Kwa sasa ajira zimekuwa ngumu sana kupatikana, sio kwa Tanzania tu bali hii ni kwa dunia nzima. Pamoja na ugumu huu wa kupatikana kwa ajira bado wengi wetu tunafikiri ajira ni sehemu ya maisha yetu. Wengi wanafikiri kuajiriwa ni haki ya msingi na inabidi waipate haki hiyo.
Zamani sana kabla ya mapinduzi ya viwanda hakukuwa na ajira. Watu walitumia nguvu, uwezo na vipaji vyao kujipatia mahitaji yao. Walioweza kuwinda waliwinda, walioweza kutengeneza vitu vya sanaa walifanya hivyo na wengi walikuwa wakulima. Kuna waliolima kwenye mashamba yao wenyewe na kuna wengine walilima kwa wenye mashamba makubwa.
Kipindi hiko hakukuwa na ajira rasmi, hakuna aliekuwa anakwenda kazini na mwisho wa mwezi kulipwa. Waliokuwa wanafanya kazi kwenye mashamba kwa kuipwa walikuwa wanalipwa kama vibarua tu.
Karne ya 18 na 19 yalitokea mapinduzi makubwa ya viwanda yaliyoanzia ulaya na kusambaa amerika na baadae dunia nzima. Baada ya mapinduzi ya viwanda ndipo hizi ajira rasmi zilipozaliwa.
Kwa nini ajira zilishamiri baada ya mapinduzi ya viwanda?
Baada ya kuona kutumia vibarua ingekuwa ngumu kukuza viwanda vyao, wamiliki wa viwanda walitafuta njia ya kupata watu wa kuwafanyia kazi kwa kipindi kirefu. Hivyo taratibu ulianza kukua mfumo wa ajira ambapo walitoa vitu mbalimbali vya kuwashawishi watu kuingia kwenye ajira. Baadhi ya vitu hivyo ilikuwa mishahara mizuri, malipo baada ya kustaafu na vingine vingi.
Vitu hivyo vilifanya watu waone ajira ndio mkombozi na kuzifurahia sana. Wenye viwanda walifaidika sana huku wafanyakazi wakiendelea kuishi maisha ya kawaida ya mshahara baada ya mshahara. Sumu hii ya ajira ilisambaa na mpaka sasa imewafanya watu wafikiri ajira ndio njia rahisi ya kukabiliana na maisha.
Japokuwa ajira zilikuwa za manufaa sana kipindi cha mwanzo sasa hivi zimekuwa mzigo kwa waajiriwa na pia zimekuwa chache kuliko idadi ya wanaotaka kuajiriwa. Hii imetokana na mapinduzi makubwa ya teknolojia ambayo yamepunguza sana idadi ya watu wanaohitajika kufanya kazi. Mashine nyingi zilizogunduliwa kipindi cha sasa zimechukua nafasi kubwa ya rasilimali watu. Mashine kama computer na ‘robots’ zimerahisisha sana kazi viwandani na hata maofisini.
Kabla hujafikiri ajira ni sehemu ya maisha yako ama ni haki yako kuajiriwa ni vyema ukaelewa ajira zililetwa ili kuwarahisishia baadhi ya watu kukuza ndoto zao. Na pia elewa siku zinavyozidi kwenda ndivyo ajira zinavyozidi kuwa ngumu hivyo usitegemee sana kwenye ajira.