Ijumaa ni siku ya furaha sana kwa wengi na jumatatu ni siku ya huzuni kubwa. Kila inapofika ijumaa unafurahia sana kwa kuwa mapumziko yanakaribia. Na kila jumatatu unahuzunika sana maana kazi zinaanza.

furahi dei

  Hali hii ya furaha na huzuni inakurudia kila wiki kwa sababu hujajua jinsi ya kupangilia siku zako za mwisho wa wiki. Kama ukiweza kupangilia vizuri siku zako za mwisho wa wiki utazifurahia sana na utaweza kuyafikia malengo yako kama ulivyopanga.

  Kuna mambo mengi sana unayoweza kuyafanya kwenye siku za mwisho wa wiki na ukazifurahia sana. Hapa kuna mambo muhimu matano ambayo ukiyafanya kila mwisho wa wiki utapata furaha kubwa na utayafikia malengo yako vizuri.

1. Pata muda wa kupumzika. Katika siku mbili za mapumziko ya mwisho wa wiki hakikisha unapata muda wa kupumzika. Hata kama umejiajiri na huna mapumziko ya mwisho wa wiki, tafuta japo masaa matano ya kupumzika kabisa na kutofanya chochote kinachohusiana na kazi unazofanya. Kwa kupumzika unajiondolea uchovu na msongo wa mawazo unaotokana na kazi unazofanya.

2. Endeleza vipaji vyako. Mara nyingi kazi unayoifanya sio kipaji chako. Kutokana tu na harakati za maisha umejikuta unafanya unachofanya ila kipaji chako ni kingine kabisa. Kama ukiweza kutenga muda kwenye mwisho wa wiki na kukiendeleza kipaji chako utanufaika sana. Unaweza kuendeleza kipaji chako kwa kujifunza ama kufanya kabisa.

3. Tenga muda wa familia na marafiki. Kutokana na majukumu ya maisha na mihangaiko ya kila siku ni vigumu sana kupata muda wa kutosha kukaa na familia ama marafiki. Tenga muda wa kuwa karibu na uwapendao na mwisho wako wa wiki utakuwa na furaha sana kwako.

4. Weka mipango ya wiki inayofuata na baadae. Ni vizuri kuwa na utaratibu wa kuweka na kupitia mipango yako mbalimbali kila mwisho wa wiki. Kabla mapumziko ya mwisho wa wiki hayajisha hakikisha wiki inayokuja umeipanga vizuri na unajua siku gani unafanya nini. Hii itakufanya usiichukie siku ya jumatatu asubuhi.

5. Jichanganye na kuza mtandao wako. Pia unaweza kutumia mapumziko ya mwisho wa wiki kujichanganya na watu tofauti tofauti na kukuza mtandao wako. Unaweza kujichanganya kwa kuongea na watu mbalimbali ambao wanafanya kazi tofauti na unazofanya ama kwa kutembelea sehemu mbalimbali zinazokuwa na watu wa aina tofauti tofauti. Kwa njia hii utajuana na watu wengi na wanaofanya shughuli tofauti tofauti.

  Mambo mengine unayoweza kufanya mwisho wa wiki ni kufanya mazoezi ya viungo, kujisomea, kujitolea kwa shughuli mbalimbali na kwenda matembezini.

  Panga na tumia vyema mapumziko yako ya mwisho wa wiki ili uweze kuyafurahia maisha yako.

  Je wewe huwa unafanya nini mwisho wa wiki? Tushirikishe kwa kuweka maoni yako hapo chini.