Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Hii dunia imekuwa na watu wengi na inaendelea kuwa na watu wengi. Lakini katika watu hao wengi waliopo na watakaokuja kuwepo hapa duniani, hakuna hata mmoja anayefanana na wewe kwa kila kitu.
Hata watu waliozaliwa mapacha wa kufanana, bado hawafanani kwa kila kitu. Kila mtu ana upekee wake ambao haupatikani kwa mtu mwingine. Kama ambavyo tumekuwa tunatumia vidole gumba kwenye utambulisho mbalimbali, ndivyo kila mmoja ana utofauti na upekee wake.
Utofauti na upekee ambao mtu anao, ndiyo pia wenye nguvu ya kufanya makubwa na ya tofauti kabisa. Kila mtu anao uwezo wa kufanya mambo ambayo hakuna mtu mwingine anaweza kuyafanya. Hilo linatokana na uwezo wa kipekee ambao upo ndani ya kila mtu.

Pamoja na utofauti huo na uwezo wa kipekee, bado watu wengi wamekuwa wanaishi maisha ya kawaida, yanayofanana na ya watu wengine na kushindwa kujenga mafanikio makubwa. Sababu kubwa inayopelekea wengi kubaki na hali duni licha ya kuwa na uwezo mkubwa ni kuiga wengine na kufuata mkumbo.
Zoezi la kuiga wengine na kufuata mkumbo huwa linaanzia kwenye mazoea ya jamii ya kuwalinganisha na kuwashindanisha watu. Tangu tukiwa watoto wadogo tumekuwa tunalinganishwa na kushindanishwa na wengine. Kwenye kila kitu, mtu ulikuwa unaambiwa mbona wenzako wanafanya hivi au vile. Shuleni wote mlipewa mtihani wa aina moja na kisha kupewa matokeo nani amefaulu na nani amefeli.
Pamoja na tofauti kubwa ambayo wanafunzi wanakuwa nayo, bado kipimo cha ufaulu kimekuwa kinapimwa kwa mtihani wa aina moja. Anayefaulu mtihani anaambiwa anaweza na anayefeli anaambiwa hawezi. Mara nyingi wale ambao wanashindwa mitihani ya darasani huwa wanakuwa na uwezo mkubwa kwenye mambo mengine kama michezo, sanaa, ubunifu n.k. Lakini kwa sababu mitihani ya darasani haina uwezo wa kupima vitu hivyo, wanaonekana hawana uwezo na kuamini hivyo kwa miaka yao yote.
Nje ya mfumo wa elimu, jamii imekuwa inawalinganisha na kuwashindanisha watu kwa hatua wanazopiga. Kwenye kila hatua ya maisha, umekuwa unalinganishwa na watu wengine. Unaambiwa mbona wenzako wameshafanya hivi au vile na wewe hujafanya. Hilo linakusukuma wewe uhangaike kufanya yale ambayo wengine wanafanya, hata kama hayana tija kubwa kwako.
Hali hii ya kulinganishwa na kushindanishwa na wengine imekuwa ndiyo kaburi la ndoto kubwa ambazo watu wengi wanazo. Watu wamekuwa wanazika ndoto zao kubwa ili tu waweze kuendana na maisha ya kijamii. Matokeo yake ni watu kuwa na maisha ambayo hawayafurahii hata kama kwa nje wanaonekana kufanikiwa.
Ili uweze kuwa muuzaji bora, ni lazima kwanza uwe mtu bora. Na ili uweze kuwa mtu bora ni lazima uwe halisi kwako na siyo kuiga wengine na kufuata mkumbo. Unapaswa kutambua utofauti na uwezo wa kipekee ulio ndani yako na kuutumia kufanya makubwa sana ambayo hakuna mwingine anayeweza kuyafanya.
Kuishi maisha halisi kwako na kufanya makubwa, zingatia yafuatayo;
1. Sikiliza Sauti Yako Ya Ndani.
Kila mmoja wetu huwa ana sauti ya ndani yake ambayo inamwambia anapaswa kufanya nini na kuwa mtu wa aina gani. Sauti hiyo ya ndani ndiyo wewe halisi, ambaye hujaharibiwa na wengine. Sauti hiyo ya ndani huwa haipotei, inaweza kunyamazishwa, lakini haipotei kabisa. Ukianza kuisikiliza sauti hiyo, itakuelekeza kila unachopaswa kufanya na kuwa.
Hatua ya kuchukua; sikiliza sauti yako ya ndani ambayo inakuambia nini unapaswa kufanya na kuwa kwenye kila hali. Achana na kelele za nje zinazokupoteza, fuata sauti ya ndani ambayo ni mwongozo sahihi.
2. Ondoka Kwenye Sanduku Ambalo Umewekwa.
Jamii imekuweka kwenye sanduku fulani na haitaki uondoke kwenye hilo sanduku. Tayari wanakuchukulia wewe ni mtu wa aina fulani, tayari imekuambia nini unaweza na nini huwezi. Jamii inataka ubaki kwenye sanduku hilo kwa miaka yako yote. Huwezi kufanya makubwa kama utaendelea kuwa vile ambavyo jamii inataka uwe. Ni lazima uwe tayari kuvunja hilo sanduku ambalo jamii imekuweka na uwe huru kuyaishi maisha yako kwa namna ya kipekee kwako. Uzuri ni tayari unajua nini unapaswa kufanya tofauti, fanya hivyo.
Hatua ya kuchukua; acha kujichukulia vile ambavyo jamii inakuchukulia, usikubali kile ambacho wengine wanakuambia unaweza au huwezi. Badala yake fanya yale unayotaka kufanya kutoka ndani yako, hayo ndiyo yanakufanya kuwa tofauti.
SOMA; Kuwa Na Usimamizi Mzuri Wa Fedha Binafsi Ili Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
3. Tambua na tumia uwezo, vipaji na uzoefu wa kipekee ulionao.
Kila mtu ana uwezo na vipaji vya kipekee, ambavyo havipo kwa watu wengine. Pia kwa kipindi chote ambacho mtu ameishi, kuna uzoefu wa kipekee ambao ameweza kuupata. Kwa kuchanganya uwezo, vipaji na uzoefu ambao mtu amepata, anaweza kufanya kitu ambacho hakuna mwingine anayeweza kufanya. Kwa kuzingatia hayo, mtu hawezi kushindwa na mwingine yeyote, kwa sababu hakuna aliye na vitu alivyonavyo yeye.
Hatua ya kuchukua; jitambue ni vitu gani unaweza kufanya kwa utofauti, jua vipaji ulivyonavyo na changanya na uzoefu ambao umeshakuwa nao mpaka sasa. Kwa kuleta vitu hivyo pamoja, utaweza kufanya kitu ambacho hakuna mwingine anayeweza kufanya.
4. Usiogope Kushindwa na Kuonekana Wa Tofauti.
Utakapochagua kuyaishi maisha ya tofauti na wengine, utashindwa na kuonekana wa tofauti. Kushindwa ni hatua za mwanzo, kwa sababu unafanya kitu ambacho hujakizoea. Kwa kufanya vitu hivyo ambavyo havijazoeleka, wengi watakuona wewe ni wa tofauti. Unapaswa kupokea hilo kama sehemu ya safari yako na kutoruhusu likukwamishe. Unapaswa kutambua kwamba kushindwa ni pale unapoacha kabisa kufanya au unapowaiga wengine. Kwa kuwa mkweli kwako, mafanikio ni lazima.
Hatua ya kuchukua; tambua kwamba kushindwa na kuonekana wa tofauti itakuwa ni tafsiri ya wengine kwako, lakini hiyo haipaswi kuwa tafsiri yako. Huwezi kushindwa kwa kuwa wewe, hivyo mara zote kazana kuwa wewe.
5. Endelea Kuwa Bora Kila Wakati.
Haijalishi una uwezo na vipaji vikubwa kiasi gani, unao wajibu wa kuviendeleza. Kitu chochote ambacho hakiendelezwi huwa kinadumaa. Kwa kipindi kirefu umekuwa unaishi kwa kushindana na kuiga wengine. Ule upekee wako umedumaa na kukosa nguvu. Unapaswa kuufufua kwa kujiendeleza wewe mwenyewe. Ndiyo maana ni muhimu sana kila wakati kuendelea kujifunza na kuchukua hatua kuwa bora zaidi. Yale yote unayofanya, yafanye kwa ubora wa hali ya juu sana. Epuka mazoea na ukawaida, kila wakati kazana kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa hapo nyuma.
Hatua ya kuchukua; kuwa mtu wa kujifunza kwa uendelevu, kamwe usibweteke na kuona tayari unajua na unaweza kila kitu. Kwa kila hatua ambayo umefikia, unaweza kwenda hatua ya juu zaidi. Shindana na wewe mwenyewe, kwa kuhakikisha unaimaliza kila siku ukiwa bora kuliko ulivyoianza. Ukiliweza hili, lazima utakuwa bora na kufanikiwa sana.
Rafiki yangu muuzaji, mwanasayansi Albert Einstein amewahi kunukuliwa akisema; “Kila mtu amezaliwa ana akili, lakini kama utampima samaki kwa uwezo wa kupaa angani, ataishi maisha yake yote akijiona ni mjinga.” Je umekuwa unajiona mjinga kwa kuhangaika na mambo gani ambayo yako nje ya uwezo wako? Jitambue sasa kwa kujua vipaji na uwezo wa kipekee ulionao na kuvitumia kuwa mtu bora na kufanya mauzo makubwa.
Kwa kila uwezo na vipaji ulivyonavyo, vitumie kwenye mauzo unayofanya na utaweza kujitofautisha na wauzaji wengine wote na kufanya mauzo makubwa. Usihangaike kushindana na wengine au kufuata mkumbo, kuwa halisi kwako na utafanya makubwa kuliko wengine. Kumbuka hakuna anayeweza kukushinda wewe kwa kuwa wewe. Hapo ndipo nguvu na upekee wako ulipo, utumie vizuri.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.