua na ukashindwa, unaona kuna kitu hakipo sawa. Na hilo linapelekea wewe uache kitu hicho na kwenda kwenye kingine. Huko unakoenda pia mambo yanakuwa hayo hayo.

Ukikubaliana na uhalisia kwamba mambo ni magumu na utashindwa, pale unapokutana nayo, unajua ni sehemu ya safari. Huachi na kwenda kwenye mambo mengine, kwa sababu unajua hata ukienda huko, mambo ni hayo hayo.

Hivyo basi rafiki yangu, ninachotaka kukushawishi hapa siyo uache kuwa hasi na uwe chanya, bali kukubaliana na uhalisia. Kuwa chanya sana, lakini usikatae uhalisia jinsi ulivyo. Badala yake kubaliana na uhalisia na utumie kupata kile unachotaka.

Pale unapokutana na magumu na kushindwa kwenye safari yako ya mafanikio, usikimbie kwa kuona mambo hayapo sawa. Badala yake kubali ni sehemu ya safari ya mafanikio na yavuke ili uweze kupata kile unachotaka.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini, nimefafanua kwa kina jinsi ya kuwa chanya na kukubaliana na uhalisia wa ugumu wa safari ya mafanikio. Karibu ujifunze na kuchukua hatua ili uweze kufanikiwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.