3456; Kipaji na kazi.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio yana mchango kutoka pande kuu mbili.
Upande wa kwanza ni wa KIPAJI.
Huu ni upande unaowakilisha yale yote ambayo mtu anazaliwa nayo.
Kuanzia uwezo wa kipekee ulio ndani ya mtu na vipaji ambavyo mtu anavyo.
Huu ni upande ambao mtu huwezi kuubadili, ni una kitu au huna.
Upande huu wa kipaji kila mtu anao, japo wengi huwa hawaujui upande huu kwao wenyewe.
Wanaishia kuyaendesha maisha yao bila ya kutumia uwezo wa kipekee na vipaji vilivyo ndani yao.
Matokeo yake ni wanaishia kuwa na maisha ya kawaida, wakati wangeweza kujijengea mafanikio makubwa sana.
Upande wa pili ni wa KAZI.
Huu ni upande unaowakilisha juhudi zote ambazo mtu anaweka kwenye kuyajenga mafanikio yake.
Kuanzia matamanio makubwa ambayo watu wanakuwa nayo, juhudi za kazi ambazo wanaweka mpaka ung’ang’anizi wao kwenye kupata kile wanachotaka.
Huu ni upande ambao mtu anaweza kuubadili vile anavyotaka, siyo vitu vya kuzaliwa navyo ambavyo ni unakuwa navyo au kutokuwa navyo.
Upande huu wa kazi kila mtu anaweza kuufanyia kazi kadiri ya anavyotaka yeye mwenyewe.
Huu ni upande ambao kila mtu anaweza kuuongeza kwa ukubwa na kupata matokeo ambayo ni makubwa zaidi.
Upande huu unampa kila mtu fursa ya kutengeneza mafanikio makubwa bila ya kujali anaanzia wapi.
Ni kwa kuongeza zaidi juhudi kwenye huu upande ndiyo mtu anaweza kuzalisha matokeo makubwa na ya kipekee kabisa.
Huwezi kujijengea vipaji vipya, lakini unaweza kujitengenezea matamanio makubwa zaidi, ukaongeza juhudi kubwa kwenye kazi na kuwa na ung’ang’anizi zaidi.
Ni kwa kuongeza hayo ambayo yapo ndani ya uwezo wako na kuyasimamia kwa uhakika ndiyo unaweza kujihakikishia mafanikio makubwa.
Mjadala wa KIPAJI na KAZI huwa umetawala sana kwenye sanaa na michezo.
Huwa kuna wasanii na wachezaji ambao wana uwezo na vipaji vikubwa na wanafanya vizuri.
Halafu kuna wasanii na wachezaji ambao uwezo na vipaji vyao ni vya kawaida, ila wanaweka juhudi kubwa sana kwenye kazi na kuwa na ung’ang’anizi, kitu ambacho kinawapa mafanikio makubwa kuliko hata wale wenye uwezo na vipaji vikubwa.
Kuanzia sasa usisingizie tena uwezo na vipaji kama kikwazo kwako kufanikiwa.
Badala yake angalia upande wa kazi ambao upo ndani ya udhibiti wako.
Mara zote ongeza juhudi za kazi unayoweka, weka kwa ukubwa zaidi na kuwa na ung’ang’anizi usiovunjwa na chochote.
Ukiwa tayari kuweka juhudi kubwa ya kazi na ukawa na ung’ang’anizi ambao hauvunjwi na chochote, hakuna kinachoweza kukuzuia kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
Iwe una uwezo na vipaji au huna, ukifanyia kazi upande wa kazi, utapata mafanikio makubwa.
Unawajibika kwa mafanikio yako mwenyewe. Fanyia kazi upande wa kazi na hakuna kitakachokushinda.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe