3457; Unaogopa mafanikio.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kadiri ya unavyotaka sana kufanikiwa, vipi kama nikikuambia kinachokukwamisha usifanikiwe ni woga wako kwenye mafanikio?
Ndiyo, namaanisha kabisa kwamba wewe mwenyewe huwa unajizuia kufanikiwa kwa sababu unayaogopa mafanikio.
Na dalili namba moja kwamba unayaogopa mafanikio ni tabia yako ya kughairisha mambo.
Rafiki, hivi unafikiri kwa nini ukae chini na kuweka mipango kabisa, halafu wakati wa kutekeleza unapofika unaamua kughairisha.
Huoni kwamba kuna kitu hakipo sawa hapo?
Unaweza kudhani unaghairisha kwa sababu ya ugumu wa kile unachopaswa kufanya.
Lakini mara nyingi unapoghairisha kufanya ulichopanga, huwa unaishia kufanya mengine ambayo ni magumu zaidi, japo yanakuwa siyo muhimu.
Kwa hiyo hapo tunaona dhahiri kwamba kughairisha ni kuhofia matokeo makubwa yanayoweza kutokea.
Na unajua ukishaweza kupata matokeo hayo makubwa, huwezi tena kutoa sababu na visingizio.
Unajua ukishaweza kufanya mara moja, utahitajika uendelee tena kufanya, kitu ambacho huenda una uvivu nacho.
Japo tunayapenda mafanikio, lakini ni magumu na yanakuja na wajibu mkubwa.
Tunapofikiria uwajibikaji unaokuja na mafanikio makubwa, tunaweza kuona bora kubaki kwenye ngazi za chini za kuridhika tu.
Na ukishakuwa mtu wa kuridhika na ngazi za chini, kamwe huwezi kupiga hatua kwenda ngazi za juu.
Kila mara utakuwa unaahirisha yale uliyopanga, siyo kwa sababu huwezi, bali kwa sababu hutaki uwajibikaji mkubwa.
Kila unapopanga kufanya vitu na ukapata wazo la kughairisha, jikamate na kujiuliza nini hasa unachoogopa kwenye mafanikio.
Ni bora uukabili ukweli kuliko kujidanganya kwamba unataka mafanikio wakati kwa ndani unayaogopa.
Kama umechagua kufanikiwa, ondokana na kila aina ya hofu uliyonayo juu ya mafanikio na fanya kama ulivyopanga.
Kubali kuwajibika na utaweza kufanya makubwa sana.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe