3483; Usiwatukane wanaokuamini.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya sababu zinazowazuia watu kufanikiwa ni kuwatukana wale wanaowaamini.

Kabla hujasema hii haikuhusu kwa sababu huwa hutukani watu, nikutake utulie hapo hapo, kwa sababu umekuwa unalifanya hilo sana.

Kukosa kwako nidhamu ni matusi makubwa sana kwa watu ambao wamekuamini.
Ni kama umewaambia; “Nyie watu hamna akili kabisa, mnamwaminije mtu kama mimi?”

Ni matusi makubwa sana kuwaahidi watu utafanya kitu halafu usikifanye kama ulivyoahidi. Watu walikuamini kwenye hiyo ahadi yako, kutokuitimiza ahadi hiyo ni matusi makubwa sana kwao.

Ni dharau ya hali ya juu sana kuchelewa kwenye kitu ambacho watu wanakutegemea ufanye kwa wakati. Kuwafanya wengine wakusubirie wewe ni kuwaambia kwamba wao hawana maana yoyote.

Ni kujishushia hadhi yako pale unapofanya chini ya mategemeo ambayo watu wanayo kwako. Ni kuwaambia hawajui namna ya kuchagua watu sahihi wa kujihusisha nao.

Unaweza kuona mambo haya ni madogo, lakini unapoyafanya kwa kurudia rudia kwa muda mrefu, madhara yake yanakuwa makubwa sana.

Watu wanapunguza imani yao kwako kidogo kidogo mpaka inafika hatua ambayo huaminiki kabisa hata useme au kufanya nini.

Na ukishafika hatua hiyo ya kutoaminika ndiyo unakuwa umejichimbia kaburi linalozika mafanikio yako.

Hatua muhimu sana ambayo itakupa mafanikio ni kuwaheshimu sana wale wote ambao wamekuamini.

Wale wote wanaokukubali kwenye kitu chochote kile, waheshimu na kuwajali sana.

Unafanya hivyo kupitia kuwa na;

Moja ni viwango vya hali ya juu sana. Jiwekee viwango vya hali ya juu kwenye mambo yote unayojihusisha nayo na pambana kukamilisha kwa viwango hivyo.

Mbili ni nidhamu kali sana ya kuahidi na kutekeleza, bila kutoa sababu zozote. Wafanye watu wawe na amani kwenye ahadi zako, kwa mara zote kuzitimiza hata kama itakugharimu kiasi gani.

Tatu ni kujitoa kweli kwenye chochote unachofanya kwa kuweka umakini wako wote kwenye kitu hicho na kukifanya kwa uhakika. Usiwe mtu wa kugusa vitu juu juu.

Nne ni kuwa mtu wa kuzalisha matokeo ya uhakika, ambayo watu hawawezi kuyapata mahali pengine isipokuwa kwako. Watu wanapenda matokeo, unapowapa hayo, wanakuamini.

Tano ni neno lako liwe sheria na mkataba wako iwe ni kushikana mikono. Wafanye watu wayaamini maneno yako kwa sababu ni ya kweli mara zote. Pia mnapokubaliana jambo na watu, hata kama ni kwa kushikana mikono tu, chukulia huo kama mkataba wenye masharti makali ambao kamwe huwezi kuuvunja.

Jenga hiyo nidhamu ya viwango hivyo na utaaminiwa na wengi, kitu kitakachokupa mafanikio makubwa.
Yote hayo yapo ndani ya uwezo wako mwenyewe, chukua hatua kuhakikisha unapata mafanikio unayotaka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe