Habari njema matajiri wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya programu ya NGUVU YA BUKU, programu inayoendeshwa kwa msingi kwamba KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI na kupitia programu hii tunatekeleza hilo kwa vitendo.

Kwa kuwa umeingia kwenye safari hii ya kujenga utajiri na uhuru wa kifedha, huwezi tena kuiangalia fedha kama ulivyokuwa unafanya huko nyuma.

Huko nyuma ulikuwa unachukulia fedha poa, hasa fedha ambazo ni ndogo ndogo. Ulikuwa unatumia tu bila ya kufikiria, kwa kuona ni fedha ambazo hazina nguvu au matokeo makubwa kwako.

Lakini sasa umejifunza na kuona jinsi ambavyo fedha ndogo ndogo unazopoteza ukizitumia vizuri unaweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako. Umeona jinsi ambavyo uwekezaji wowote unaofanyika kwa muda mrefu unazalisha utajiri mkubwa.

Na kama programu yetu inavyoitwa NGUVU YA BUKU, fedha ndogo ndogo, kuanzia shilingi elfu moja ina nguvu ya kujenga utajiri. Kwa kila fedha unayoishika, ni mbegu ya kujenga utajiri mkubwa. Lakini mbegu hiyo itakuwa na manufaa kama itapandwa kwenye eneo sahihi na siyo kuliwa.

Tofauti ya wanaojenga utajiri na wanaobaki kwenye umasikini huwa siyo kipato, bali jinsi wanavyotumia kipato hicho. Kwenye maeneo mengi, wale wenye kipato kidogo au cha kati huwa wanaweza kujenga utajiri mkubwa kuliko wale wenye kipato kikubwa. Hiyo ni kwa sababu wenye vipato vikubwa huwa wanajikuta wakiwa na matumizi makubwa pia.

Ili kujenga utajiri mkubwa kupitia uwekezaji mdogo mdogo wa muda mrefu, unapaswa kubadili sana mtazamo wako kwenye kila fedha inayopita kwenye mikono yako.

Tumeshajifunza kwamba kwa kila kipato unachoingiza, sehemu yake unapaswa kuweka pembeni kwa ajili ya uwekezaji. Kiasi kinachoshauriwa ni asilimia 10, lakini mtu anaweza kufanya kiasi kingine kulingana na hali yake. Kwa ambaye amebanwa sana na hawezi asilimia 10 anaweza kuanza na kiasi kidogo. Na kwa ambaye hana majukumu mengi, anapaswa kwenda zaidi ya hiyo asilimia 10.

Pamoja na kiwango hicho cha kuondoa kwenye kila kipato chako, kuna mianya mingine mingi ya kuweza kuweka akiba na kuwekeza zaidi kupitia kipato cha ziada ambacho mtu unaingiza.

Kipato hicho cha ziada kinaweza kutokana na malipo ya ziada ambayo mtu unakuwa umeyapata au kiasi cha fedha unachokuwa umeokoa kutokana na matumizi fulani.

Kwenye kipato cha ziada, hapo unapata fedha ambayo hukuwa unategemea kupata. Labda umepewa zawadi fulani ya fedha kutokana na vitu ambavyo umefanya. Au hata umeokota fedha, kitu ambacho hakikuwa kwenye hesabu zako za fedha.

Kwenye kuokoa fedha kutokana na matumizi, hapa unakuwa umepata punguzo kwenye manunuzi ambayo ulikuwa umepanga kufanya au kupata zawadi ambayo inaokoa kufanya matumizi ya aina fulani.

Kila mtu huwa anakutana na hizi fursa za kupata kipato ambacho hakikuwa kwenye mipango yake. Lakini wengi wamekuwa wanaishia kutumia vibaya kipato hicho cha ziada na kushindwa kunufaika nacho.

Kwa kuwa upo kwenye programu hii ya NGUVU YA BUKU na umedhamiria kujenga utajiri na uhuru wa kifedha, kila fedha yoyote ya ziada unayoipata unapaswa kuipeleka moja kwa moja kwenye uwekezaji.

Kila unapopata fedha ambayo haikuwa kwenye mahesabu na mipango yako, hapo hapo ipeleke kwenye uwekezaji. Jizuie haraka sana kuanza kuiwekea mipango fedha ambayo hukuwa na mipango nayo. Hata kama kuna mahitaji fulani uliyokuwa nayo, usione fedha uliyopata ndiyo mkombozi wako. Badala yake endelea na mikakati yako mingine kwenye kutatua yale unayopitia.

Kila fedha inayokuja kwako na haikuwa na mipango uliyoweka tangu mwanzo, peleka yote kwenye uwekezaji. Hapo utakuwa unakuza uwekezaji wako na kufikia uhuru wa kifedha mapema.

SOMA; STAAFU NA UHURU WA KIFEDHA.

Pamoja na fedha zinazokuja kwako zenyewe, unapaswa kuchukua hatua za makusudi za kupata fedha za ziada kwenye kila siku yako. Na kila fedha ya ziada unayoweza kupata kila siku, peleka yote kwenye uwekezaji.

Baadhi ya hatua unazoweza kuchukua kila siku ili kuingiza kipato cha ziada ni kama ifuatavyo;

1. Fanya kazi au biashara yako kwa viwango vya juu sana kiasi cha watu kusukumwa kukushukuru kwa kukupa zawadi mbalimbali. Watu huwa wanathamini vitu vizuri, unapofanya vizuri, watu wanakupa zawadi na wewe utageuza zawadi hizo kuwa fedha na kuwekeza.

2. Punguza matumizi ambayo umekuwa unafanya kwa kujirudia rudia kila siku lakini maisha yako hayawezi kukwama hata ukiacha matumizi hayo. Mifano ni gharama kubwa unazoweza kuwa unatumia kwenye mawasiliano, usafiri, chakula n.k. Punguza kitu kimoja ambacho unakilipia kila siku na hiyo fedha peleka kwenye uwekezaji.

3. Kwenye kila manunuzi unayofanya, omba punguzo. Hata kama ni eneo ambalo unaambiwa hakuna punguzo kabisa, wewe omba punguzo. Jenga hoja nzuri na kwa ushawishi kwa nini unastahili kupewa punguzo. Kwa kuwa vizuri kwenye mapatano, utashangaa jinsi ambavyo utapata punguzo kwenye maeneo mengi ambayo watu wengine hawapati punguzo. Kila kiasi unachookoa kwenye punguzo, kiwekeze moja kwa moja.

4. Jicheleweshe kufanya matumizi ambayo yana muda wa kufanya. Kwenye matumizi ya lazima unayopaswa kufanya, huwa kuna muda wa kufanya hivyo. Huenda ni malipo ambayo unapaswa kufanya na kuna miezi mitatu mbele ya kufanya hivyo. Unaweza kuona kulipa mapema inakupa utulivu, lakini kama kuna muda wowote mbele yako, utumie kuchelewesha kufanya malipo. Hapo unatenga kabisa fedha ya kufanya malipo hayo, lakini hulipi mapema, badala yake unaiwekeza kwanza iendelee kukuingizia faida hata kidogo kidogo na wakati wa kulipa unapofika unaitoa fedha hiyo na kufanya malipo. Hata kama utapafa faida ndogo, bado ina manufaa kuliko kutokupata kabisa.

5. Uza vitu vyote ambavyo unavyo na hujavitumia kwa zaidi ya miezi sita. Binadamu huwa tuna tabia ya kukusanya vitu ambavyo hatuvitumii, tukiamini siku moja tutakuwa na uhitaji navyo. Matokeo yake ni kukalia fedha ambazo zingeweza kuwa zinatuingizia faida hata kama ni kidogo. Jikague ni vitu gani unavyo na hujavitumia kabisa kwa zaidi ya miezi sita kisha viuze na upate fedha za kuwekeza. Anza na nguo ulizonazo ambazo hujavaa kwa miezi sita kisha nenda kwenye vitu vingine, iwe ni vitu binafsi au ambavyo umekuwa unatumia kwenye shughuli zako. Angalia kila kitu kama fedha ambayo haikuingizii faida na hakikisha unapata njia ya kupata fedha hiyo na kuiwekeza.

Kama ambavyo tumejifunza hapa, bado tunazo fursa nyingi za kuingiza kipato cha ziada na kufanya uwekezaji mkubwa zaidi. Chukua hatua kwenye haya uliyojifunza ili uweze kunufaika na kufanya uwekezaji mkubwa.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili, kama sehemu ya kuthibitisha umesoma, umeelewa na unaenda kuchukua hatua ili kufikia uhuru wa kifedha.

1. Kwenye kazi au biashara unayofanya, ni huduma gani ya kipekee unayoweza kuitoa na ukajitofautisha sana na wengine kiasi cha watu kupenda kufanya kazi na wewe na kukupa zawadi mbalimbali? Unawekaje huo upekee na utofauti ili watu waweze kukupa zawadi hizo?

2. Ni matumizi gani ambayo umekuwa unayafanya kila siku, ambayo unaweza kuacha kuyafanya na maisha yako yasiathirike sana? Kwenye matumizi hayo unaweza kuokoa kiasi gani kila siku?

3. Ni vitu gani ambavyo unavyo na hujavitumia kabisa kwa kipindi cha miezi sita iliyopita? Shirikisha mpango wako kwenye kuviuza au kuvikodisha kwa wengine ili upate fedha ya ziada ya kuwekeza.

4. Je huwa unaomba punguzo kwenye kila kitu? Kama ndiyo umekuwa unapata matokeo gani? Na kama siyo nini kimekuwa kinakukwamisha? Shirikisha mpango wako wa kuwa unaomba punguzo kwenye kila manunuzi.

5. Shirikisha maeneo ambayo umekuwa unafanya malipo mapema kuliko muda unaohitajika na jinsi unavyoweza kutenga malipo unayopaswa kufanya lakini kusubiri mpaka muda ufike, huku ukiwekeza malipo hayo na kupata faida hata kama ni kidogo.

6. Karibu uulize swali au kutoa maoni na mapendekezo kwenye somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.

Shirikisha majibu ya maswali haya kwenye mjadala wa somo hili, huo ndiyo uthibitisho wa kushiriki kwenye programu hii kikamilifu.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.