3450; Kuwa, Fanya, Pata.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu anataka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yake.
Lakini ni wachache sana wanaoyapata mafanikio makubwa kadiri ya wanavyotaka.
Siyo kwa sababu wachache hao ndiyo pekee wenye uwezo wa kufanikiwa.
Bali kwa sababu ndiyo wanaokuwa wanajua namna sahihi ya kupata mafanikio wanayoyataka.
Wengi ambao hawafanikiwi huwa wanafikiri inabidi wapate kwanza kile wanachotaka, ndiyo wawe wamefanikiwa na kufanya yale wanayotaka.
Hivyo wanatanguliza KUPATA kisha KUWA na hatimaye kufanya.
Mpangilio huo umekuwa haufanyi kazi kwa sababu kilichotangulizwa siyo sahihi.
Ni sawa na kuweka mkokoteni mbele ya punda badala ya nyuma yake.
Mpangilio sahihi ambao umewaletea watu mafanikio makubwa unaanza na KUWA, kisha KUFANYA na hatimaye KUPATA.
Mtu anaanza kuwa vile anavyotaka kuwa akiwa ameshafanikiwa, kisha anafanya yale waliofanikiwa wanafanya na hilo linamwezesha kupata hayo mafanikio wanayokuwa wanataka.
Kwa kuanza na KUWA, akili ya ndani inavuta kwa mtu fursa mbalimbali zinazoendana na kile anachokuwa.
Kwa kufanya, mtu anazitumia fursa zinazojitokeza kuzalisha matokeo mazuri.
Hayo yanapelekea mtu kupata anachotaka, kama ataendelea kuwa na kufanya kwa muda mrefu bila kuacha.
Amua ni mtu wa aina gani unayetaka kuwa ili maisha yako yawe ya mafanikio.
Jua mpangilio wa siku nzima wa aina hiyo ya mtu pamoja na mafunzo na hatua unazopaswa kupiga.
Kisha chagua kuishi kwa namna hiyo kila siku kwa miaka bila ya kuacha.
Hata kama mafanikio yatachelewa, kitendo cha kuishi vile ambavyo utaishi ukiwa umefanikiwa, inakupa hali kubwa ya kuridhika.
Tambua hii siyo sawa na kuigiza mafanikio ili kuyapata (fake it till you make it). Bali ni kuyaishi mafanikio yenyewe, hata kabla hujayafikia.
Inakuwa rahisi zaidi kwako kuyafikia mafanikio kama utaanza kuyaishi kabla hata hujayafikia.
Na hilo ni rahisi kama utaujua mchakato sahihi wa mafanikio unayoyataka kisha kufuata mchakato huo kwa msimamo bila kuacha.
Kitu kingine kitakachokupa ushindi wa uhakika kwenye hili ni kuweza KUWA na KUFANYA kwa muda mrefu zaidi kuliko wengine wote.
Wengi huwa wanaianza hii safari lakini wanaishia njiani, hasa pale matokeo yanapochelewa.
Wewe usiwe kama hao wengi, endelea kuwa na kufanya kwa muda mrefu zaidi hata kama huyaoni matokeo.
Hakikisha tu mchakato wako ni sahihi na nenda ukiboresha.
Matokeo mazuri na makubwa yatakuja yenyewe kwa wakati wake.
Anza kwa KUWA yule unayemtaka,
Kisha FANYA yale unapaswa kufanya,
Na utaweza KUPATA kila unachotaka.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe