Kila mtu ana malengo kwenye maisha yake(kama huelewi kama una malengo soma hapa). Na ili kuweza kuyafikia malengo hayo ni lazima kuwa na mipango. Kuna wakati mtu unakuwa na mipango mizuri sana ila utekelezaji unakuwa mgumu sana.
Unakuwa na mpango wako mzuri ila kila unapotaka kuanza unahisi kama hujajipanga vya kutosha ama unaona mafanikio unayotaka kufikia ni makubwa sana. Kwa kuona mafanikio ni mkubwa sana inakufanya uone mipango uliyoweka ni kidogo sana kuyafikia. Hivyo unajikuta muda unakwenda na hakuna cha maana ulichofanya ili kuweza kufikia malengo yako.
Hali kama hiyo haitokei kwako tu, inatokea kwa kila mtu na hali hii ndio inatofautisha wanaofanikiwa kufikia malengo yao na wanaoshindwa kufikia malengo waliyojiwekea. Kuna tofauti gani kati ya wanaoshindwa na wanaoweza kuyafikia malengo yao?
Wanaoshindwa kufikia malengo yao hukubaliana na nafsi zao kwamba malengo waliyoweka huenda ni makubwa sana na mipango waliyoweka haitoshi kuwafikisha kwenye malengo yao. Hivyo kuamua kuacha na kuweka maleng mengine ambayo hali inaweza kuwa ile ile, na mwisho wa siku kujikuta hakuna lolote alilowahi kupanga likafanyika.
Wanaoweza kufikia malengo yao wanaelewa kwamba malengo yao ni makubwa na ili kuyafikia ni lazima kufanya jambo kila siku au kila mara kuwafikisha kwenye malengo yao. Mtu yeyote aliefanikiwa kwenye jambo lolote amefanya jambo hilo mara kwa mara ama kila siku kwa muda mrefu. Amefanya mambo madogo madogo kwa kurudia rudia mpaka alipofikia malengo aliyojiwekea.
Hata jambo liwe gumu kiasi gani ukiweza kulifanya kila siku inakuwa tabia yako na mwishowe hutumii nguvu kutaka kufanya jambo hilo. Ukiweza kujijengea tabia ya kufanya kitu fulani cha kukufikisha kwenye malengo yako kila siku basi inakuwa tabia yako na hutohitaji nguvu nyingi kuendelea kukifanya. Inakuwa ni sehemu ya maisha yako na unajisiki furaha kufanya.
Kila siku unasafisha kinywa chako(kupiga mswaki), iwe subuhi au jioni kuingana na utaratibu wako. Ila kuna siku umewahi kujiulizauliza kama upige mswaki ama la? Si moja kwa moja tu ukiamka unajua lazima upige mswaki. Hutumii nguvu yoyote kujilazimisha kupiga mswaki. Hivi ndivyo inavyokuwa kwa tabia ama jambo lolote unalofanya kila siku. Unakuwa utaratibu wa maisha na ni rahisi sana kufikia malengo yako.
Kwa mfano kama unataka kujifunza kutengeneza program za computer, ama unataka kuwa mwandishi. Kwa kutenga saa moja kila siku la kucheza na codes za program ama kuandika ni zaidi ya masaa 300 kwa mwaka. Kama ukiweza kufanya kila siku na ikawa tabia yako, masaa 300 ni mengi sana kwa chochote utakachotaka kujifunza.
Cha msingi ni kutokuacha kufanya, yaani hakikisha huachi kufanya unachotaka kufanya ili ufanikiwe. Kama jinsi ambavyo hujawahi kuacha kupiga mswaki, vivyo hivyo usiache kufanya unachotakiwa kufanya ili kuyafikia malengo yako.
Unaweza kufanya chochote unchoweza kufikiri. Usitishwe na ukubwa wa ndoto ama ukubwa wa mafanikio. Weka mipango na fanya jambo kila siku a kukufikisha kwenye malengo yako.