Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Ili uweze kufanya mauzo makubwa, ni lazima uwe muuzaji bora.
Ili kuwa muuzaji bora, ni lazima uwe mtu bora.
Na ili uweze kuwa mtu bora, lazima ujitambue wewe mwenyewe.
Kujitambua wewe mwenyewe kunahusisha kujua haiba yako, ambayo ni tabia zako za ndani na jinsi unavyofanya mambo yako.
Haiba huwa ndivyo mtu ulivyo na huwa haibadiliki kirahisi. Pamoja na kujifunza na kuchukua hatua, haiba ya mtu huwa inabaki vile vile, kwa sababu ndivyo alivyo.
Njia bora ya kunufaika na haiba ni kujua haiba yako kisha kuitumia vizuri kupata kile unachotaka kwenye maisha.

Huwa kuna njia mbalimbali za kupima haiba za watu, lakini inapokuja kwenye kazi, biashara na mauzo, mfumo wa DISC PERSONALITY PROFILE ndiyo wenye manufaa zaidi.
Mfumo wa DISC PERSONALITY unagusa maeneo makubwa manne yanayomjenga mtu ambayo yanaunda kifupisho cha DISC. Maeneo hayo ni Dominant, Influence, Steadiness na Conscientiousness. Kwa kuchukua herufi ya kwanza ya kila neno ndiyo unapata kifupisho cha DISC.
Hapo chini ni sifa za kila eneo katika hayo manne na vitu ambavyo mtu anakuwa anataka kwenye kila eneo.
HAIBA YA UTAWALA (DOMINANT);
Sifa;
1. Wanyoofu (Direct).
2. Wafanya maamuzi (Decisive).
3. Wenye nia (Determined).
4. Kuchukua hatari (Risk taker).
5. Kutatua matatizo (Problem solver).
Wanachotaka;
1. Kuheshimiwa.
2. Machaguo.
3. Udhibiti.
HAIBA YA USHAWISHI (INFLUENCE)
Sifa;
1. Shauku (Enthusiasm).
2. Kuchangamana na wengine (Interactive).
3. Ubunifu (Imaginative).
4. Kusukumwa na hisia (Emotional).
5. Watu wa mitoko (Outgoing).
Wanachotaka;
1. Kukubalika na kutambulika.
2. Umaarufu.
3. Ukaribu na watu.
HAIBA YA UTULIVU (STEADINESS)
Sifa;
1. Imara (stable/steady).
2. Watulivu (reserved).
3. Kutopenda mabadiliko (resistance to change).
4. Kutabirika (predictable).
5. Uaminifu (loyal).
Wanachotaka;
1. Usalama.
2. Msimamo.
3. Kukubalika.
HAIBA YA UTIIFU (CONSCIENTIOUSNESS)
Sifa;
1. Watiifu (compliant).
2. Waangalifu (Careful).
3. Wachambuzi (analytical).
4. Wenye uwezo (competent).
5. Kutafakari (contemplative)
Wanachopenda;
1. Usahihi (accuracy).
2. Uthibitisho (confirmation).
3. Ubora (excellence).
SOMA; Epuka Mashindano Na Kufuata Mkumbo Ili Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
KUTATHMINI HAIBA YAKO.
Kujua haiba, unapaswa kuchagua maeneo mawili ambayo yanaendana na wewe zaidi na kuyafanyia kazi hayo.
Usakaji unataka mtu kuwa na haiba ya Ushawishi na Utiifu. Ushawishi unamsaidia msakaji kuwafikia watu wengi zaidi huku Utiifu ukimwezesha kuwachambua kwa usahihi wale wenye sifa za kuwa wateja tarajiwa.
Ukamilishaji unataka mtu kuwa na haiba ya Utawala na Ushawishi. Utawala unamsaidia mkamilishaji kuweza kukamilisha mauzo kwa kuwaelekeza wateja hatua wanazopaswa kuchukua. Ushawishi unawafanya waweke mbele maslahi ya wateja badala ya kujiangalia wao tu kwenye kukamilisha mauzo.
Uhudumiaji unataka mtu kuwa na haiba ya Utulivu na Utiifu. Utulivu unawafanya kuwa waaminifu na kuaminika na wateja, huku utiifu ukiwawezesha kuwahudumia vizuri wateja na kuwa waangalifu.
Ijue haiba yako kwa kujua maeneo mawili yanayoendana na wewe zaidi kisha jiboreshe kwenye maeneo hayo. Ukishajua haiba yako, fanyia kazi yale maeneo ambayo una uimara ili uweze kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Badala ya kukazana kuboresha maeneo ambayo una udhaifu, boresha maeneo ambayo tayari una uimara. Ukiboresha madhaifu unaishia kuwa na madhaifu makubwa zaidi na hivyo kukwama zaidi. Lakini ukiboresha maeneo ambayo tayari una uimara, unakuwa imara zaidi na kupata matokeo bora.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.