3471; Wakati wake bado.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna mambo ni sahihi kabisa kuyafanya, lakini manufaa yake yatategemea ni wakati gani umeyafanya.

Yaani unaweza ukafanya mambo kwa wakati fulani ukafanikiwa, halafu ukarudia kufanya mambo hayo hayo kwa wakati mwingine ukashindwa.

Kwa mfano, maisha ya mafanikio yanahitaji sana mtu uwe na mlinganyo sahihi. Utoe vipaumbele kwa mambo mengi ambayo yote ni muhimu.
Lakini hilo litakuwa na manufaa kwako kama tayari umeshajenga mafanikio.

Kama bado hujajenga mafanikio, kuwa na mlinganyo ni kujidanganya na kujipoteza. Kwa sababu hakuna matokeo makubwa yanayoweza kuzalishwa kwa kufanyia kazi vipaumbele vingi kwa wakati mmoja.

Mafanikio makubwa yanataka mtu uweke kila kitu chako kwenye eneo moja mpaka lilete matokeo.
Ukitawanya tu umakini na rasilimali zako, unaishia kupata matokeo ya kawaida ambayo ni kushindwa tu.

Kwa maana hiyo basi, ili ujenge mafanikio makubwa, unahitaji kukosa mlinganyo na usawa kwenye maisha yako kwa kipindi fulani.
Halafu ukishayapata mafanikio, unapaswa kuwa na mlinganyo sahihi ili uweze kuyatuna na kudumu nayo kwa muda mrefu.

Kwenye safari yako ya mafanikio usiangalie usahihi wa kile unachofanya pekee.
Badala yake angalia na usahiui wa wakati ambao unafanya kitu hicho.
Fanya kitu sahihi, mahali sahihi na kwa wakati sahihi.
Hivyo ndivyo mafanikio makubwa yanavyojengwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe