Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.

Kitu kikubwa sana ambacho kila biashara inahitaji ili kuwafikia wateja wengi zaidi na mara kwa mara ni sababu ya msingi ya kuwafikia wateja hao. Kama ambavyo tumeshajifunza, zipo njia nyingi za kuwafikia wateja, kuanzia kukutana nao ana kwa ana, kuwapigia simu, kuwatumia jumbe na hata kutumia mtandao.

Njia za kuwafikia tayari zipo, kinachobaki ni sababu za kuwafikia. Kwa sababu mara nyingi ukiwafikia wateja moja kwa moja, hasa pale wanapokuwa hawakujui au hawana uhitaji, kukataliwa huwa ni kwa nafasi kubwa. Lakini pale wateja wanapokuwa wanakujua au wana uhitaji, huwa wanakupokea vizuri zaidi.

Kwa mkakati wetu wa CHUO CHA MAUZO wa kutengeneza wateja mara zote na kuwafuatilia kwa msimamo bila kuacha, hatuwezi kusubiri mpaka wateja watujue au wawe na uhitaji ndiyo tuwafikie. Hivyo tunalazimika kutafuta sababu nyingine zitakazotupa uhalali wa kuendelea kuwafikia wateja.

Moja ya sababu tunazoweza kuzitumia kuwafikia wateja mara kwa mara bila ya kupata mapingamizi makali ni sikukuu na siku maalumu.

MATUMIZI YA SIKUKUU KUWAFIKIA WATEJA.

Siku za sikukuu ni zile ambazo zina matukio yanayojulikana na watu wote na hivyo unaweza kuzitumia kama njia ya kuwafikia wateja. Sikukuu zinaweza kuwa za kidini, kijamii, kisiasa n.k. Sikukuu huwa zinakuwa na mapumziko kwa watu wote, hata kama mtu hahusiki moja kwa moja.

Kwa kuwa sikukuu zinawagusa watu wote, ni sababu nzuri ya kuwafikia wateja, kupitia kuwapa salamu za sikukuu hizo. Uzuri ni kwamba hakuna mtu anayeweza kukataa salamu za sikukuu pale unapomtumia, zaidi ni wengi huwa wanafurahia.

Pale watu wanapopokea salamu za sikukuu, huwa wanazingatia na kufurahia zoezi hilo. Hapo biashara inakuwa imepata nafasi ya kuwafikia wateja na kuendelea kukumbukwa.

Kila biashara inapaswa kutumia sikukuu zilizopo kuwafikia wateja kwa mara ya kwanza na hata kuendelea kuwafuatilia. Hilo linafanyika kupitia kutuma jumbe kwa njia mbalimbali kwenye siku hizo za sikukuu.

Uzuri ni kwamba karibu kila mwezi huwa kuna sikukuu ambayo inaweza kutumika kuwafikia wateja. Kwa mfano kwa nchi ya Tanzania, zifuatazo ni sikukuu zilizopo kwenye kila mwezi.

Januari kuna sikukuu za mwaka mpya na mapinduzi.

Februari kuna sikukuu ya wapendanao.

Machi kuna sikukuu ya pasaka, japo hii wakati mwingine huenda Aprili.

Aprili kuna sikukuu ya Karume.

Mei kuna sikukuu ya wafanyakazi.

Juni kunaweza kuangukia sikukuu ya Eid.

Julai kuna sikukuu ya sabasaba.

Agosti kuna sikukuu ya nanenane.

Oktoba kuna sikukuu ya Nyerere.

Disemba kuna sikukuu za uhuru na krismasi.

Hapo ni zile sikukuu kubwa na zenye mapumziko, bado kuna sikukuu nyingine ndogo ndogo ambazo zipo kwa wingi na watu wanazifuatilia.

Kwa uwepo wa sikukuu hizi, tunaona kabisa kwamba biashara inaweza kuwafikia wateja mara kwa mara bila ya kuwachosha. Kwa sababu kinachohitajika ni kuwapelekea tu wateja salamu za sikukuu.

SOMA; Usakaji Na Ufuatiliaji Wa Wateja Kwa Kutuma Ujumbe Wa Simu Kwa Watu Wengi.

MATUMIZI YA SIKU MAALUMU KUWAFIKIA WATEJA.

Umewahi kupata salamu za siku yako ya kuzaliwa kutoka kwenye mitandao ya simu unayotumia. Ulijisikiaje pale ulipopokea ujumbe ukikutana jina lako na kukutakia heri ya siku yako ya kuzaliwa?

Najua ulijisikia vizuri sana. Swali ni je unadhani kwenye huo mtandao kuna mtu anazingatia siku za kila mteja na kuandaa ujumbe wa kumtumia? Jibu ni hapana, hakuna mfanyakazi yeyote kwenye mtandao wa simu unaotumia anayejua kuhusu siku yako ya kuzaliwa. Lakini wana mifumo ambayo inatumia taarifa zilizopo kuwatumia wateja jumbe mbalimbali.

Mifumo hiyo ndiyo imetumia taarifa za siku yako ya kuzaliwa kukutumia ujumbe wa siku hiyo. Licha ya kwamba ujumbe uliopokea ulitokana na mfumo, bado ulijisikia vizuri na kuona mtandao huo unakujali.

Siku ya mtu ya kuzaliwa ni siku muhimu sana ambayo huwa anaikumbuka na wengi kuisherekea kwa njia mbalimbali. Ukiweza kujua kuhusu siku hiyo kwa wateja wako ni sababu nyingine nzuri ya kuweza kuwafikia.

Matukio maalumu ni yale ambayo yana maana kwa watu na ukiweza kuyatumia unaweza kuwafikia na wakaona unajali. Baadhi ya matukio hayo ni kama ifuatavyo;

1. Siku ya mtu ya kuzaliwa.

2. Kumbukizi ya matukio muhimu kwenye maisha ya mtu, mfano ndoa.

3. Siku za kuzaliwa za watu muhimu kwenye maisha ya mtu.

4. Siku ambazo mtu amepata ushindi fulani na kustahili pongezi.

5. Siku ambazo mtu amepata changamoto fulani na kustahili pole.

Siku maalumu zinategemea mteja mmoja mmoja na hivyo kuhitajika kuwafuatilia wateja kwa karibu na kuwa na taarifa zao nyingi.

Uzuri wa siku maalumu ni kwamba huwa zina maana kubwa kwa wateja, hivyo zinapotumika kuwafikia, wanaona wanajaliwa sana. Kwa biashara kuwafikia wateja kwa salamu mbalimbali kwenye siku zao maalumu, watu hao wanaona biashara inawajali sana na wao kuijali pia.

Kama wauzaji, tuna wajibu wa kukusanya taarifa nyingi za wateja wetu na kuzitumia vizuri kuwafikia wateja hao ili kupokelewa vizuri na kuwa na ushawishi.

MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE KUTUMIA SIKUKUU NA SIKU MAALUMU KUWAFIKIA WATEJA.

Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia kwenye kutumia sikukuu na siku maalumu kuwafikia wateja ili kupokelewa vizuri, kukumbukwa na kuwa na ushawishi.

1. Zijue siku zote za sikukuu na maalumu kwa wateja wako mapema ili kuwa na maandalizi mazuri ya kuwafikia.

2. Andaa ujumbe mzuri ambao utautuma kwa wateja kwenye siku hizo. Ujumbe uwe ni wa salamu, ambapo unataja sikukuu au siku hiyo maalumu, unakuwa na jina la mteja na la biashara na mawasiliano.

3. Kwa siku ambazo ni maalumu sana ka wateja, kuwapigia simu au kukutana nao ana kwa ana ina nguvu zaidi kuliko kutumia ujumbe pekee.

4. Biashara inaweza kuandaa matukio maalumu kwenye siku hizo za sikukuu na siku maalumu. Kwa siku za sikukuu, matukio yanakuwa yanayowahusu watu wote. Na kwa siku maalumu matukio yanakuwa yanahusu mteja mmoja mmoja.

5. Kutoa zawadi kwenye sikukuu na siku maalumu ni njia nyingine ya kuwafikia wateja na kuendelea kukumbukwa.

6. Kama biashara ina wateja au watu wengi wa kuwafikia, matumizi ya mifumo ya kutuma ujumbe kwa watu wengi (BULK SMS) unapaswa kutumika kurahisisha zoezi hilo.

Kwa biashara na wauzaji, hatupaswi kupoteza fursa nzuri ya sikukuu na siku maalumu kuwafikia wateja. Ni vigumu kukataliwa na wateja au kuonekana msumbufu pale unapotumia siku hizo kuwafikia wateja. Kuwa na ratiba ya sikukuu zote zilizopo kwenye miezi yote ya mwaka na zitumie kuwafikia wateja. Na kwa mteja mmoja mmoja, jua siku zao maalumu na kuzitumia kuwapelekea salamu zitakazowafanya waikumbuke biashara na kuona inawajali.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.