Hivi tajiri mkubwa duniani ama nchini akija kwako na kukwambia ana ‘dili’ la hela nyingi sana, na yuko tayari kukupa hela yoyote unayotaja wewe kama tu utaweza kumtimizia hitaji lake. Anakwambia kwamba amepimwa na kugundulika moyo wake hauwezi kufanya kazi kwa muda mrefu hivyo anahitaji kuwekewa moyo mwingine haraka iwezekanavyo, anakuuliza kama uko tayari kutoa moyo wako na atakupa hela utakayotaka. Je utamjibu nini? Je utamwambia akupe kiasi gani cha hela? Pamoja na shida nyingi ulizonazo bado utakataa kuutoa moyo wako. Hii inaonesha kwamba uhai wako ni wa thamani sana na hakuna beio unayoweza kuweka juu ya uhai wako. Kama uhai wako ni wa thamani sana je unaupa mwili wako thamani ya kutosha? Unaijali afya yako kwa kiwango cha kutosha?
Wengi wetu huwa tunachukulia afya zetu kimzaha sana, yani hatupo makini kabisa na afya zetu. Tunakula hovyo, hatufanyi mazoezi, hatujikingi na magonjwa na mbaya zaidi hatupimi afya zetu.
Afya ni mali yenye thamani sana kwenye maisha yetu. Wengi tunazijua kanuni za afya na kila siku zinasemwa kupitia vyombo mbalimbali. Kwa kifupi ili kuwa na afya njema ni lazima kufanya yafuatayo.
1. Kula mlo kamili wenye virutubisho vyote vinavyhitajika mwilini kwa kiwango kinachohitajika, usipunguze wala usiongeze.
2. Fanya mazoezi mara kwa mara ili kuweka mwili katika hali ya ukakamavu na pia kupunguza virutubisho vilivyozidi kama mafuta.
3. Pima afya mara kwa mara, kuna vitu huwezi kuviona kama vinashida mara moja kwani huchukua muda kujulikana. Kwa mfano shinikizo la damu, sukari, na maambukizi mbalimbali.
4. Jiepushe na mazingira hatarishi ambayo yanayeza kuathiri afya yako, kaa kwenye mazingira safi.
5. Usitumie sumu zinazoweza kudhuru afya yako kama madawa ya kulevya, uvutaji wa sigara na dawa zozote ambazo hujashauriwa kitaalamu.
6. Fanya starehe kwa kiasi, kama unatumia vileo tumia kwa kiasi.
7. Pata mapumziko ya kutosha, pata usingizi wa kutosha. Ili mwili uweze kufanya kazi vizuri lazima mwili upate mapumziko ya kutosha, usifanye kazi kupita kiasi.
8. Jikinge na msongo wa mawazo, epuka mambo yanayokusababishia msongo wa mawazo.
Hizo ni baadhi tu ya kanuni za afya ambazo ukizifuata afya yako itakuwa katika hali nzuri. Kila mtu anazijua ila tatizo liko kwenye kuzitekeleza. Weka malengo ya kuwa na afya bora na uwe na mpango wa kufikia malengo hayo. Afya yako ni muhimu sana kwako.